January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM)

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 19 hadi 25 Juni 2022 ulihusisha jukwa la biashara, wanawake na vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Waziri wa Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alisema Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la biashara ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili fursa za biashara na uwekezaji kwenye Jumuiya ya Madola na Bara la Afrika na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hizo zikiwemo athari zitokanazo na janga la Uviko-19 na mgogoro kati ya mataifa ya Ukraine na Urusi;

Aidha kwa upande wa jukwaa la wanawake Waziri Mulamula alisema Jukwaa hilo lilijadili usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake kwenye nyanja zote; kuongeza nafasi za uongozi kwa wanawake; kutoa elimu bora kwa watoto wa kike na namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za wanawake.

Pia kwa upande wa vijana Balozi Mulamula alisema jukwa hilo lilijadili masuala ya ajira kwa vijana, kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana; elimu kwa vijana; kusaidia vijana wajasiriamali; matumizi ya teknolojia kwa vijana; kujiajiri; na kuongeza udhamini kwenye shughuli za vijana.

Mbali na hayo Waziri Mulamula alizungumzia kuhusu mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuhiya ya Madola uliofanyika tarehe 24 Juni 2022;

“Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mwana wa Mfalme wa Uingereza, Charles, The Prince of Wales, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo; Mhe. Rais Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha mwaka 2022-2024; Mhe. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madola tangu mwaka 2018; Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola walioshiriki CHOGM 2022; na baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama walioshiriki Mkutano huo.”

Katika Mkutano huo Tanzania ilisisitiza umuhimu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kusaidia nchi wanachama kutekeleza programu za kukuza uelewa miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na binafsi ili kutambua majukumu waliyonayo katika kuhudumia wananchi, hivyo kuepuka rushwa na vitendo ambavyo vinakinzana na kanuni za utawala bora na utawala wa sheria.

Balozi Mulamula alisema Wakati wa Mkutano wa CHOGM, kulifanyika mikutano mingine mingi ya pembezoni ambayo ilijadili mada mbalimbali. Mikutano miwili kati ya hiyo ilijadili Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele.;

“Malengo ya Mkutano huu yalikuwa ni kupokea mikakati ya viongozi katika kukabiliana na malaria na magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Mhe. Makamu wa Rais alieleza changamoto kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kukabiliana na magonjwa haya wakati ambapo mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanaendelea. Aidha, alieleza uzoefu, mafanikio na mikakati ya Tanzania kukabiliana na magonjwa hayo.”

Waziri Mulamula alisema
Makamu wa Rais na yeye mwenyewe walifanya mikutano ya uwili na viongozi mbalimbali waliohudhuria mikutano hiyo. Lengo lilikuwa ni kuitangaza nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za utoaji wa huduma kwa jamii.;

“Makamu wa Rais alieleza ukubwa wa changamoto ya malaria nchini Tanzania ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 94 ya wananchi wapo kwenye hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo. Kadhalika, Mhe. Makamu wa Rais alifafanua jitihada za kukabiliana na malaria ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mwaka 2021-2025 unaolenga kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025 na kutokomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030.”

Pia Balozi Mulamula alifanikiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Amina Mohammed na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair na kuwapa salamu za Rais Samia.

“Ujumbe wangu katika mazungumzo hayo ni kuhusu maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba Tanzania ni eneo salama kwa wawekezaji. Maeneo niliyosisitiza ni kilimo, utalii, afya na usafiri wa anga na Uchumi wa buluu hasa katika usimamizi na uendeshaji wa bandari na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.”