November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Unyanyapaa unavyoathiri matumizi ya huduma za uzazi wa mpango kwa vijana


Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma


MGANGA Mkuu wa Jiji la Dodoma Dkt.Andrew Method amesema wanatarajia kuanza ujenzi wa jengo la ghorofa nne katika hospitali ya Makole jijini Dodoma ambalo litawezesha upatikanaji wa huduma nyingi zikiwemo za afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa vijana.
Akizungumza na Mtandao huu Dkt.Method amesema,kwa sasa vyumba ni vichache katika hospitali hiyo hali inayosababisha vijana kuchangamana na watu wazima wakati wa kupata huduma hizo hali inayoondoa uhuru wa vijana kupata huduma hizo.
Amesema,hivi sasa wapo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi ambapo amesema,ujenzi huo utakamilika kwa muda wa miezi tisa mara baada ya kazi kuanza.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha uzazi wa Mpango Loy Mazengo amesema ili kuwafanya vijana wanakuwa na uhuru pindi wanapoenda hospitalini hapo kwa ajili ya kupata huduma za uzazi wa mpango,kwa sasa wametenga siku moja kwa mwezi ambayo huwaweka vijana pamoja na kuwapa elimu ya matumizi  sahihi ya njia za uzazi wa mpango.
Amesema hiyo ni kutokana na unyanyapaa uliopo miongoni mwa wateja wanaofika kupata huduma hiyo kuwaona vijana wanaotumia huduma za uzazi wa mpango kama wanakosea kupata huduma hizo.
“Kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu wazima kuwanyanyapaa vijana lakini tumetenga siku moja katika mwezi ambayo tumekuwa tukizungumza na vijana peke yao kuhusu umuhimu wa wao kutumia huduma hizo kwa wale ambao wameshaanza mahusiano.”amesema Mazengo
Baadhi ya vijana wanaotumia huduma hizo wameiomba seriali kutengeza mazingira mazuri ya wao kupata huduma hizo na siyo kuchangamana na watu wazima hali ambayo wamesema inawatia hofu.
“Kimsingi hivi sasa utandawazi unasababisha vijana wanaingia katika mahusiano mapema,kuna wengine wana akili darasani lakini anaingia kwenye mahusiano ,anapata mimba na anaatisha masomo,ni heri kutumia njia za kujikinga ambazo zitamwezesha kufikia malengo yake ya kuhitimu masomo yake.”amesema Amina Abdallah
Naye Andrew Makingo mkazi wa Mji Mpya jijini Dodoma amesema mbali ya kujikinga na mimba zisizotarajiwa pia ,matumizi sahihi ya huduma za uzazi wa mpango pia inaweza kuwakinga dhidi ya maambukizi ya virus vya UKIMWI na magonjwa mbalimbali ya ngono inategemeana na njia anayotumia muhusika..