Asilimia kubwa ya wananchi hao walikuwa wakitumia maji yasiyo salama ya visimani na katika madimbwi ,hali ambayo iliwaletea shida katika afya zao kutokana na baadhi ya wananchi kuumwa vichocho na kuhara damu.
Kwa kuona hilo Miradi ya Maendeleo ya Kijamii(LADP),chini ya Mradi Mkubwa wa Kufua Umeme wa Rusumo uliopo katika Mpango wa Bonde la Mto Nile(Nile Basin Iniative NELSAP)uonafadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank),iliamua kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo kuwafikishia maji safi na salama wananchi wanaoishi karibu na mradi huo.Kupitia mradi huo, wananchi wapata fursa ya kuchagua eneo la maji baada ya kuona ni namna gani wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yao.
Wanawake ndio wahanga wakubwa wa matukio mbalimbali ikiwemo kuchota maji kwa umbali mrefu huku familia ikimsubiri,migogoro ya ndoa pamoja na kukumbana na wanyama wakali pindi wanapoenda kuchota maji hususan nyakati za alfajiri.
Alex Bushahu Mkazi wa Kijiji cha Kasulo Kitongoji cha Ngoma anasema eneo la songambele ni miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa na uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa kipindi cha muda mrefu.Â
Anasema awali wananchi wake walikuwa wakichota maji katika madimbwi ambayo yalikuwa yakipatikana kwa umbali wa Kilometa Moja na nusu,ambapo maji hayo yalikuwa si safi wala salama ka matumizi ya binadamu.
Upatikanaji maji vijiji vya Ngoma,Benguka ulivyoleta matumaini mapya kwa wananchi Bushahu anasema kutokana na uhaba huo wa maji watu walilazimika kuchota maji hayo na kuyatumia ambapo yalikuja kuwaletea madhara makubwa watu kuugua Kichocho na kuhara damu.
”Hali ya wanakijiji cha Ngoma ilikuwa ni mbaya sana katika upande wa maji safi na salama,wamama walikuwa wanaamka usiku kwenda kuchota maji ambapo ukutana na vitu mbalimbali wakiwemo wanyama wakali,”anasema na kuongeza
”Bado ukifika huko utakutana na foleni ambayo ni lazima mtu akae ili aweze kusubiri foleni ipungue zamu yake ikifika na yeye achote maji,huku familia inamsubiri huku mwanaume anataka kumuona mama amerudi mapema basi migogoro ya familia ilikuwa ni mingi kuliko sasa,”anasema.
Anaishukuru NELSAP kupitia mpango wake wa Miradi ya Maendeleo ya Kijamii (LADP) kwa hatua kubwa walioichukua ya kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho cha Ngoma kwani sasa hivi hali imebadilika wapo vizuri kiafya na hata migogoro ya familia imepungua .
Anasema kutokana na uwepo wa maji ya uhakika kijiji chao sasa kimekuwa miongoni mwa vijiji vyenye maendeleo watu wameanzisha miradi ya bustani katika magati ambayo yapo karibu na mabomba na kufanya maendeleo yakue kwa kasi.
Anasema kijiji hicho kina idadi ya kaya 30 huku idadi ya watumiaji maji katika kaya hizo ni 150 ambapo kila mwezi kila kaya inapaswa kulipia maji hayo 1000 ambapo ukusanywa na kupelekwa,Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ambapo fedha hizo zinakuwa kwaajili ya ukarabati wa bomba endapo litaharibika na matumizi mengine yanapotokea.
”Kwa kweli tunashukuru sana kwa hatua hii ya NELSAP sasa hivi maji yako karibu na watu wanachota maji muda wowote ule wanapoyahitaji haya ni maendeleo makubwa katika kijiji chetu cha Ngoma,”anasema na kuongeza
”Tunaomba NELSAP isiishie hapa iendelee katika vijiji vingine kusaidia huduma hii iweze kupatikana kwa uhakika na watu waweze kupata maendeleo yao kwani ikiwa muda mrefu watu wanatumia kutafuta maji,maendeleo ukosekana” anasema.
Kwa upande wake Mtaokeo Mkuthe Msimamizi wa Mradi wa Maji Benako Benguka Kijiji cha Lakalemela Wilayani Ngara anasema wanaishukuru NELSAP kupitia LADP kwa kuwafanyia maboresho makubwa ya bomba ambalo lilikuwa linategemewa na wananchi wengi wa Benako.
Anasema uboreshaji huo wa bomba umeweza kuwasaidia kwa asilimia kubwa kuondokana na adha ya maji ambapo awali walikuwa wanakumbana nayo kutokana na foleni ya usubiriaji wa maji kuwa kubwa.
”Kwa kweli tunashukuru sana sana NELSAP kwa kuja kutufanyia maboresho katika bomba letu na kuhakikisha sasa maji yanatoka mengi na ya uhakika tofauti na miaka ya nyuma maji yalikuwa hayatoki kwa wakati kutoka na miundombinu iliyowekwa tangu zamani kutokuwa mizuri na kutoendana na wakati.
”Miaka ya nyuma watu walikuwa wachache ila kwa sasa tupo watu wengi hivyo maji yaliyokuwa yanatoka awali yalikuwa hayatutoshelezi kutokana na wingi wa watu hivyo kusababisha wamama kudamka alfajiri kuja kupanga foleni kwaajili ya kupata maji,”anasema.
Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji Maji Benguka,Josephilda Tinuga anasema ukosekanaji wa maji kwa kipindi cha nyuma ulikuwa wa hali ya juu hali ambayo wakinamama walikuwa wakigombana na wanaume zao kutokana na kuchelewa katika maji.
Amesema pia watoto walikuwa hawaendi shuleni kutokana na kusubria maji yatoke au kukaa katika foleni ili waweze kukapa maji hivyo kusababisha utoro kukithiri katika shule zao.
”Uwepo wa maji katika Kijiji cha Ngoma na Lekalemela umeweza kutusaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na shida za maji za awali tulizokuwa tunazipata,hivyo tunasimamia vizuri mradi huu ili uwe endelevu kwani ni huduma ambayo inatusaidia sisi wenyewe na familia zetu,”amesema na kuongeza
”Awali watu walikuwa wanapata changamoto kweli kwani dumu moja lilikuwa linauzwa 500 hadi 1000 kwa baadhi ya maeneo ambapo mtu mmoja anauwezo wa kutumia madumu hata manne au matano kwa siku kwa familia moja ila kwa sasa hivi kila kaya inapaswa kulipa kiasi cha sh.1000 kwa mwezi ambapo imesaidia kurahisisha maisha,”amesema.
Naye Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ya Kijamii upande wa Tanzania (LADP),Irene Chalamila anasema NELSAP chini ya LADP imeweza kuwa na mradi wa maji safi kwaajili ya wananchi wa rusumo ambapo mradi wa kufua umeme upo.
Anasema lengo kubwa la mradi huo ni kuwasaidia kwa urahisi wananchi wa Rusumo na maeneo mbalimbali ambapo mradi wa kufua umeme ulichukua ardhi zao ili kuendeleza mradi huo.
”Kama faida kwao pamoja na kulipa zile fidia za kuchukua maeneo yao, tuliona ni vizuri kuwapatia miradi mbalimbali kwa lengo la kuboresha maisha yao ambapo miongoni mwa miradi hiyo pamoja na kuwafikishia wananchi wa Rusumo na maeneo jirani maji safi na salama ya kutumia,”amesema.
”Maji tunayachukua kutoka mto Ruvu ambapo yanapampiwa na kuyafanyia ‘treatment’ yote ya kuweka dawa za kuua vijidudu na kupeleka katika tanki za juu kisha tunayapeleka katika vijiji,”anasemaÂ
Anasema hali ya maji ilikuwa sio nzuri, kwa wananchi wa Rusumo na maeneo jirani awali wengi walikuwa wakitumia maji ya mto ruvuvu au Akagera ambayo yalikuwa hayajatayarishwa ipasavyo
More Stories
Hivi ndivyo TASAF ilivyoshiriki kumaliza kilio cha wananchi Kata Bwawani, Arusha
Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni