November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Unyonyeshaji sahihi upunguza udumavu na utapiamlo kwa watoto

Na Suleiman Abeid,Timesmajira Online

AGOSTI Mosi hadi Agosti 07 ya kila mwaka dunia huadhimisha wiki ya unyonyeshaji ikiambatana na uhimizaji wa lishe bora kwa wanawake wajawazito na watoto maadhimisho ambayo yali asisiwa mnamo mwaka 1990 nchini Italia katika mji wa Florence.

Kuasisiwa kwa maadhimisho haya kulitokana na sababu kadhaa wa kadhaa ambazo zilisababisha tatizo la vifo vingi vya watoto wachanga na wadogo na wakati mwingine akinamama wajawazito kupoteza maisha wakati wakijifungua.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akigawa uji wa lishe kwa baadhi ya watoto katika maadhimisho ya Siku ya unyonyeshaji na lishe.

Pamoja na juhudi za kuboresha huduma za afya, chanjo na matibabu ya magonjwa ya watoto lakini hali ilibaki ama kuzidi kua mbaya huku maelfu ya watoto wakipoteza maisha.

Tafiti mbalimbali zilizoendeshwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa zilibaini pia moja ya changamoto inayochangia vifo vya watoto wachanga ni wanawake walioajiriwa kushindwa kunyonyesha watoto wao ipasavyo.

Hali hiyo ilisababishwa na wanawake hao kunyimwa likizo ya uzazi ya kutosheleza kutimiza wajibu wao wa uzazi na jukumu la kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato kukabiliana na changamoto za usawa wa kijinsia katika ajira na utumishi.

Katika kukabaliana na changamoto za vifo vya watoto wachanga kutokana na kutonyonyeshwa kikamilifu, miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa kwenye kikao kilichofanyika Julai 30 hadi Agosti mosi mwaka 1990 ilikuwa ni kuzitaka nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi kwa wa wanawake kunyonyesha watoto wao maziwa pekee kwa miezi sita baada ya kujifungua.

Katika kikao hicho lilipitishwa azimio la Inocenti la kuanzishwa kwa maadhimisho endelevu ya wiki ya Unyonyeshaji Duniani kila tarehe 01 Agosti hadi Agosti 07 ya kila mwaka ili iwe wiki ya hamasa kuikumbusha jamii umuhimu wa unyonyeshaji watoto maziwa ya mama na yalianza rasmi mwaka 1992.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme (mwenye gauni jeusi) na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi (kushoto) wakinywa uji wa lishe baada ya kuzindua maadhimisho ya siku ya Unyonyeshaji na Lishe ambayo yamefanyika kimkoa Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa duniani ambayo huadhimisha wiki ya unyonyeshaji sambamba na uhimizwaji wa lishe bora kwa watoto ambapo kwa Kauli mbiu ya wiki hiyo kwa mwaka huu wa 2023 inasema “saidia unyonyeshaji, wezesha wazazi kulea waoto na kufanya kazi zao kila siku”.

Maadhimisho haya yamelenga kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuendeleza na kusaidia unyonyeshaji na ulishaji bora wa watoto na fursa maalum kwa watu wote kuendeleza na kuimarisha unyonyeshaji maziwa ya mama kama njia bora zaidi ya kujenga afya ya mama na mtoto kimwili na kiakili.

Mkoani Shinyanga maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika Soko la Ndala Manispaa ya Shinyanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ambaye ametoa wito kwa akinamama wenye watoto wachanga kuhakikisha wanawanyonyesha watoto wao miezi sita bila kuwapa chakula chochote kingine wala maji.

Mndeme amesema iwapo akinamama watawanyonyesha watoto wao kwa kuzingatia muda huo wa unyonyeshaji kwa miezi sita itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha udumavu hali itakayowawezesha watoto kukua wakiwa na afya njema na ustawi.

Anasema,maziwa ya mama yana sifa ya kipekee ya kuwa na kinga ya mwili ambayo humkinga mtoto dhidi ya magonjwa, hivyo kuchangia kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na kujenga mahusiano mazuri kati ya mama na mtoto wake.

Mkuu huyo anatoa wito kwa akinamama wote wanaojifungua wahakikishe mtoto ananyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa ili kusaidia maziwa yatoke mapema na anyonyeshwe maziwa ya mama pekee bila ya chakula na kinywaji kingine (hata maji) katika miezi sita ya mwanzo.

Kwa upande wa Lishe Mkuu huyo wa Mkoa anasema Serikali inatambua bado zipo changamoto nyingi katika kukabiliana na utapiamlo hapa nchini na moja ya changamoto kubwa kuliko zote ni uelewa mdogo wa masuala ya lishe katika jamii ikiwemo unyonyeshaji, kuanzia ngazi ya familia hadi watendaji na viongozi wa serikali.

Mmoja wa akinamama wenye watoto akitoa ushuhuda jinsi alivyomnyonyesha mwanae maziwa pekee kwa miezi sita bila matatizo yoyote.

“Uelewa mdogo kuhusu masuala ya lishe pia umesababisha masuala ya lishe kutopewa kipaumbele katika jamii ambako ndiko waliko watoto na wanawake wengi wanaohitaji zaidi huduma bora za lishe,” anaeleza Mndeme.

Ili kuhakikisha masuala ya lishe bora yanaendelea kuimarika mkoani Shinyanga Mkuu huyo wa Mkoa anatoa wito kwa maofisa watendaji wa kata, vijiji na mitaa ndani ya Mkoa kuhakikisha wanasimamia na kuadhimisha siku ya afya na lishe za vijiji/mitaa (SaLiKi) kila robo ya mwaka.

Anasema maadhimisho haya ya ngazi ya vijiji na mitaa yafanyike kwa ushirikiano na wataalamu wa afya na lishe ngazi zote ili kutoa elimu kwa wananchi wote wa maeneo husika huku akitoa wito kwa wananchi kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa ili kuboresha lishe na afya ya mama na mtoto.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile anasema suala la unyonyeshaji ni muhimu kwa watoto wachanga kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita na kwamba humsaidia mtoto kukua akiwa na afya njema.

Anasema iwapo akinamama watazingatia suala la unyonyeshaji itachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 32 mpaka asilimia 24 na pia kuhakikisha kupunguza ukondevu kutoka asilimia 4.5 mpaka kufikia asilimia 1.3.

Ofisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Yusuph Hamisi anasema lishe bora ni ile inayozingatia ulaji unaofaa na kuzingatia ulishaji wa watoto kwa kuzingatia makundi matano muhimu ya vyakula na kwamba Mkoa wa Shinyanga una asilimia 27.5 ya watoto waliodumaa kutokana na ukosefu wa viinilishe vya kutosha kwa muda mrefu.

Hamisi anasema, “…Tunaposema muda mrefu, udumavu unatokea tangu mtoto anapokuwa tumboni kwa mama tangu mimba inapotungwa mpaka mtoto anapofikisha miaka miwili ambacho huwa ni kipindi muhimu kwa ajili ya kutengeneza mtoto asipate udumavu,”.

“Kwani udumavu hauathiri mwili pekee bali unaathiri na akili, hivyo tunaposema ulishaji ni lazima kwanza tuhakikishe akinamama wajawazito wanakula vyakula kulingana na makundi yote matano na baada ya mjamzito kulishwa vizuri, lakini ahudhurie kwenye vituo vya afya ili aweze kupata ushauri na huduma nyingine za afya,”.

Baadhi ya wakazi wa mji wa Shinyanga, Lembe Mashaka, Esther Wilson na Asha Bakari wanasema iwapo elimu ya unyonyeshaji ikiendelea kuhimizwa na kutolewa mara kwa mara ni wazi watoto wengi watazaliwa wakiwa na afya njema.

“Mbali ya elimu ya unyonyeshaji na Lishe lakini vilevile viongozi wetu wa Manispaa ya Shinyanga waboreshe masoko yaliyoko kwenye kata zetu ili wananchi waweze kujipatia mahitaji muhimu kwa ukaribu ikiwemo matunda na mbogamboga ambavyo ni muhimu katika uboreshaji wa lishe kwa watoto na akinamama wajawazito,” anaeleza Esther Wilson.

Wataalamu wa masuala ya afya wanaeleza kuwa utapiamlo hata katika kiwango kidogo hudhoofisha mfumo wa kinga za mwili na na kuongeza uwezekano wa vifo vitokanavyo na maradhi mbalimbali kama malaria, kuhara na maambukizi katika mfumo wa njia ya hewa kwa watoto wachanga na wadogo.

Hivyo iwapo watoto wachanga na wadogo watapatiwa lishe bora ni wazi ukuaji wa ubongo wao utaboreka na ikumbukwe kuwa ubongo wa mtoto hukua kwa haraka hasa wakati wa ujauzito na katika miaka miwili ya mwanzo ya uhai wake.