October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushirikiano wa Tanzania na Japan kuwezesha ujenzi wa Flyover Morocco Dar

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na Japani hususan katika Sekta ya miundombinu ambapo Tanzania inaendelea na mazungumzo na nchi hiyo ya kushirikiana katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya kupunguza msongamano wa magari katika miji na majiji.

Ameeleza kuwa Tanzania imeanza mazungumzo na Japani ya kushirikiana katika usanifu na ujenzi wa barabara ya juu (FlyOver) katika eneo la Morocco jijini Dar es Salaam itakayopunguza msongamano wa magari na kurahisisha shughuli za kiuchumi.

Bashungwa amesema hayo leo Oktoba 03, 2024 wakati akifungua mkutano wa mashirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Japani ya kujipanga kimkakati katika ujenzi wa miundombinu ubora.

“Sasa hivi tunaendelea na mazungumzo na Japani kuhusu ujenzi wa Flyover ya Moroco kwa kufanya usanifu na ujenzi pamoja na kuboresha maeneo mengine yenye mapishano ya barabara ili kupunguza matumizi ya taa za barabarani”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua nchi kwa kuweka mazingira wezeshi na kuvutia uwekezaji na biashara kwa nchi zingine kwa kuimarisha ushirikiano na upatikanaji wa masoko kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Umoja wa Soko la Afrika.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji mbalimbali wanaofika nchini kuwekeza, kufanya biashara na kuondoa urasimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameeleza kuwa maendeleo ya nchi yoyote yanategemea sana sekta ya usafiri kwani ni kiungo muhimu kwa biashara ya ndani na ya kimataifa ambapo kwa sasa Tanzania ina jukumu muhimu kama lango la kimataifa kwa baadhi ya nchi jirani ili kurahisisha usafirishaji na upatikanaji wa soko la kimataifa.

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Baraka Luvanda ameeleza umuhimu wa mkutano huo ambao umewakutanisha wabobezi katika ujenzi wa miundombinu bora na ya kudumu inayoweza kuhimili majanga kama vile matetemeko ya ardhi na vimbunga kutoka nchi ya Japan na hivyo watasaidia kutoa michango na uzoefu kwa makampuni ya ujenzi kwa nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania katika ujenzi wa miundombinu yote nchini.