March 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utata kifo cha mwanafunzi Janeth

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Kagera

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Kagera juu ya kifo cha   Janeth Mbegaya(8),mwanafunzi wa shule ya msingi Tumsime iliyopo Wilaya ya Muleba mkoani humo,aliyedaiwa  kufariki kutokana na kubakwa,kulawitiwa  na kuchomwa sindano ya sumu imekinzana   na ya wazazi wa marehemu huyo.

Ambapo baba mzazi wa Marehemu Enock  Mbegaya  ( 33 )mkazi wa Kijiji na Kata Kibanga wilayani Muleba,amesema mtoto wake alifariki Machi 10 mwaka huu akiwa hospitali ya Rubya.

Mbegaya,amedai kuwa familia ikiwa katika utaratibu wa kusafirisha mwili wa mtoto wao waliyejua kuwa kifo chake kimetokana na ugonjwa wa maralia, ghafla wakapokea taarifa iliyowashtua baada ya Daktari ambaye hawakujua jina lake, na kujitambulisha kwa familia kuwa hawaruhusiwi kuchukua mwili wa marehemu hadi kibali kutoka Jeshi la Polisi kwa sababu kifo cha mtoto huyo siyo cha kawaida.

‘’Kijana mmoja aliyejitambulisha kama daktari alituita wanafamilia  tulikuwa  watano,  akatueleza sababu ya kifo cha mtoto wetu ni kubakwa,kulawitiwa na kuchomwa sindano yenye sumu.Yeye ndiye aliyethibitisha kifo chake sio kama tunavyofikiria kuwa amekufa kutokana na maralia, amesema Mbegaya na kuongeza:

“Tukashangaa na kumuuliza mbona mlikuwa mnatueleza kuwa anaumwa maralia, akajibu  kuwa baada ya kufuatilia vipimo zaidi  na  kuongeza utalaam  ndiyo tukagundua hilo, tukaendelea na matibabu kuona kama atapona ndiyo amefariki,”.

Amesema kabla ya kwenda kituo cha Polisi  walitaka  kujiridhisha  kuhusu hayo matukio waliyoelezwa  na Daktari,  wakati wao walikuwa wanajua mtoto wao amefariki kifo cha kawaida kutokana na ugonjwa wa maralia.

Amedai kuwa walipofika chumba cha kuhifadhia maiti (mochwari ),walionesha mwili wa mtoto wao upande wa mbavu zake ulikuwa umepigwa na kuvujia damu, na Daktari huyo aliwaeleza kuwa ameingiliwa kinyume na maumbile  na kuchomwa sindano ya sumu.

Baada ya kujiridhisha ndipo walipoenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Muleba  ndipo uchunguzi ukafanyika  mbele ya Polisi  lakini cha kushangaza maelezo ya Daktari  yalibadilika ghafla.

“Daktari  baada ya kufanya uchunguzi  chini ya Jeshi la Polisi,ndipo maelezo yalipobadilika na kusema ni kweli mtoto alishaingiliwa na kutolewa bikira, inaweza kuwa iliondolewa zamani,nikamuuliza Daktari mbona awali ulitueleza kuwa mtoto ameingiliwa siku za karibuni kati ya siku 5 hadi 7 je? kwa nini sasa unabadilisha maneno hakunijibu chochote,”.

 “Naamani hiki kitendo amefanyiwa baada ya kwenda shuleni  alitoka nyumbani  Januari mwaka huu akiwa  mzima wa afya, anatembea vizuri.Mtoto mdogo aliyetolewa bikra wanafunzi,matroni au mzazi unaweza kugundua kwa haraka kama uko naye karibu.Nilimuuliza mwalimu mtoto wangu ameanza kusoma hapo akiwa na umri wa miaka 5 na miezi 7 hadi sasa amefariki na miaka  8  akiwa anaishi shuleni,kama mzazi nimeumia  amerudishiwa akiwa marehemu na kumzika,” .

Hata hivyo anasema amesikitishwa na kitendo cha daktari kubadilisha maneno kuhusu chanzo cha kifo cha mwanaye  na kudai kuwa amemuachia Mungu.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda, alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo amesema  kuwa mnamo Machi 5 mwaka huu, marehemu akiwa shuleni alijisikia vibaya  na tumbo lilianza kumuuma alipewa dawa za maumivu  lakini hazikumsaidia, ndipo Machi 7 mwaka huu walipoamua kumpeleka kituo cha afya Kaigara akiwa hawezi kuongea.

Chatanda,amesema alipimwa maralia na sukari na kubainika kuwa na maralia Kali,ndipo daktari alimchoma sindano na baada ya hapo alionekana kukosa nguvu ikabidi kumuwekea dripu ili kumuongezea nguvu ingawa zoezi hilo lilikwama baada ya mishipa ya damu kutoonekana.

Amesema Machi 9 mwaka huu alipewa rufaa kupelekwa hospitali ya Rubya  baada ya kupokea historia ya mgonjwa Daktari alimpima na kubaini kuwa damu yake ilikuwa na bakteria  wakati akiendelea na matibabu mtoto aliaga dunia.

“Mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari wa hospitali ya Rubya, hata hivyo wazazi hawakuridhika hali iliyopelekea mwili huo kufanyiwa uchunguzi upya na madaktari kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu Wilaya Muleba  na kubaini kuwa  marehemu alifariki baada ya kupungukiwa damu,maji pamoja na njaa baada ya kutokula kwa muda mrefu,”amesema

Amesema hayo yamebainika katika uchunguzi wa awali na kudai kuwa kuna sampuli zimechukuliwa kwenye mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Hata hivyo marehemu alizikwa Machi 11,2025 nyumbani kwao Kijiji na Kata ya Kibanga wilayani Muleba mkoani Kagera.