*Aiwezesha kuongeza vifaa tiba vya uchunguzi wa maabara vyenye uwezo mkubwa wa kuchakata sampuli za maabara 2,500 kwa saa moja
Na Joyce Kasiki, TimesmajiraDodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeimarisha huduma za uchunguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Hayo yamesemwa jijini Dodoma hivi karibuni na Dkt. Rachel Mhaville kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne kwa Hospitali ya Muhimbili kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema chini ya uongozi wa Rais Samia, Serikali imeweza kuongeza Vifaa Tiba vya Uchunguzi wa Maabara vyenye uwezo mkubwa wa kuchakata sampuli za maabara takribani 2,500 kwa saa moja ili kuongeza upatikanaji haraka wa majibu na kupata matibabu mapema kwa wagonjwa wa nje na waliolazwa.
Dkt. Mwavile alisema vifaa hivyo vina thamani ya sh. bilioni 1.8. Kwa mujibu wa Dkt. Mhaville upatikanaji wa vifaa hivi umerahisisha utoaji wa majibu kwa haraka, magonjwa kugundulika haraka, kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri matibabu na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kibobezi ikiwemo upandikizaji mimba (IVF), upandikizaji figo na uloto
Alisema katika jitihada za Serikali za kuthibitisha ubora wa vipimo na majibu yanayotolewa na maabara kwenye viwango vinavyokubalika kimataifa ili kutumika na mamlaka au taasisi yoyote duniani, Serikali imeendelea kuboresha maabara zetu na hatimaye kwa mara nyingine Shirika la Viwango vya Ukaguzi Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADCAS) liliweza kutunuku cheti cha Ithibati ya Ubora wa Maabara (ISO 15189:2022) kwa Kampasi ya Upanga na Mloganzila.
Ili kuhakikisha ubora wa huduma zinazotolewa, hospitali imeanzisha Benki ya kuhifadhi sampuli na vimelea kwa ajili ya tafiti (Biorepository).
“Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanikiwa kuanzisha benki ya kuhifadhi sampuli kwa ajili ya mafunzo na tafiti za kisayansi mbalimbali wa vimelea vya magonjwa kupitia maabara kuu ikiwa ni ya kwanza katika hospitali za umma iliyolenga kuboresha huduma za tafiti za kisayansi na mafunzo,”alisema.
Kuhusu ununuzi wa Vifaa Tiba vya Uchunguzi, Tiba kupitia Mionzi na Mawimbi, Dkt. Mhaville alisema Serikali imenunua na kusimika mtambo wa kisasa (Angio-Suite) wa Tiba Radiolojia (Interventional Radiology) uliogharimu sh. bilioni 2.
Alifafanua kuwa mtambo huo umewezesha hospitali kutoa matibabu ya ubingwa bobezi ambayo yalikuwa hayapatikani hapa nchini na kuongeza idadi ya aina za matibabu ya kibobezi katika eneo hilo ambapo takribani wagonjwa 2,300 wamehudumiwa tangu ulipofungwa mwaka 2022.

Aidha, kupitia mtambo huo, kwa mara ya kwanza nchini, Hospitali imefanikiwa kuanzisha huduma mpya za kuweka mirija myembamba (catheters) kwa kutumia matundu madogo, kutoa damu iliyoganda katika mishipa ya damu na nyinginezo nyingi ambazo zinafanyika kwa ustadi wa hali ya juu.
Aidha, alisema Serikali ilinunua mashine mpya ya Mammography iliyogharimu sh. bilioni .8 ambayo ina uwezo wa kupima na kutoa picha zinazoweza kugundua uvimbe kwenye matiti ukiwa katika hatua za awali kabisa.
Aidha, alisema wagonjwa 810, wamehudumiwa kwa kutumia mashine hiyo tangu iliponunuliwa mwishoni mwa mwaka 2024.
“Mashine hii ambayo ni kisasa na pekee kwa hospitali za umma, inatumiwa na madaktari wabobezi wa radiolojia ya wanawake imeleta mapinduzi ya utoaji wa huduma za uchunguzi wa kisasa kwa wenye magonjwa ya matiti nchini,” alisema.
Dkt. Mhaville Serikali imeongeza mashine moja ya CT-Scan (dual) iliyogharimu sh.1.8 yenye uwezo wa vipande 128 hivyo kuongeza idadi ya wagonjwa wanaopimwa kwa siku kutoka 20 hadi zaidi ya 50 na majibu kupatikana kwa haraka, kumwezesha daktari kufanya maamuzi mapema na wagonjwa kupata matibabu stahiki kwa wakati.
Aidha, katika kipindi hichohicho, Serikali imeongeza mashine moja ya MRI yenye nguvu sumaku ya 1.5T ambayo inaweza kuona uvimbe mdogo kabisa katika kupiga picha za uchunguzi iliyogharimu sh. bilioni 2.6 Bil.
Hiyo imesaidia kuondoa muda wa mgonjwa kusubiri kati ya siku 4 hadi 5 ambapo sasa kipimo hicho kinfanyika siku hiyo hiyo aliyoandikiwa mgonjwa. “Haya ni mafanikio makubwa katika kuboresha huduma za matibabu nchini,” alisema.
Pia alisema Mashine ya Kidigitali ya X-Ray iliyogharimu kiasi cha sh. milioni 358 ambapo kutokana na uwekezaji huo, Hospitali imefanikiwa kupunguza muda wa kutoa majibu ya radiolojia (turn-around time) kutoka saa 48 hadi 24 tangu mgonjwa anapopima.
Aidha, alisema hospitali ilifanikiwa kununua vifaa vingine vingi ikiwemo mashine za kusaidia wagonjwa kupumua 18 zilizogharimu kiasi cha sh. milioni 932, mashine za endoskopia zilizogharimu sh. milioni215.
More Stories
DAWASA:Upatikanaji huduma ya maji Dar asilimia 93
Mmoja afariki,33 wajeruhiwa ajali ya tingatinga na coaster
Siku saba ziara ya Samia zilivyopelekea neema Tanga