Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, amesisitiza umuhimu wa teknolojia na utafiti wa kina katika kuboresha uchunguzi na matibabu ya magonjwa adimu.


Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu Duniani ambayo huadhimishwa 28 Februari kila mwaka ambapo mwaka huu yaliyofanyika katika hospitali hiyo, Prof. Janabi ambaye pia alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu “Zaidi ya Unavyowaza” alieleza kuwa matumizi ya akili bandia (AI) na nyenzo za kisasa za uchunguzi yanaweza kusaidia madaktari kutambua kwa haraka na kwa usahihi.
“Kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa afya kwa kutumia teknolojia mpya kutasaidia kuboresha matibabu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora,” alisema Prof. Janabi.
Aidha, alisisitiza kuwa ni muhimu kuendelea kuchapisha tafiti na nyenzo za elimu kuhusu magonjwa adimu ili kuongeza uelewa wa jamii na kuwapatia madaktari maarifa sahihi ya kushughulikia wagonjwa wa aina hiyo.


Akizungumzia uzoefu wa madaktari katika kuchunguza matibabu na magonjwa adimu, Daktari wa watoto na mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa homoni (Pediatrician /endocrinologist) kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Kandi Muze, alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wagonjwa wa magonjwa adimu ni upungufu wa rasilimali za matibabu na uelewa mdogo wa jamii kuhusu hali zao. “Msaada wa jamii na elimu sahihi vitasaidia wagonjwa na familia zao kupata mazingira bora ya matibabu na msaada wa kihisia,” alisema Dkt. Muze.



Akitoa ushuhuda katika maadhimisho hayo kuhusu safari ya mwenye ugonjwa adimu, Baba wa Yusra ambaye ameishi na ugonjwa wa Gaucher tangu mwaka 2016, Khamis Kaundu, aliwashukuru madaktari kwa jitihada zao katika matibabu, akisisitiza kuwa wagonjwa wengi wanategemea msaada wa kitabibu ili kupata nafuu na kuokoa maisha ya wanaogua magonjwa adimu.
Akizungumzia matokeo ya utafiti uliofanywa na Madaktari wa Watoto kuhusu magonjwa adimu, Dr. Mariam Noorani alisema Kuna zaidi ya magonjwa 7,000 dunia nzima huku asilimia 8 ya watu duniani wana magonjwa adimu, ambapo madaktari hawana elimu wala ujuzi ya kutosha na wanapata changamoto nyingi.



“Mengi ya magonjwa haya huanza utotoni na vipo kwenye vinasaba, huku uelewa na ufahamu wa watoa huduma ni muhimu katika kugundua na kutibu mapema magonjwa adimu, magonjwa mengi hayana tiba kamili” Dr. Noorani
Prof. Janabi aliwataka watafiti na wataalamu wa afya kuangazia chanzo halisi cha magonjwa haya, akisema kuna haja ya kufanya tafiti mpya ili kupata majibu sahihi kuhusu sababu zinazochangia kuenea kwake. “Wanasayansi wa afya tunapaswa kufikiria kwa upana zaidi. Tunahitaji tafiti mpya zitakazotueleza kwa uhakika chanzo halisi cha magonjwa adimu. Bila kuelewa kiini chake, hatuwezi kuwa na tiba sahihi wala mbinu bora za kinga,” alisema Prof. Janabi.


Aidha, alitoa wito kwa watafiti kuhakikisha matokeo ya tafiti zao yanawasilishwa kwa lugha rahisi, ikiwemo Kiswahili, ili kuongeza uelewa kwa jamii pana.
Katika hitimisho lake, Prof. Janabi alihimiza watu kujikinga na maradhi kadri inavyowezekana, akitaja kuwa zaidi ya watu bilioni mbili duniani hufilisika kutokana na gharama kubwa za matibabu. Alisisitiza kuwa juhudi za utafiti, teknolojia, na uhamasishaji wa jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na magonjwa adimu.
Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu 2025 yaliratibiwa na Taasisi ya Alikimara Rare Desease Foundation ikishirikisha wadau kutoka tasisi mbalimbali ikiwemo Hospitali za Muhimbili, Aga Khan, Jumuiya ya Madaktari wa Watoto, Tanzania Human Genetics Organisation (THGO), Chuo Kikuu cha Muhimbili pamoja na Chuo Kikuu cha Aga Khan.




More Stories
Mo Dewji na Urithi anaoujenga ,unavyoenda mbali zaidi ya mafanikio binafsi
Mulika Community kusaidia Serikali kukomesha vitendo vya ukatili
TMDA yashinda tuzo za PRST ya Umahiri katika kampeni bora ya utoaji elimu jamii