November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Korosho changa

Unyama wa kutisha, wanafunzi wadaiwa kulazimishwa kutafuna korosho changa

Na Said Hauni, TimesMajira Online, Lindi

WANAFUNZI wawili katika Shule ya Msingi Chilala, Kata ya Rutamba, Wilaya na Mkoa wa Lindi, wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya kikatili, ikiwemo kuchapwa viboko saba kila mmoja na kulazimishwa kutafuna korosho mbichi bila ya kuondolewa maganda ya nje, hali iliyowasababisha kupata homa na kuvimba midomoni yao.

Habari zilizothibitishwa na wanafunzi wenyewe, wazazi na Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Lindi, Danciani Mtauka, juzi zinaeleza kuwa wanafunzi hao walifanyiwa ukatili huo na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Frank Kisinga, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Wanafunzi hao wa darasa la pili na la tatu mmoja akiwa na umri wa miaka 10 na mwingine miaka 13, walidai kupewa adhabu ya kuchapwa viboko na kutafunishwa korosho changa baada ya mwalimu huyo kuwatuma kwenda shambani kuokota korosho na kuziwasilisha shuleni hapo.

Wakizungumza na timesmajira,online mkoani hapa mbele ya wazazi wao na Mwalimu Mkuu wao, Frank Kisinga, watoto hao walidai siku hiyo majira ya saa 9;0 alasiri wakiwa wanaendelea na masomo yao, wao na wanafunzi wenzao walitumwa kwenda shamba la shule ili kila mmoja akaokote na kupeleka idadi ya korosho kumi kila mmoja.

Wamedai wakiwa wanatekeleza agizo hilo, baadhi ya wanafunzi wenzao waliacha kuokota korosho zilizoanguka chini na kuanza kuangua korosho changa za kwenye mti.

Wamedai baada ya hapo viranja wa shule hao walioongozana nao shambani waliwashtaki kwa mwalimu mkuu kwamba wao wameangusha korosho mbichi.

Pia, wamedai mara baada ya kufikishwa mbele ya mwalimu huyo, walichapwa viboko saba kila mmoja, kisha kulazimishwa kutafuna korosho mbichi.

“Ni roho mbaya za viranja wetu,sisi hatukuwa tumeangusha korosho changa,lakini kule kwa mwalimu tukashtakiwa sisi,” alidai mmoja wa wanafunzi hao.

Wamesema wakati wanapelekwa kwa huyo Mwalimu, mikononi mwao kila mmoja alikuwa na idadi ya korosho kumi kama walivyotakiwa kufanya na baada ya kuchapwa viboko saba kila mmoja, alilazimishwa kutafuta korosho mbichi walizookota.

Wazazi wa wanafunzi hao wamesema kitendo kilichofanywa na mwalimu huyo sio cha kiungwana, kwani ni ukatili dhidi ya watoto wao. Wazazi hao waliuomba uongozi husika kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa walimu wenye tabia ya aina hiyo.

“Kama sio uuaji ni kitu gani,watoto walishachapwa viboko tena saba, kulikuwa na sababu gani kuwalazimisha watafune korosho mbichi? Huo ni unyama na ukatili wa kutisha,” amesema mmoja wa wazazi hao.

Kufuatia kitendo hicho wazazi wa watoto hao walikwenda Kituo cha Polisi Kata ya Rutamba kutoa taarifa ambapo walipewa PF3 kisha kuwapeleka watoto wao Kituo cha Afya Katani kupata matibabu.

Baada ya kufika kwenye kituo hicho cha afya walishauriwa peleka Hosptali ya Mkoa, Sokoine kwa ajili kufanyiwa uchunguzi wa afya.

“Tunashukuru kipimo cha Utra-sound kimeonesha vijana wetu wapo salama, hakuna madhara ndani ya miili yao,” amesema mmoja wa wazazi wa watoto,

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Kisinga alipoulizwa kuhusu madai ya wanafunzi hao, alikiri kuwatuma wanafunzi hao na wengine kwenda shamba la shule kuokota korosho na kwamba kutokana na makosa waliyoyafanya aliwachapa viboko vitatu kila mmoja na sio saba kama inavyodaiwa.

“Ni kweli saa 9;0 alasiri niliwaambia wanafunzi wa darasa la pili hadi ka sita kwenda shamba letu la shule kuokota korosho,’’ amesema Kisinga.

Amesema baada ya kufika shambani ndipo wanafunzi hao wawili waliamua kuporomosha madunge (korosho changa) ambapo viranja waliwapeleka mbele yake na aliwapa adhabu ya viboko vitatu kila mmoja na sio saba kama inavyodaiwa, kwani anatambua utomvu wa korosho una madhara kwa mwanadamu.

TimesMajira, Online ilipowasiliana na Ofisa Elimu Shule za Msingi Wilaya ya Lindi, Dancani Mtauka,kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo, amekiri kupata taarifa hiyo na kueleza tayari amewaagiza wasaidizi wake kulifuatilia ili kufahamu ukweli,kabla maamuzi mengine kufanyika.

Msaidizi wa Kisheria (SHIMKIM),Tarafa ya Mingoyo, Manispaa ya Lindi, Hadija Mnunduma, akizungumzia tukio hilo, alionekana kusikitishwa na kitendo hicho na ameomba uongozi wa Idara husika kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya walimu walio na tabia hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Lindi,Stanley Kulyamo, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi ili kupata kauli yake kama Ofisi yake inayo taarifa ya kitendo cha kikatili kinachodaiwa kufanywa na kiongozi wa shule hiyo, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.