November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uongozi Shule ya Holyland watumia mbinu mbadala kuinua elimu Mbeya

Na Esther Macha, Timesmsjira,Online,Chunya

ILI kuinua kiwango cha elimu Wilayani Chunya mkoani Mbeya uongozi wa shule ya Holyland iliyopo Mji mdogo wa Makongolosi umekuwa uikitumia mbinu za kuzungumza na wazazi waliopo katika mji huo ili waweze kufahamu umuhimu wa elimu kwa watoto badala ya kuwapeleka kwenye shughuli za uchimbaji na kilimo cha tumbaku .

Akizungumza na Timesmajira,Online kuhusiana na mikakati ya kuinua elimu katika Mji wa Makongolosi, mkuu wa shule ya mchepuo wa Kiingereza Holyland, Kenya Mahada amesema katika vikao hivyo, ambavyo ushirikisha wanajamii na wazazi vilenga kuwawezesha kufahamu umuhimu wa elimu kwa watoto .

“Sisi huwa tunaitisha vikao kwa wanajamii na wazazi na hata wale ambao watoto wao hawasomi katika shule yetu na kuzungumza nao, lakini pia tumekuwa tukitembelea maeneo mbalimbali hasa vijijini kuwapa mwamko wa kuwaleta watoto shule kupata elimu ili kusaidia jamii ya kitanzania ambayo ipo pembezoni,” amesema Mahada.

Mkuu wa shule ya mchepuo wa Kiingereza Holyland, Kenya Mahada

Akizungumzia kuhusu kuinua kiwango cha elimu, amesema huwa wanashirikiana katika michezo na kuandaa mada mbali mbali na shule zingine za mchepuo wa kiingereza zilizopo mkoani Mbeya eneo la Mbalizi lengo ni kuwashirikisha watoto ili waweze kuinuka katika nyanja mbali mbali za kimasomo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza iitwayo HolyLand iliyopo wilayani Chunya ambayo ni ya awali na msingi, Lawena Nsonda (Baba Mzazi) amesema shule hiyo imefanya vizuri kwenye mtihani wa Mock kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake kwa kushika nafasi ya kwanza kiwilaya .

Lawena amesema katika shule hiyo wana utaratibu wa kuwapeleka watoto kwenye vivutio ya utalii ili waweze kujifunza kwa vitendo waweze kupata mwamko wa kusoma vizuri.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema mwelekeo wa shule hiyo ni kuwapeleka kwenye vivutio vya utalii watoto wa shule pamoja na wazazi ili waweze kupata moyo wa kusomesha watoto wao.

Mkurugenzi wa shule ya mchepuo wa kiingereza iitwayo HolyLand iliyopo wilayani Chunya ambayo ni ya awali na msingi, Lawena Nsonda (Baba Mzazi)

Naye Mwalimu wa shule ya awali na Msingi HolyLand iliyopo katika Mji mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya, Mwanaidi Albert amesema lengo la ziara hiyo ya kwenye vivutio vya utalii ambayo ilijumuisha watoto ,wazazi pamoja na walimu ni kuwawezesha kuona vivutio vya ndani, ili waweze kujua nchi ina vitu gani pamoja na kujifunza .

Aidha, Mwalimu Mwanaidi amesema wanafunzi walifurahi ikiwa ni pamoja kujifunza tabia za wanyama na kuwa baada ya kutoka kwenye vivutio hivyo wanafunzi wamekuwa na mabadiliko makubwa kwenye masomo darasani .