December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uraia Wetu kuzileta azaki 60 kwa pamoja Kanda ya Ziwa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Jumla ya mashirika yasiyo ya kiserikali (Azaki)60 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa watanufaika na mradi Uraia Wetu,ambao umelenga kuyajengea uwezo wa kufanya kazi pamoja na kuwa na sauti ya pamoja katika kushughulikia changamoto mbalimbali.

Mradi huo ambao unasimamiwa na kutekelezwa na Shirika linalotetea na kulinda haki za watoto ( NELICO) kwa ufadhili wa Foundation For Civil Society(FCS) ambapo unotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu 2023 hadi 2025 na kugharimu kiasi cha milioni 110.

Ofisa Mradi wa Uraia Wetu kutoka NELICO Eva Onesmo

Hayo yamebainishwa na Ofisa Mradi huo kutoka NELICO Eva Onesmo ,wakati akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa Uraia Wetu,ambapo ameeleza kuwa lengo ni uwajengea uwezo mashirika yasiyo ya kiserikali Azaki ili yaweze kufanya kazi zake kihalali,kisheria bila kuwa na migogoro wala changamoto yoyote.

Anaeleza kuwa kwa sababu wanafahamu kwamba Azaki zipo kwa ajili ya kusaidia shughuli za serikali hivyo wanazijengea uwezo na lengo kubwa wakifika mwisho wa mradi kama sekta wawe na sauti ya pamoja kwa maana kwamba wanapotakiwa kutatua au kushughulikia changamoto yoyote wana sekta wote nchini wawe na sauti moja.

“Kuwatengenezea mazingira salama katika utekelezaji wa kazi zao mradi ambao ni fursa katika sekta ya mashirika hayo kwani umujikita huko unaotekelezwa Tanzania nzima,ambao umegawanyika katika ngazi kuu tatu ,taifa, Kanda ambapo NELICO tumepata fursa ya kusimamia Kanda ya Ziwa nzima kwa mikoa ya Mwanza, Shinyanga,Simiyu,Kagera,Geita na Mara, ni fursa kwa wanasekta kufanya kazi moja kwa moja na serikali kwa ukaribu na kuangalia namna gani kwa pamoja tunaweza kutengeneza mazingira rafiki kwa Azaki,”ameeleza Onesmo.

Kaimu Mkurugenzi wa NELICO Eddy Kennedy

Kaimu Mkurugenzi wa NELICO Eddy Kennedy amesema,lengo kuu pia la mradi wa Uraia Wetu ni kuweka nguvu ya pamoja kwa jamii zenye kero ikiwemo kuondoa migongano ya kisheria.

Kennedy amesema shughuli za uchechemuzi siku zote zinahitaji nguvu ya pamoja ukienda Azaki moja na Azaki nyingine kivyake vyake kidogo uwa ni changamoto.

“Ili serikali ipate kujua taarifa tunazozitoa,yale ambayo tunayaibua huku chini kama kero za wananchi zina nguvu au zina uhalisia wowote tuungane kuwa na lugha moja,tuweke nguvu zetu pamoja tupeleke ujumbe ambao umedhamiria kuleta mabadiliko,”.

Anaeleza kuwa mradi huo umeletwa kutokana na mapungufu mbalimbali ambayo wameyaona yapo katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kikatiba na sheria ambayo yanaleta mkanganyiko na mgongano yanayowapa changamoto katika kusimamia demokrasia nchini.

Hivyo wakaona kuwa wanahitaji nguvu ya pamoja kwasababu wanafanya kazi na jamii ambao ndio watu wanaopitia kero mbalimbali ambazo zinasababisha kuwa na haja ya kubadili katiba au sheria.

“Kutokana na changamoto zinazoletwa na sheria na migogano mbalimbali mfano sheria hiyo ya ndoa inayomruhusu mtoto mwenye umri wa miaka kati ya 14 na 15 kuolewa na ukizingatia kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inamtambua mtoto ni mtu yoyote mwenye umri chini ya miaka 18, unakuta kuna mgongano sasa tunasema kuna haja ya sisi kuja pamoja kama Azaki zimazofanya kazi na jamii kuwa pamoja,nguvu moja,sauti moja,kauli moja kupeleka hoja kwa vyombo vya maamuzi iwe Bungeni au kwa yoyote anatefanya maamuzi ili tuweze kubadilisha tuondoe migongano ilikuwa na sheria ambazo ni rafiki kwa watu na kuleta usawa,”amesema Kennedy.

Mratibu wa Mtandao wa Ushirikiano wa Vyombo vya Habari na AZAKI Tanzania (TMSN),Edwin Soko

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao wa Ushirikiano wa Vyombo vya Habari na AZAKI Tanzania (TMSN),Edwin Soko amesema kuwa, mradi huo utaongeza uwezo wa raia kujua haki za kiraia kwa mapana na hii italeta mabadiliko makubwa kwenye jamii.

Soko amesema kuwa TMSN kupitia wanachama wake watakuwa mabalozi wazuri wa utekelezwaji wa mradi huo huku wakiunga mkono na kuleta mabadiliko kwa kufanya uchechemuzi wa Uraia Wetu ambao umekuja wakati muafaka hasa kama taifa linaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

“Mradi huu wa Uraia Wetu utakuwa na manufaa makubwa kwa Azaki zetu za Kanda ya Ziwa kwa sababu zinaletwa pamoja,kujadiliana hali nzima ya Uraia Wetu ambao ni uwanja mpana ikiwemo ni jinsi gani watu wanauelewa wa haki yao ya kupiga kura na mambo mengine,”amesema Soko.