June 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ussi awataka wananchi Handeni kulinda miundombinu ya maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ili miradi ya maji iwe endelevu na wasiweze kurudi tena kwenye shida ya maji kama ilivyokuwa zamani.

Akizungumza leo Juni 8, 2025 alipofika kuweka Jiwe la Msingi Mradi wa Usambazaji Maji Kwamaizi uliopo Kata ya Kideleko, Halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga, Ussi amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji, hivyo wananchi watoe ushirikiano kubaini wezi na waharibifu wa miundombinu.

“Niwaombe sana wananchi muitunze miradi hii ya maji safi na salama. Serikali imekuwa inatumia fedha nyingi .kujenga majengo haya (matenki), Serikali imekuwa inatumia fedha nyingi kuhakikisha kila mwananchi anafikishiwa maji safi na salama. Nimesikiliza vizuri taarifa iliyotolewa hapa, na kuwasikia wananchi wenyewe wakielezea kuwa walikuwa wanapata maji umbali wa kilomita tano. Kilomita tano ni nyingi sana.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi akizungumza na wananchi wa Kideleko.”

“Leo hii mradi umekuja kabisa kuondosha ile adha ya maji na sasa maji yapo karibu na mitaa yetu, yanafika kwa wakati, na ni safi na salama. Najua baadhi ya miongoni mwenu wapo wanaopinga jitihada za Serikali na maendeleo yanayofanywa kwa ajili ya wananchi, naomba ninyi mlio wengi muwe walinzi kwa wengine, wale wote wanaofanya vitendo vya uharibifu nendeni mkatoe taarifa kwa mamlaka husika kwa usahihi. Nakumbuka wapo watendaji wa mitaa na vijiji, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi pamoja na madiwani” amesema Ussi.

Ussi amesema anawashukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Handeni Trunk Main (HTM) kwa kujenga tenki la mradi kwa kiwango cha juu, na kusema taasisi zilizokabidhiwa dhamana ya kuwapatia wananchi maji zinafanya vizuri ikiwemo Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

“Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza (wa pili kulia) akionesha ramani ya Mradi wa Maji Kwamaizi.”

“Nawashukuru Mamlaka yetu ya maji ya HTM pamoja na RUWASA, kwa kweli wamekuwa wanafanya kazi kubwa na nzuri ndani ya Taifa hili. Sisi binafsi tumekuja hapa tumejionea, nyuma yangu hapa ukigeuka, unaukuta mradi mkubwa wa kimaendeleo wa maji safi na salama, kwa kweli unakwenda kusaidia wananchi walio wengi, kwa kweli tunakushukuru Mkuu wa Wilaya (ya Handeni, Japhari Kubecha) pamoja na wananchi kwa kupokea mradi huu. Naamini wananchi wengi wangekuwa hawajaupokea mradi huu, sidhani kama leo tungekuja kuona haya tuliyoyaona.

“Tungekuja kuona kitu kingine au mambo mengine, lakini sio huu mradi wa maji safi na salama. Lakini wananchi wenyewe wameonesha hamasa, wameonesha bashasha, wameonesha upendo, lakini kabla ya mradi huu kuanza, mlionesha mashirikiano mazuri kwa maana mlikaa na wananchi hawa mkawaeleza ni jinsi gani mnataka kutengeneza mradi huu wa maji, ndiyo maana hatua iliyofikia sasa kwa kweli ukiambiwa ni hatua ya kuweka jiwe la msingi hautokubali, utasema ni hatua ya kulizindua hili jengo (tenki)” amesema Ussi.

“Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa ya mradi.”

Akisoma taarifa ya ujenzi ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza amesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Kata ya Kideleko wapatao 6,037 waishio katika mitaa ya Kideleko, Kampene, Muungano, Ndekai na Bangu. Mradi huo unatekelezwa na WaterAid Tanzania, HTM, RUWASA Handeni pamoja na Halmashauri ya Mji Handeni.

“Mradi huu ulianza kutekelezwa Julai 20, 2024 na unatarajiwa kukamilika Juni 30, 2025. Gharama za mradi huu ni sh. 537,439,796, ikiwa WATERAID imechangia sh. 462,694,796, Serikali Kuu kupitia HTM na RUWASA imechangia sh. 63,620,000, na wananchi wa Kata ya Kideleko wamechangia sh. 11,125,000” amesema Mhandisi Mgaza.

Mhandisi Mgaza amesema kazi zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa chujio la maji (slow sand filtration) lenye ukubwa wa lita 100,000, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji lenye urefu wa mita 1,485, ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji lenye ukubwa wa lita 100,000 kwenye mnara wa mita sita, ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la tenki la kuhifadhi maji lenye ukubwa wa 400m2.

“Tenki la Mradi wa Maji Kwamaizi.”

Uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yenye urefu wa mita 2,358, ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji vyenye mfumo wa malipo ya kabla (Prepaid water meter) na ufungaji wa mitambo ya kusukuma maji kutoka katika chanzo cha bwawa la Kwamaizi hadi kwenye tenki la kuhifadhi maji.

“Jumla ya sh. 443,595,219 zimetumika kwa ajili ya ununuzi wa mabomba, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji, ujenzi wa chujio la maji (Slow Sand Filtration) na ujenzi wa Tenki la kuhifadhi maji lenye ukubwa wa lita 100,000 kwenye mnara wa mita sita. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 70.

“Tunamshukuru sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha za utekelezaji wa mradi huu” amesema Mhandisi Mgaza.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Kwamaizi.”
“Baadhi ya wafanyakazi wa HTM na RUWASA wakifurahi pamoja baada ya mradi kukubaliwa kuwekwa jiwe la msingi.”