Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
IMEELEZWA kuwa moja ya mambo muhimu ambayo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameyatekeleza kwa moyo mkunjufu ni uboreshaji wa miundombinu ya sekta ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji safi na salama.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 13,2025 na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, wakati akikagua utekelezaji wa mradi wa maji unaotokana na chanzo cha Mto Kiwira katika eneo la New Forest, jijini Mbeya.
“Vitu ambavyo aliweza kuvifanyia uchambuzi yakinifu ni kusikiliza kero za miundombinu ya maji ndani ya Taifa hili. Ndiyo maana hata alipochaguliwa kuwa Rais, aliunda wizara mahsusi inayoshughulika na sekta ya maji pekee, ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za maji safi na salama,” amesema Ussi.

Aidha, Ussi amesema mradi huo unaotekelezwa mkoani Mbeya ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maji nchini, ukiwa kati ya miradi mitano bora inayotekelezwa kwa ubora na umakini mkubwa.
Ameongeza kuwa kabla ya kufika Mbeya, aliwahi kuona mradi mkubwa wa maji jijini Mwanza, akiamini ndiyo wa mfano wa kuigwa, lakini alishangazwa kuona mradi wa Mto Kiwira ukiwa na ubunifu na usanifu wa hali ya juu, jambo linalodhihirisha dhamira njema ya Rais Samia katika kutekeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
Pia amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kujenga imani kubwa kwa wananchi kupitia uboreshaji wa miundombinu ya maji, akilenga “kumpunguzia mwanamke ndoo kichwani” kama alivyoahidi.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge na mgombea wa Jimbo la Uyole, Dkt.Tulia Ackson, amesema Mwenge wa Uhuru umefika katika eneo hilo kukagua tanki la maji lenye ujazo wa lita milioni 5, likiwa miongoni mwa hatua muhimu za utekelezaji wa mradi huo.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake kwa kufanya kazi bora na yenye viwango. Viongozi tunaona kazi kubwa inayofanyika, hivyo mnastahili pongezi,” amesema Dkt. Tulia.
Naye Mkurugenzi wa Uzalishaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Mbeya UWSA, Mhandisi Barnabas Konga,amesema mradi huo unatekelezwa kwa mfumo wa usanifu na ujenzi (Design and Build), ambapo utekelezaji wake ulianza Aprili 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2025.
“Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji katika eneo la New Forest lenye ujazo wa lita milioni 5 umefikia asilimia 45 ya utekelezaji,” amesema Mhandisi Konga.
Ameongeza kuwa mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji kwa gharama ya Shilingi Bilioni 119.8.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina