Na Jackline Martin, TimesmajiraOnline, Dar
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip
Mpango, amesema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suuhu Hassan, mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji yameimarika na kuwa bora zaidi kwa kipindi kifupi.
Makamu wa Rais Dkt. Mpango aliyasema hayo jana wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa mwaka 2024 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara,
licha ya misukosuko ya uchumi na kijamii inayoendelea Duniani kote.
Aliongeza kwamba katika mwaka 2023, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuwa asilimia 5.0 ikilinganishwa na asilimia 4.7 mwaka 2022 huku matarajio kwa mwaka 2024 ni ukuaji wa asilimia 5.5.
Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa Jukwaa hilo kutoa maoni na
mapendekezo kwa uhuru ili kuweza kuboresha vema sera za kodi na uwekezaji nchini.
Alisema maoni yatakayotolewa katika Jukwaa hilo yatatumika katika
mchakato wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Aidha amewataka Mawaziri wa Fedha kuzingatia ushauri wa sekta binafsi na walipa kodi wote ili wadau waone umuhimu wa ushiriki wao katika jukwaa hilo.
Halikadhalika alitoa wito kwa washiriki kujikita katika kuibua njia za kibunifu zitakazosaidia kuongeza mapato ya Serikali bila kuumiza wafanyabiashara na Wawekezaji.
Amewataka kujadiliana kwa kina kuhusu namna ya kutumia zaidi
ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, mathalan kupitia hatifungani zitakazotolewa na taasisi na mashirika ya umma kugharamia miradi ya maendeleo.
Pia aliwasihi mijadala kujielekeza katika kubaini na kudhibiti
vihatarishi vya matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ikiwemo wizi wa kimtandao na utoroshaji wa mitaji.
Makamu wa Rais alisema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani imeendelea kufanya maboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa kodi ili kujibu malalamiko ya wawekezaji ikiwemo Kurekebisha sheria za kodi, Kuweka utulivu wa sera za kodi, Kuendelea kujenga na kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara ikijumuisha ujenzi wa vituo 10 vya utoaji
huduma kwa pamoja mipakani (One-Stop Border Posts), Kufanya mapitio na kuhuisha sera na sheria mbalimbali pamoja na kukamilisha Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuunganisha mifumo ya taasisi saba (7) ambazo ni NIDA, TRA, BRELA, TIC, Kazi, Uhamiaji na
Ardhi.
Pia alisema hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na Kuanzisha Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya Walipakodi, kuwianisha majukumu ya kitaasisi ili kurahisisha utoaji huduma, kuendelea kufanya mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara pamoja na kutoa vivutio vya
kikodi ikiwemo kutoa misamaha ya kodi na kiwango cha asilimia sifuri (0) cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mtaji na malighafi.
Makamu wa Rais amesema makusanyo ya mapato ya Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaliongezeka kwa asilimia 22.1 kutoka Sh. trilioni 17.6 mwaka 2020/21 hadi sh. trilioni 22.6 mwaka 2022/23.
Ongezeko hilo la ukusanyaji wa mapato limeiwezesha Serikali kuendelea kuongeza Bajeti yake kutoka sh. trilioni 36 mwaka 2021/22 hadi Sh. trilioni 44.4 mwaka 2023/24.
Alisema ongezeko la bajeti limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na injini na mabehewa yake, mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (94.8%, mradi wa Kinyerezi I Extension (100%) na mradi wa kufua Umeme wa Maji Rusumo (99.7%).
Vilevile kupeleka huduma ya umeme kwenye vijiji 10,987 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara (sawa na 89.19%), ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara na madaraja unaendelea ambapo jumla ya miradi 23 ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na daraja la Kigongo – Busisi (80.0%).
Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Wizara inatambua umuhimu wa kuongeza ushirikishwaji wa wadau kwa kuwa bado kuna changamoto katika masuala ya kujenga uchumi na kukuza ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Alisema bado ipo changamoto katika ulipaji wa kodi kwa hiari hasa matumizi ya mashine za kielektroniki na utoaji risiti.
Waziri Nchemba alisema bado ipo tabia ya kuwepo na visingizio mbalimbali vinavyopelekea kutotolewa kwa risiti za kielektroniki ikiwa ni pamoja na mnunuzi kuongozwa kukwepa kodi kwa kupewa bei ya chini ya bidhaa kutoka kwa muuzaji kwa sharti la kutopewa risiti.
Alisema Jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ikikumbukwa utaratibu ambao umekuwa ukitumika siku zote ni kupata maoni ya wadau kupitia Vikao vya Kamati ya Maboresho ya Sera za Kodi.
Aliongeza kwamba katika kuhakikisha wadau wengi zaidi wanashiriki kutoa maoni, Wizara iliandaa Jukwaa la Kodi lililofanyika tarehe 11 Januari 2023 jijini Dar es Salaam ili kupata maoni yao
badala ya kuwasubiria kwenye vikao vya Kamati.
Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tangu mwaka 2019 – 2023 Serikali imefanya mabadiliko na maboresho ya kisera, kisheria na kikanuni 665 yanayohusu kodi na yasiyohusu kodi.
Alisema kati ya hayo maboresho 416 yamelenga kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini huku maboresho 460 yakiwa yamefanyika katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Aliongeza kwamba kwa sasa Tanzania inakidhi vigezo vikubwa vya
mazingira bora ya uwekezaji ikiwemo vigezo vya kuwa na utulivu wa kisiasa na amani, mazingira bora ya kisheria na urekebu, uwepo wa soko la bidhaa zitakazozalishwa,utulivu wa kiuchumi, vipaji na nguvukazi, ubora wa miundombinu, viwango vya chini vya kodi, uwepo wa ardhi pamoja na uwepo wa fedha za kugharamia miradi ya uwekezaji wa ndani.
Kauli Mbiu ya Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024 ni “Maboresho ya sera katika uwekezaji, ukusanyaji wa mapato ya ndani na ukuaji wa uchumi jumuishi”
More Stories
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi
Muhoji Sekondari kumaliza changamoto ya umbali kwa wanafunzi Musoma vijijini
Tanzania mwenyeji mkutano wa nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika