November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene

Utata waibuka ununuzi magari Jeshi la Polisi

Na Angela Mazula,TimesMajira Online

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amejitosa kuanza kufuatilia sababu zilizokwamisha kutoletwa nchini magari 369 kati ya 777 yaliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya Jeshi la Polisi kwa miaka nane sasa.

Mkataba wa ununuzi wa magari hayo baina ya Serikali na Kampuni Ashok Leyland ulikuwa utekelezwe ndani ya mwaka mmoja, lakini imechukua miaka nane hadi sasa bila magari 369 kati ya 777 kukabidhiwa kwa mnunuzi.

Akizungumzia hilo jijin i Dar es Salaam, akiwa Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi wakati wa ziara yake ya siku nne ya kutembelea vikosi mbalimbali vya jeshi hilo, Waziri Simbachawene amesema hadi sasa ni magari 497 yaliyoletwa nchini ni .

Amesema, kati ya hayo magari 22 yalikuwa chini ya kiwango. “Tangu magari hayo yaangizwe ni muda mrefu sana, lazima ijulikane ni sababu gani zilichelewesha kuletwa kwa magari hayo,” amesema.

Amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kukaa kwa pamoja na timu zima ambayo iliyokuwa inashughulika na mikataba ya ununuzi wa magari hayo kujadiliana ili kujua hatima ya hayo magari 369 ambayo hayajaletwa nchini wakati tayari yamelipiwa.

Waziri Simbachawane ameagiza viongozi hao kuhakikisha kabla ya Bunge lijalo kuanza (mwezi ujao) muafaka kuhusiana na magari hayo uwe umepatikana.

“Ni lazima majibu yapatikane kutoka kwa mkandarasi aeleze magari hayo yanapatikana lini kwa sababu hili ni jambo la muda mrefu zaidi ya miaka saba au nane tangu kuingiwa mkataba huu,” amesisitiza.

Wakati huo huo ujenzi wa sehemu ya utunzaji na utengenezaji wa silaha hapa nchini umekamilika kwa asilimia 85 baada ya Serikali kutoa kiasi cha sh. milioni 666 kwa ajili ya matengenezo katika eneo hilo lililopo Kurasini Jijini Dar es Salam.

Akizungumza wakati wa ziara yake, Waziri Simbachawene amesema kwa sasa hali ya ujenzi inaendelea na kukamilia kwa zaidi ya asilimia 85 ambapo ni sehemu ya kuhifadhia, kupokea malighafi na kuzihifadhi malighafi.

Aidha Waziri amesema, baada ya ujenzi huo ukikamilika majengo ya zamani yatavunjwa kwa ajili ya kuanza kutumia majengo mapya, kwani ujenzi wake utakamilika siku za hivi karibuni.

“Bohari kuu ya polisi kwa hapa jijini Dar es Salaam wanafanya vizuri ila changamoto kubwa ipo katika vituo mbalimbali na kuweza kuanzisha vituo vingine sita vya ushonaji katika mikoa mbalimbali na kuondoa kabisa tatizo la sare kwa askari wote hapa nchini,”amesema.

Waziri amezitaka taasisi mbalimbali hapa nchini kupeleka maombi ya tenda kwa Polisi kwa ajili ya kushonewa sare mbalimbali kwani jeshi hilo lina uwezo mkubwa wa kushona na kusambaza nguo hizo kwa wakati kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato kwa jeshi hilo kupitia sekta hiyo.