January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushiriki wa Samia G20 wainufaisha Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraaliyekuwa Rio de Janeiro

USHIRIKI wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa G20 uliomalizika wiki iliyopita katika mji wa Rio de Janeiro, nchini Brazil umekuwa wa manufaa makubwa kwa Tanzania na Bara la Afrika.

Manufaa ya mkutano huo kwa Tanzania yalianikwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akizungumza na wahariri vya vyombo vya habari jijini Rio de Janeiro baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Rais Samia alisema ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa G20 una manufaa makubwa kwa Tanzania, lakini pia kama Afrika.

Alisema anashukuru kwa mwaliko, maana Tanzania sio mwanachama wa G20, lakini wameona kuna sababu ya kutuliaka kama Tanzania kushiriki kwenye mkutano huo.

“Kwa sababu kama mnavyojua kundi la G20 ni nchi zote zilizoendelea na zenye uchumi mkubwa, kwa hiyo ukipata fursa ya kualikwa na kupewa nafasi ya kusema, kwanza hayo ni mafanikio, kutambulika, kuitwa na kusema mbele yao,” alisema Rais Samia.

***Mambo matatu kwenye mkutano huo

Rais Samia alisema kwenye mkutano huo walikuwa na mambo matatu makubwa.

***Kuondoa njaa

Rais Samia suala la kwanza walilozungumzia ilikuwa ni kuondoa njaa, ambapo walifanya tathmini ni kwa kiasi gani dunia imeweza kuondoa njaa.

“Tumeona kazi haijafanyika vizuri kwa sababu kuna watu wengi duniani bado wana matatizo ya njaa na sio Afrika peke yake na katika maeneo mengine duniani tofauti.

Kwa hiyo katika kulizungumza hili nchi nyingi zimetoa mikakati ya nini tufanye kupunguza njaa, lakini kuna zile ambazo hali zao ni nzuri wameweza kutoa matumaini na ahadi za kusaidia kifedha, kiufundi, teknolojia na mambo mengine ili kuondosha njaa,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwa upande wetu (Tanzania) tulipopewa nafasi ya kusema kwenye hili, tulizungumza hali halisi Tanzania kwamba sisi Tanzania tukienda kama hali ilivyo, bila kuathiriwa na matukio yoyote ya mabadiliko ya tabianchi, basi tunajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128 na tunaweza kuwauzia wenzetu.

Lakini tuna uwezo wa kuzalisha zaidi na tukaweza kulisha majirani, kulisha bara la Afrika na hata nchi za nje ya Afrika.”

Rais Samia alitoa mfano kwa akisema kwa sasa hivi kuna mazao ya mboga mboga ambayo Tanzania inasafirisha mpaka Ulaya, lakini kuna mahindi na mpunga ambayo Tanzania inalisha nchi za jirani.

Kwa upande wa maharage, Rais Samia alisema Tanzania inalisha China. ” Tunalisha China Soya na Soya yetu wanaipenda kweli kweli Wachina, ila tuna vikwazo ambavyo tukisaidiwa tunaweza kuzalisha zaidi,” alisema.

***Ataja vikwazo kwenye kilimo

Rais Samia alitaja kikwezo cha kwanza ni tafiti za kilimo. Katika eneo hilo alisema wanadhani kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye tafiti hasa kwenye mambo ya kilimo.

Alitaja eneo la pili kuwa ni masuala ya mambo ya kutumia mashine katika kilimo , matrekta, mashine za kuvunia, mashine za kumwagilia na mambo kama hayo.

“Tukiweza kufanya hivyo tunaweza kuzalisha chakula kingi sana,” alisema.

***Mbolea

Rais Samia alisema tatizo lingine lingine ni mbolea, ambapo kwa muda mrefu Tanzania tunanunua mbolea kutoka nje.

“Ndani nadhani tuna viwanda viwili vya kuzalisha mbolea, lakini pamoja na viwanda hivyo vya ndani, bado tunaagiza mbolea kutoka nje , nadhani kazi yetu ni kuvutia wawekezaji wa viwanda vya mbolea kuja kuwekeza halafu tuweze kuzalisha na kusabamza mbolea ya kutosha kwa wakulima wetu,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Kwa sababu ukiangalia viwango vya matumizi ya mbolea Duniani, Tanzania hatujafika hata nusu kwa heka, kwa hiyo tukiweza kutumia mbolea vya kutosha, mbolea zinazotakiwa, kwa mfano Intercom pale wanazalisha mbolea ambayo wanachanganya na mbolea kidogo ya viwandani na mambo mengi ni yale yale yanayopatikana ndani ya nchi, wanachanganya wanazalisha na mbolea inakuwa nzuri,” alisema.

Rais Samia alisema kwenye mambo hayo matatu tukiweza kufanya vizuri Tanzania kweli inaweza kulisha bara la Afrika, lakini na dunia pia.

“Kwa sababu kama mbogamboga zetu na maharage yanakwenda Ulaya na mambo mengine, asali maeneo mengine duniani huko ni kulisha Ulimwengu.

Kwa hiyo tukiongeza jitihada hayo mambo hayo matatu niliyoyasema tutaenda kufanya vizuri.”

***Jambo la Pili kwenye mkutano wa G20

Rais Samia alitaja jambo la pili ambalo walizungumza kwenye mkutano huo ni safari kutoka hapa tulipo kwenye matumizi ya diseli kwenda kwenye matumizi ya nishati jadidifu (nishati inayotokana na maji, jua na upepe.

Alisema wenzetu walioendelea walikuwa wanasema wako mbali, wengine wanasema wapo asilimia 80, 90 na wengine wamefikia asilimia 100, nyingine ni nchi ndogo, lakini kwa sababu wana maji ya kutosha, wana mambo mengine wameweza kufikia asilimia 100 ya matumizi ya nishati jadidifu.

|”Sisi wengine bado tuko kwenye safari , bado tunatumia diseli,gesi, kwa mfano sisi Tanzania, Bwawa letu lile (Bwawa la Mwalimu Nyerere) tunatumia Hydro ambayo hiyo, ndiyo nishati Jadidifu , lakini kwa sasa tuseme asilimia 60 ya umeme wetu unatokana na gesi, wanapiga kelele tusitumie gesi, lakini safari, na sisi tumeomba watupe muda zaidi.

***Nishati safia ya kupikia

Rais Samia alisema kama ilivyo agenda yake, alizungumzia suala la nishati safi ya kupikia na kuwatka watuunge mkono kuhakikisha watu wengi Afrika wanapata umeme kutokana na vyanzo vyote hivyo (maji, jua upepe) ili wananchi wapate umeme, waweze kupika kwa kutumia umeme na kupika kwa kutumia nishati safi.

“Na nishati safi hapa sio tu umeme, kuna nishati nyingine mfano pale kwetu Tanzania tunatengeneza mkaa kutokana na vumbi la makaa ya mawe ambao wataalam wamefanya utafiti wameweza kutoa gesi ambazo zina madhara na kufanya mkaa uwe salama.

Kwa sasa hivi unasambaa kwa wingi sana na nishati safi, kwa hiyo ndilo la pili tumezungumzia na kwa bahati nzuri kuna mabenki yanatuunga mkono kwenye nishati safi ya kupikia, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika, Norway nao wametuunga mkono vizuri sana.

Lakini pia kama mnavyoelewa Januari nchini tutakuwa na mkutano mkubwa wa kuangalia mambo ya umeme, lengo ni ikifika 2030 karibu watu milioni 300 Afrika kati ya watu milioni 700 wawe wanatumia umeme.

“Sasa hivi watu milioni 700 Afrika hawana umeme kabisa, angalau tunataka ikifika 2030 watu milioni 300 wawe wamepata umeme, sasa Mungu akijalia huko nami ninamaliza dhamana hii (Urais) kwa hiyo nitajidai kweli kwamba nimewezesha watu milioni 300 ndani ya Afrika kupata umeme na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia ,” alisemaa.

****Jambo la tatu mkutano G20.

Rais Samia alisema kwenye mkutano huo,walizungumzia mambo ya utawala bora na utawala wa sheria.

“Hapo sasa wengine tulikuwa wasikilizaji, lakini yaliyosemwa humo ni haja ya kuona ulimwengu unakwenda salama, haja ya kusimamisha vita vinavyoendelea, haja ya kutoa njia ya kusaidia wale waliofikwa na maafa ya vita na mengine, kuona wanasaidiwaje.

Kwa hiyo wenzetu wenye misuli ndipo walijitutumua kila mtu kusema lake, hatuelewi kama miito ya kusimamisha vita imepokelewaje, hatujui, lakini yalisemwa sasa imetosha, vita visimame na tuone dunia inakwenda kwenye mwelekeo mzuri,” alisema Rais Samia na kuongeza kwenye mambo hayo hayo makubwa yaliyozungumziwa kwenye mkutano huo na sisi (Tanzania) tunahusika, hatuhusiki na vita, lakini kwenye suala la utawala bora tunahusika kwa sababu kwenye ukanda wetu wa SADC na EAC bado hakuko salama kwa hiyo kama hakuna usalama, ukanda wote ule bado unakuwa kwenye wasiwasi.