Na Joyce Kasiki Timesmajira online,Mwanza
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) inaendelea kutekeleza kwa kasi mradi mkubwa wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji katika Jiji la Mwanza na maeneo ya jirani.
Mradi huu unahusisha ujenzi wa matenki matano ya kuhifadhi na kusambaza maji, ulazaji wa mabomba makuu ya kusafirisha maji pamoja na ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji (pump houses), kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa jiji hilo na viunga vyake.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano katika Mamlaka hiyo Vivian Temumesema matenki hayo yatakuwa yakipokea maji kutoka katika chanzo kipya cha uzalishaji maji kilichoko Butimba.
Amesema hatua hiyo inatarajiwa kunufaisha wakazi wengi, hususan wale wanaoishi maeneo ya pembezoni na yenye miinuko ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya huduma ya maji.
Aidha amesema,hadi kufikia sasa, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 35 ambapo matenki yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 31 yanajengwa katika maeneo ya Kagera – Lita Milioni 10,Kisesa – Lita Milioni 5,Fumagila – Lita Milioni 10,Nyamazobe – Lita Milioni 5 na Usagara – Lita Milioni 1.
Sambamba na hilo amesema , mtandao wa mabomba yenye urefu wa kilomita 40.5 unatarajiwa kulazwa kutoka vituo vya kusukuma maji vya Sahwa na Butimba hadi kwenye matenki hayo ambapo hadi kufikia sasa, jumla ya kilomita 13.7 za bomba tayari zimeshalazwa, huku kazi nyingine zikiendelea kwa kasi.
Kwa mujibu wa Temu,mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026, ambapo baadhi ya kazi — zikiwemo ulazaji wa bomba litakalopeleka maji kwenye tenki la Kisesa (ambalo tayari limekamilika) — zinatarajiwa kukamilika mapema, mwezi Machi 2026.
Utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wadau wa Maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Française de Développement – AFD). Mradi unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 450,000 wa Jiji la Mwanza na maeneo yanayolizunguka.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi,Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Waisa Werema ambaye eneo lake ni miongoni mwa maeneo yanayopitiwa na mradi huo, amepongeza hatua kubwa ya maendeleo ya mradi na kueleza kuwa tayari umeanza kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa huduma ya maji kwa wakazi wake.
Aidha, Werema ametoa pongezi kwa Serikali na kwa Mkurugenzi Mkuu wa MWAUWASA, Nelly Msuya, kwa ushirikiano mzuri na viongozi wa mitaa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina