November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Utambuzi wa ardhi muhimu kuondoa dhuluma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ametoa rai kwa mamlaka pamoja na jamii, kuzingatia utambuzi wa ardhi ili kuepusha dhuluma na migogoro juu ya raslimali hiyo muhimu nchini.

Othman ametoa rai hiyo mapema leo, alipokutana na watendaji na wananchi mbalimbali Makaani Vitongoji alikofika kusikiliza malalamiko yao juu ya madai ya kuporwa na kulazimishwa kuondoka katika maeneo wanayoishi pamoja na tishio la athari za mazingira.

Amesema licha ya mantiki kwamba eneo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi za muda mrefu ambazo zinahitaji juhudi za makusudi za utatuzi wa pamoja, bali chimbuko la yote ni kukosekana utaratibu sahihi wa kutambua ardhi.

“Tatizo kubwa ni kuwepo chombo cha kusimamia matumizi ya ardhi kama inavyohitajika katika miongozo ya kisheria, kutofuatwa kwake dhuluma ya raslimali hii itaendelea katika maisha yote”, amebainisha Othman.

Pia amebainisha mapendekezo ya takriban Sheria Saba (7) zilizopitishwa mnamo Mwaka 1989, ikiwemo ya utambuzi wa Ardhi ambayo amesema bado haijafuatwa.

Ameongeza kuwa migogoro itaendelea kuchipua kila siku endapo hapatakuwa na utambuzi wa ardhi hivyo kama wanataka kutambua umiliki wa ardhi kwanza wahalalishe wananchi kile walichoharamishiwa katika ardhi yao ya haki na halali”.

Ameeleza kuwa tatizo ni la serikali na mamlaka zake ambapo ni kama zimeshindwa katika usimamizi wa ardhi kwa utaratibu wa haki licha ya kwamba inapeleka lawama kwa wananchi.

“Ukweli ni kwamba kwa kuzingatia maslahi binafsi hata kwa baadhi ya viongozi na watu wengine wenye mamlaka, kinachojidhihirisha ni kudhulumu na wengi kudhulumiwa haki ya ardhi na hata baadhi kwa madai ya kukosa karatasi za nyaraka ambazo wengine wamezipata ili kutenda dhuluma,”.

Amesisitiza juu ya mkanganyiko katika upatikanaji na utoaji wa nyaraka za ardhi Othman amesema”tatizo la nchi yetu kila mmoja ni bosi wa ardhi,haijulikani ni Sheha, Mkurugenzi au yoyote yule maana kila mtu ana mamlaka na anatoa maamuzi ya ardhi,”.

Hivyo amesema kunahitajika utaratibu sahihi wa kumiliki ardhi ili kuepusha dhuluma na migogoro pia kuwaongoza wananchi kumiliki rasilimali hiyo katika misingi ya haki.

Pamoja na hayo Othman amewahakikishia wananchi hao kwamba serikali itakabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na utaratibu unaostahiki kwa kuhusisha sekta zote husika.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud, amefahamisha kuwa mamlaka yake inajitahidi kukabiliana na malalamiko ya wananchi zikiwemo changamoto za watu wa Kijiji hicho licha ya kuwa kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa kwa sasa zimeibuka na zinahitaji busara ya namna ya kukabiliana nazo.

Akifahamisha adhima ya Mkoa wake katika kuzikabili changamoto hizo, Mattar amesema, “Dhamira yetu na ya Serikali hii ya awamu ya nane siyo kudhulumu wala kuwakosesha wananchi haki zao, bali la msingi ni kukaa na kushirikiana pamoja na kufuata taratibu,”.

Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Ofisi yake pindi zinapojitokeza changamoto, ili kila mtu aweze kuendelea na maisha kwa kuzingatia haki.

Akitolea ufafanuzi baadhi ya malalamiko ya wananchi, juu ya madai ya ardhi yanayozunguka pia maeneo ya Vitongoji Kwareni, Liko la Vumba na Kimbu-Sadi,Ofisa Mazingira Wilaya ya Chake-Chake kisiwani Pemba Mwalim Khamis Mwalim, amesema kutokana na uhalisia kwamba maamuzi ya kuipima, kuitumia na kuihalalisha ardhi kwa watumiaji wakiwemo wawekezaji kunahitaji maamuzi ya sekta Jumuishi.

Sambamba na kuwashirikisha kikamilifu wananchi, wamiliki wa maeneo hayo walistahili kushauriwa, kufidiwa pia kuongozwa juu ya utaratibu wa kulitumia tena kwa ajili ya uzalishaji eneo ambalo sasa linatumika kuchimba mawe, kokoto na rasilimali za namna hiyo.

Wakiwasilisha kilio chao kwa serikali mbele Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Wakazi wa Kijiji hicho akiwemo Saleh Nassor Juma, wamesema wanachokishuhudia sasa ni madhira yanayotokana na ugumu wa maisha kufuatia kulazimishwa kuondoka katika ardhi yao muhimu kwa ajili ya kilimo, makazi na mifugo, tangu asili na zama, pahala ambapo wao na wazee wao wamezaliwa.

“Ardhi yetu imevamiwa, inachukuliwa na tunalazimishwa kuondoka kama mnavyoona, tunahisi hii ni kusaliti hata ile sera na miongozo ya Mzee Karume ya kwamba wananchi wapate ahuweni ya kumiliki pahala pa maisha yao,” amesisitiza Saleh.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,amekamilisha ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba, kwa ajili ya shughuli mbalimbali za chama,jamii na serikali, akiambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib.