November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Usiyoyajua kuhusu pori la Akiba Liparamba,kuna miti iliyogeuka mawe

Na Albano Midelo,TimesMajira Online,Ruvuma

NI mbuga chache za wanyama pori hapa nchini ambazo zimebahatika kuwa na maingilio au mapitio ya wanyama ambayo yanaitwa ushoroba kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine jirani .

Pori la wanyamapori Liparamba lililopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa mapori au mbuga za wanyama zilizobahatika kuwa ushoroba wa wanyama.

Mfano wa ramani ya Afrika ambayo imechorwa na maji juu ya mwamba kwenye mto Mkuyu ndani ya pori la Liparamba

Afisa Utalii wa Pori hilo Maajabu Mbogo anasema pori hilo ambalo lilianzishwa mwaka 2000,limebahatika kuwa na wanyamapori wakubwa na wadogo wakiwemo tembo,simba,chuo, viboko, mamba, tandala, pofu, palahala, kuro,nyati, pundamilia, fisi,chui na mbweha.

Anaongeza kuwa katika pori hilo kuna aina mbalimbali za ndege kama vile kanga,koribustard(Mbawala) na fundichuma.

“Neno liparamba ni la kabila la kimatengo ambao ni wenyeji wanaoishi Wilaya ya Mbinga,maana liparamba ni mbuzimawe,pori hili lina makundi makubwa ya tembo,ambao ni wakimbizi kwa sababu huwa wanatoka Msumbiji na kuhamia Liparamba’’,alisema Mbogo.

Anasema makundi makubwa ya tembo kutoka Msumbiji wanaanza kuingia kwa wingi katika pori la Liparamba kuanzia Machi kila mwaka na kufikia mwezi Julai,tembo wanaanza kurudi nchini Msumbiji na kwamba inapofika kati ya Septemba na Oktoba wanabaki tembo wachache sana ndani ya hifadhi hiyo.

Miss Utalii Tanzania 2020 Ruvuma Fidea Hilary akiwa ameshika mti aina ya mtetereka uliogeuka jiwe kutoka hifadhi ya Liparamba

“Inapotokea kule nchini Msumbiji majangili yamewashambulia tembo au kuwasumbua,tembo hao wanapoingia katika hifadhi ya Liparamba hawatoki,wanaweza ndani ya pori la Liparamba kati ya miaka miwili hadi mitatu bila kutoka na kurudi Msumbiji kwa sababu Liparamba ni sehemu salama ya kuishi tembo’’,alisisitiza.

Anavitaja vivutio vingine vilivyopo katika pori hilo ni uwepo wa aina mbalimbali za nyoka kama vile jamii ya mamba na kobra na kwamba pori hilo lina maporomoko ya maji ya Nakatuta katika Mto Ruvuma ambayo ni kivutio cha asili cha utalii.

Kwa mujibu wa Afisa Utalii huyo,pori hilo lina vivutio vinavyofaa kufanya utalii wa kupanda kwenye mawe kwa sababu ndani ya hifadhi hiyo,kuna mawe makubwa yanayofaa kwa utalii wa aina hiyo.

Anasema ndani ya pori hilo kuna miti ya ajabu ukiwemo mti wa mtetereka ambao ukikauka unabadilika na kuwa jiwe na kwamba miti ya aina hiyo ipo kwa wingi katika eneo la Nakatuta kandokando mwa Mto Ruvuma hivyo kuvutia watalii wengi wanaopenda kufanya utafiti wa miti na mimea.

Kulingana na Mbogo katika eneo la Nakatuta pia kuna miti mingine jamii ya kambakamba ambayo ukiikata inatoa maji ambayo unaweza kujaza kwenye chupa,kunywa na kukata kiu kabisa.

Afisa Utalii huyo amesema katika pori hilo kuna mito ya kuvutia ambayo inapita ndani ya hifadhi,ukiwemo mto Lumeme ambao unamwaga maji yake katika mto Ruvuma.Anasema mto Lumeme haukauki na unafaa kwa utalii wa kuogelea na kuvua samaki.

Analitaja eneo lingine linalofaa kwa utalii katika pori hilo ni makutano kati ya mto Ruvuma na mto Namakunguru ambako kuna jiwe kubwa lenye urefu wa meta 70 toka chini ya Mto Ruvuma hadi juu ambalo linafaa kwa utalii wa kupanda.

Katika eneo la Mkuyu ndani ya pori la Liparamba pia kuna kivutio kinachowashangaza wengi ambacho,maji yanayotiririka kwenye mto Mkuyu yametengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba.

“Maji yameweza kutengeneza mfano wa ramani ya Afrika juu ya mwamba,ukichukua ramani ya Afrika na kuangalia ramani iliyotengezwa na maji hakuna tofauti ni ramani kabisa ya Afrika,haya ni moja ya maajabu katika pori la Liparamba’’,anasema Mbogo.

Kwa upande wake Mhifadhi Msaidizi wa pori hilo Paul Protas amesema mgeni anapofika katika pori la Akiba Liparamba anaweza kupata nafasi ya kutembelea bwawa la Mkuyu ambako mtalii anapata nafasi ya kuogelea na kufanya utalii wa kuvua samaki na kumrudisha ndani ya maji.

Protasi anakitaja kivutio kingine kilichopo katika pori hilo ni uwepo wa ndege aina ya koribustard(Mbawala) ambaye hapa nchini anatumika kama alama ya Taifa kama ilivyo kwa mnayama twiga.

“Huyu ni ndege mkubwa ana uwezo wa kufikisha uzito KG 16,ana urefu wa SM 1330,huyu ni ndege wa kitaifa,anachinjwa kwa kibali kinachoombwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’,anasisitiza.

Kwa upande wake Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema pori hilo lina kiwango cha juu cha hifadhi ambacho kinatiliwa mkazo kisheria katika ulinzi,usimamizi, uendelezaji na matumizi ya busara ya mali hai ikiwemo misitu,samaki na wanyamapori.

Utafiti umebaini kuwa Liparamba ni eneo kipekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo, ambalo lipo karibu na ziwa Nyasa na uwepo wa msitu mnene wa asili na wenye mandhari ya kuvutia na eneo muhimu la kuhamia wanyamapori kati ya nchi Tanzania na nchi ya Msumbiji.

Amesema serikali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii imelenga kutenga eneo hilo kama kielelezo cha ukanda wa viumbehai katika mazingira yao ya asili kwa kupunguza kasi ya mabadiliko makubwa yatokanayo na maendeleo na uharibifu wa binadamu na kuweka sehemu ya utafiti wa mazingira,elimu ya uchunguzi wa miti,wanyama na samaki.