Fresha Kinasa,TimesMajira Online,Mara
SHIRIKA la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania limesema litaendelea kushirikiana na Serikali kwa ukaribu katika uhamasishaji jamii juu ya uhifadhi wa Bonde la Mto Mara kwa manufaa endelevu.
Pia, limeahidi kuvitangaza vivutio vilivyopo mkoani humo, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ili iweze kutambulika kimataifa kwamba inapatikana katika mkoa huo kwa lengo la kuchochea maendeleo ya wananchi na mkoa huo kwa ujumla.
Sawiche Wamunza, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Ushirikiano, UNDP Tanzania, ameyasema hayo Septemba 15, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mara (“Mara Day”) kilichofanyika Uwanja wa Mwenge, Wilaya ya Butiama.
Amesema, kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi wa Bonde la Mto Mara, shirika hilo limekuwa likishiriki katika maadhimisho hayo kila mwaka, na mwaka huu limefanikiwa kupanda miti 11,000 kando kando ya Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania, ambalo linaanzia Milima ya Mau nchini Kenya na kuishia Ziwa Victoria nchini Tanzania.
Wamunza amesema shirika hilo limeendelea kuhamasisha ushirikiano wa kikanda ili kuona namna ya kuendelea kuhifadhi Bonde la Mto Mara, ambalo pia ni chachu ya uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Huku akisema kampeni ya upandaji miti kando ya Bonde la Mto Mara itaendelea kufanyika kwa uendelevu.
“Tutaendelea kuutangaza Mkoa wa Mara, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, watu wajue iko Mkoani Mara kupitia utalii kuwezesha maendeleo ya mkoa,” amesema Wamunza.
Aidha, amesema shirika hilo limeendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo kupitia sekta mbalimbali hapa nchini, ikiwemo kilimo.”Huko nyuma tulikuwa na mradi wa kuhamasisha vijana walime kilimo cha mboga mboga ili wauze kwenye hoteli za kitalii kujipatia kipato,” amesema Wamunza.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutoka nchini Tanzania Mhandisi Mwajuma Waziri amesema dhamira ya Serikali ya Tanzania kuhifadhi bonde la mto Mara ni kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa maji ya kutosha kwa ajili ya maendeleo.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewataka Wananchi wa Mkoa wa Mara kutunza mazingira, kulinda vyanzo vya maji na ikolojoa kwa manufaa ya vizazi vya Sasa na vijavyo Huku akisema tukio la Mara day ni ishara ya udugu, umoja na mshikamano baina ya watanzania na Wakenya.
Pia Kanali Mtambi, amesisitiza Wananchi kutojihusisha na shughuli zinazoathiri bonde la mto Mara kwani bonde hilo bado ni tegemeo kubwa.
Uamuzi wa Mkutano wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Bonde la Ziwa Victoria, uliofanyika Mei 4, 2012 Kigali, nchini Rwanda, ulielekeza kufanyika kwa maadhimisho ya Mara Day kwa kupokezana kati ya Kenya na Tanzania.
Maadhimisho ya Mara Day kwa mwaka huu 2025 ni ya 14, na yalikuwa na kaulimbiu isemayo”Hifadhi Mto Mara, Linda Uhai”Ambapo huadhimishwa kila mwaka Septemba 15 kwa kupokezana baina ya nchi ya Kenya na Tanzania tangu yalipoanza.
Tarehe ya maadhimisho ya Mara Day inahusiana na tukio la wanyama (nyumbu) kuhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania kwenda Maasai Mara, Kenya kwa ajili ya kutafuta malisho na kuzaliana, kisha kurejea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi