March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushirika Dodoma waleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi waliojiunga na ushirika

Na Joyce Kasiki,Timesmajiraonline,Dodoma

MRAJISI  wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amesema kuwa mfumo wa ushirika mkoani humo umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali, kutokana na usimamizi madhubuti wa vyama vya ushirika pamoja na uhamasishaji endelevu wa wananchi kujiunga na vyama hivyo.

Akizungumza katika maonyesho ya Nanenane 2025 jijini Dodoma, Chitinka alisema hadi sasa mkoa huo una jumla ya vyama 126 vya ushirika, ambapo 27 ni vya kilimo na zaidi ya 70 ni SACCOS zinazotoa huduma za kifedha kwa wanachama wao, zikiwemo zile za maeneo ya kazi na zile za kijamii zinazohudumia wananchi wa kawaida, wajasiriamali na wafanyabiashara.

“SACCOS zimekuwa chachu ya maendeleo kwa wanachama wake, kwani zimewawezesha wengi kuanzisha miradi, kukuza mitaji na kuinua kipato chao. Ushirika sasa ni nguzo ya uhakika katika kuwakomboa wananchi kiuchumi,” alisema Chitinka.

Kwa mujibu wa Chitinka, mazao matano makuu yanayoongoza kwa uzalishaji katika mkoa wa Dodoma ni ufuta, choroko, mbaazi, dengu na zabibu. Alibainisha kuwa kupitia ushirika, wakulima wa mazao hayo wamewezeshwa kuuza kwa tija na kuongeza kipato chao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo zaidi ya tani 1,000 za mazao mbalimbali zimeuzwa.

Kupitia mfumo huu wa stakabadhi ghalani, wakulima wamepata bei nzuri ya mazao yao, na pia Serikali imeongeza mapato yake. Huu ni ushahidi wa namna ushirika unavyobadilisha maisha ya wananchi,” alisisitiza.

Akiweka mkazo juu ya zao la zabibu ambalo ni maarufu katika mkoa huo, Chitinka alisema kuwa ushirika umesaidia wakulima wa zabibu kuongeza thamani ya mazao yao kwa kuzalisha bidhaa kama mchuzi wa zabibu, zabibu kavu na mvinyo.

Tuna viwanda viwili vya kuongeza thamani ya zabibu, ambavyo vinazalisha bidhaa zenye ubora unaovutia masoko ya ndani na nje ya nchi. Katika maonyesho haya, vyama vya zabibu vimeuza kwa kasi na kupata kipato kikubwa,” alisema.

Aidha, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa kutoka nje ya Dodoma wamekuwa wakinunua mchuzi wa zabibu kutoka kwa vyama hivyo kwa ajili ya kutengeneza wine nje ya nchi, jambo linaloongeza fursa za soko na ajira kwa vijana wa eneo hilo.

Chitinka amebainisha kuwa SACCOS nyingi zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuinua uchumi wa wanachama wake kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Baadhi yao wameweza kupanua biashara, kuanzisha miradi mipya na hata kuongeza ajira.

“Ushirika wa kuweka na kukopa umekuwa ukitoa mikopo ambayo imewawezesha wananchi wengi kuinuka kiuchumi. Ushiriki wa SACCOS kwenye maonyesho ya Nanenane pia umetoa hamasa kubwa kwa wengine kujiunga,” alisema.

Mrajisi huyo alisema kuwa wanatoa elimu na kufanya uhamasishaji katika jamii ili watu wengi zaidi waelewe umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika, huku wakihakikisha kuwa vyama vyote vinavyosajiliwa vinaendeshwa kwa uwazi na kufuata sheria.

“Tunasajili, tunasimamia lakini pia tunafuta vyama visivyotekeleza wajibu wao. Tunataka kuona ushirika unakuwa chombo cha kweli cha maendeleo ya watu, alieleza.

Kwa sasa, mkoa wa Dodoma unaendelea na maandalizi ya kuanza minada ya mazao ya mbaazi, choroko na dengu, ambapo tayari bidhaa hizo zimeanza kukusanywa katika maghala mbalimbali kwa ajili ya kuuza ndani na nje ya nchi.

Chitinka amesema kuwa mafanikio haya yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali, wadau wa maendeleo, na wanachama wa vyama vya ushirika ambao wameonyesha mwamko mpya wa kutumia ushirika kama chombo cha kujiletea maendeleo.

“Ushirika siyo tena hadithi ya jana, ni suluhisho la leo na matumaini ya kesho. Tunawahamasisha wananchi wote mkoani Dodoma wachangamkie fursa hizi na kuwa sehemu ya mageuzi ya kiuchumi kupitia vyama vya ushirika,” alihitimisha.