Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe.
WATAALAM wa kilimo mkoani Songwe wametakiwa kuendelea kusimamia suala la kuhuisha orodha ya wakulima kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku pamoja na kudhibiti vitendo vya utoroshaji wa mbolea hiyo ya nje ya nchi.
Maelekezo hayo yalitolewa Oktoba 23, 2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Katibu Tawala huyo yupo kwenye ziara ya siku nne katika Halmashauri hiyo ya Mbozi, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara za kutembelea halmashauri zote za Mkoa Songwe kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za serikali.
Seneda amesema kuwa ni muhimu wataalam wa kilimo kuendelea kusimamia na kuhuisha orodha ya wakulima katika mfumo wa ruzuku ya mbolea ili kuwa na taarifa sahihi za wakulima wanaostahili kupata mbolea hiyo kwa Mkoa huo.
“Wakati tunelekea kwenye msimu wa kilimo niombe wataalam kuendelea kusimamia uhuishaji wa orodha ya wakulima ikiwemo kudhibiti utoroshaji wa mbolea yetu ya ruzuku,kama mnavyojua nchi za wenzetu wanaotuzunguka hawana ruzuku kwenye mbolea hivyo ni vizuri tukadhibiti ili mbolea yetu yote ya ruzuku itumike hapa ndani,” amesisitiza Seneda.
Amewataka wataalam hao wa kilimo kutoa taarifa sahihi kwa wakulima juu ya mwenendo wa hali ya hewa na mazao yanayostahili kulimwa ili kuongeza hali ya uzalishaji wa chakula.
Pia wataalam hao wametakiwa kupanga taratibu nzuri za kuwatembelea wakulima mara kwa mara na kuwapa mbinu bora za kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija.
Hivi karibuni akiwa Mkoani Songwe , Waziri wa Kilimo Husein Bashe akizungumza na wadau wa kilimo amesema Mkoa wa Songwe ndio unaongoza nchini kwa kuhujumu na wizi wa mbolea ya ruzuku ambapo kwa sehemu kubwa vitendo hivyo hufanywa na watendaji wa serikali wakishirikiana wafanyabiashara.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi