Na Agnes Alcardo, Timesmajira online, Dar
WASIMAMIZI wa ujenzi wa makambi ya bomba la mafuta wahimizwa kutekeleza ujenzi wa mradi kwa kuzingatia ufanisi, usawa, utekelezaji wa mradi kwa wakati na kuzingatia fursa kwa wazawa.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta katika kambi namba 15 iliyopo Handeni na 16 iliyopo Muheza mkoani Tanga.
Akizungumza na Meneja ujenzi kutoka kampuni ya EACOP, Patton Trevor Makame alipongeza namna mradi unavyotekelezwa kwa kuzingatia ufanisi, utaalam na muda ambavyo vyote vinaleta matuamaini katika utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta.
“TPDC ni m-bia kwenye utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta kwa ushiriki wa asilimia 15 ambapo tumeendelea kulipa mchango wetu kwenye mradi kwa wakati na kwasababu hiyo ni jukumu letu kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake hivyo msisite kuwasilisha changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha utekelezaji wa ujenzi wa mradi ili kupatia ufumbuzi kwa wakati bila kiuathiri ujenzi,”.
Pia Makame amewahimiza wakandarasi waliopo katika maeneo ya ujenzi kuzingatia masuala ya fursa za kazi kwa wazawa wakiwemo wa maeneo yanayozunguka mradi ili kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na uwepo wa mradi wa EACOP.
Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa kambi namba 15 na 16 Meneja Ujenzi wa mradi huo Patton Trevor, ameeleza kuwa kambi namba 16 inakamilisha shughuli za ujenzi za mwanzoni unaotekelezwa na kampuni ya wazawa ya JV Sperk ambayo inategemewa kukabidhi eneo la ujenzi wa kambi kwa kamapuni ya CPP mwanzoni mwa Februari.
Aidha ameeleza kuwa kambi namba 15, tayari kazi za ujenzi imeanza na inaendelea vizuri, pamoja na hayo alieleza hali ya ajira katika kambi hizo ambapo, katika kambi namba 16 ina jumla ya wafanyakazi 207 ambao kati yao watanzania wako 206 na mgeni ni mmoja huku kambi namba 15 ina jumla ya wafanyakazi 136 kati ya hao watanzania 131 na wageni 35.
Aidha, Makame pamoja na kuangalia maendeleo ya ujenzi na kupata taarifa za ajira, alikagua huduma za dharura za afya katika kambi hizo ambapo amepongeza huduma ya afya upande wa vifaa tiba pamoja na uwepo wa madaktari wa huduma za dharura watatu kwa ajili ya kutoa matibabu ya dharura pale yanapohitajika.
Akitoa maelezo ya huduma ya afya ya dharura katika kambi namba 16, Daktari wa Dharura, Lunyalula Kasanda, alieleza kuwa chumba cha huduma ya dharura kimewekwa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya mgonjwa.
Ambapo pamoja na uwepo wa vifaa vingine ipo mitungi ya hewa ya oksijeni ambayo ina uwezo wa kutoa huduma hadi masaa 10 pamoja na uwepo wa gari ya wagonjwa iliyojitosheleza kwa vifaa tiba kwa ajili ya kuokoa maisha ya mgonjwa.
Akihitimisha ziara yake Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC amewataka wasimamizi na wafanyakazi wote kwa ujumla kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha ufanisi, ujuzi pamoja na kuzingatia muda unaohitajika kukamilisha kila hatua katika ujenzi wa kambi hizi.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua