June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Upatikanani  pembejeo wawanyanyua wakulima Hanang


 
 
Na Mwandishi Wetu, Hanang — Manyara
 
Wakulima wa zao la mahindi Wilayani Hanang mkoa wa Manyara, wameipongeza Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, hatua iliyochangia ongezeko kubwa la mavuno msimu huu.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima hao walisema kuwa utoaji wa ruzuku ya mbolea, upatikanaji wa mbegu bora, pamoja na huduma za ugani zilizotolewa kwa karibu na maafisa kilimo, vimekuwa chachu ya mafanikio katika uzalishaji wa mahindi mwaka huu.
 
“Tunaishuru na kuipongeza Serikali kwa programu hii ya pembejeo. Tumezipokea kwa wakati, ikiwa ni pamoja na elimu kutoka kwa maafisa ugani iliyotusaidia kuboresha ukulima wetu. Mvua pia zilikuwa za kutosha, na matokeo yake ni mavuno mazuri kuliko miaka iliyopita,” amesema Kibaisi Maideshi mkulima kutoka eneo la Endasaki.
 
Kwa mujibu wa Maideshi, juhudi za Serikali zimeanza kuleta matokeo chanya mashambani, huku wengi wao wakisisitiza kuwa kwa sasa kilimo kimeanza kuonekana kuwa na tija, hasa kwa wakulima wanaofuata maelekezo ya kitaalamu.
 
“Tunafarijika kuona kuwa juhudi zetu zimezaa matunda. Tunaiomba Serikali iendelee kutusaidia zaidi kwa kutuongezea mafunzo juu ya ukulima wa kisasa, na kuhakikisha kuwa huduma bora za ugani zinaendelea kutufikia kwa wakati ili kuendana na msimu,”ameongeza



Mkulima mwingine aliyejitambulisha kama Maria Bashiri amesema upatikanaji wa pembejeo umesaidia siyo tu kuongeza uzalishaji bali pia kunyanyua hali ya kimaisha hasusani kwa wakulima wadogo ambao maisha yao ya kila siku yanategemea uzalishaji wa mashambani.
 
“Ukosefu wa pembejeo ni moja kati ya changamoto kubwa iliyokuwa inafanya maisha ya wakulima wadogo kama mimi kubaki pale pale. Baada ya utaratibu huu wa ruzuku ulioletwa na Serikali, maisha yetu yanaanza kubadilika taratibu kwa kuwa tunaweza kufanya kilimo chenye tija na uzalishaji zaidi na hivyo kutusaidia kuboresha hali ya familia zetu,”amesema
 
 
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Chemba ya biashara,viwanda na kilimo (TCCIA) Manyara, Zainab Rajabu amesema programu ya pembejeo kwa wakulima imesaidia sana kuboresha kilimo na kufafanua kuwa msimu huu wakulima wamevuna kwa wingi kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwenye upatikanaji wa pembejeo na usimamizi wa karibu wa shughuli za kilimo.


 
“Tunaendelea kuhamasisha wakulima kutunza mavuno yao vizuri na kushirikiana kupitia vyama vyao vya ushirika ili kuongeza ufanisi na tija zaidi,” amesema.
 
Wakulima wamehimizwa kuendeleza ushirikiano na taasisi za kilimo pamoja na kuchangamkia fursa za mafunzo na teknolojia mpya zinazolenga kuongeza thamani ya mazao yao na kuimarisha kilimo chenye tija kwa maendeleo endelevu.