March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Urambo wafungua milango ya uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Urambo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora imefungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta mbalimbali,ambapo wametenga eneo la ardhi lenye ukubwa wa hekari 72 kwa ajili ya kazi hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Halmashauri hiyo,Grace Quintine, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya Halmashauri katika kikao cha Baraza la Madiwani.

Amesema Halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri zenye mazingira bora ya uwekezaji na ardhi nzuri inayofaa kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Ambapo amesema,maboresho ya miundombinu ya huduma za kijamii ambayo yameendelea kufanywa na serikali ni kivutio muhimu kwa wawekezaji.

Guintine amefafanua kuwa Urambo ni mahali salama kwa uwekezaji na kwa mwaka huu wa fedha wameratibu maeneo maalumu yanayofaa kwa uwekezaji ambapo wametenga eneo lenye ukubwa wa hekari 72 katika Kata za Usoke na Kapilula.

Mbali na uwekezaji huo, halmashauri pia imeendelea kuandaa mazingira yatakayosaidia kufanikisha utekelezaji shughuli za maendeleo ikiwemo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

“Kwa sasa tunafuatilia upatikanaji wa zaidi ya shilingi bilioni 1,kwa ajili ya kukamilishaji baadhi ya miradi na kuratibu upatikanaji wa maeneo mengine ya uwekezaji katika wilaya yetu hiyo,”amesema.

Pia amesema,kwa mwaka jana Halmashauri hiyo iliidhinishiwa na Bunge mapato na matumizi ya kiasi cha shilingi bil 39.3 ila hadi kufikia Novemba 30, 2025 walikuwa wamekusanya jumla ya shilingi bil 15 kutoka vyanzo vya ndani.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Athumani Mwiniko,amesema kuwa Madiwani watashirikiana na watalaamu ili kuhakikisha shughuli za maendeleo zinatekelezwa ikiwemo kuongeza vyanzo vipya ya mapato.

Ametoa wito kwa Madiwani, wataalamu na watendaji wa vijiji na kata kushirikiana na kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki katika shughuli za maendeleo.