November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa umeleta maendeleo nchini


Na David John,Timesmajira Online

SERIKALI ya Tanzania imesema ushirikiano wake na Nchi ya Ufaransa umesaidia kuleta maendeleo katika nyaja mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki na Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro katika hafla ya kusherekea siku ya Uhuru wa nchi ya Ufaransa miaka 234 iliyopita.

Amesema toka nchi ya Tanzania ipate uhuru imekuwa na uhusiano mzuri na Serikali ya Ufaransa katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Waziri Ndumbaro amesema Serikali ya Ufaransa ni nchi ya pili ambayo imekuwa ikileta watalii wengi Tanzania ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja zaidi ya watalii laki moja wamekuja nchini hapa.

“Uhusiano wetu ni mzuri na tumekuwa tukishirikiana sana,tunaposherekea siku hii tunatafakari namna ya kuboresha uhusiano pamoja na ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa,”amesema Waziri Ndumbaro

Amesema hatua hiyo imeendelea kuchochewa zaidi toka kuanzishwa kwa ndege ya Air France ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Paris na kuja Dar es salaam.

“Tunatarajia watalii watazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa kupitia kuongeza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili utaendelea tunatarajia watalii wataongezeka zaidi,”amesema Waziri Ndumbaro

Pia amesema katika sekta ya nishati kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania umekuwa ukitekelezwa na kampuni ya kifaransa.

Aidha amesema uhusiano baina ya nchi hizo mbili umekuwa ukipimwa katika nyaja mbalimbali ikiwemo za kisiasa na kidemokrasia.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Nabil Hajlaoiu amesema uhusiano baina ya nchi hizo mbili yameweza kuleta matokeo mazuri.

Amesema serikali ya Ufaransa imekuwa ikishirikiana na nchi ya Tanzania katika maeneo elimu, kilimo,masuala ya jinsia, mazingira pamoja na kilimo.

Balozi Hajlaoiu ameeleza kuwa katika kuboresha zaidi uhusiano Serikali ya Ufaransa imefungua ofisi ndogo ya Balozi katika Mkoa wa Dadoma.

“Tunajivunia na kufurahia uhusiano baina yetu na Serikali ya Tanzania kupitia umoja wetu na mshikamano ambao umekuwa ukileta matokeo mazuri,”amesema Balozi Hajlaoiu.