November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UNDP, TADB watekeleza miradi 12 ya kuinua kilimo nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira,Online Arusha

SHIRIKA la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) wanashirikiana kutekeleza miradi 12 inayopeleke fedha kuinua sekta ya kilimo nchini kwa kutumia njia za ubunifu badala ya kutumia utaratibu wa vigezo vya urari na ukwasi katika kufikira maombi ya mikopo na uwezeshwaji wa wakulima.

Jitihada hiyo ya pamoja kati ya taasisi hizo mbili imeelezwa jijini hapa jana na Afisa Miradi wa UNDP, Amon Manyama, wakati wa kikako cha pamoja baina ya wawekezaji wa kutoka Ulaya, viongozi wa Serikali na taasisi za kimkakati za kuinua sekta ya kilimo.

Mkutano huo ulioitwa Wawekezaji wa Ulaya katika Kilimo cha Tanzania (European Investors in Agricultural Dialogue), uliandaliwa na European Business Group nchini na umehudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda na Balozi wa Uholanzi, Jeroen Verheul.

Manyama hakueleza thamani ya miradi yote na mahali inakotekelezwa, lakini alisema utekelezaji wa miradi hiyo unaongozwa makubaliano ya awali (MoU) baina ya taasisi hizo mbili.

Akiunga mkono maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, aliyoyatoa kabla yake, Manyama amesema upelekaji fedha ya kuinua sekta ya kilimo katika nchi zinazoendelea kama Tanzania unadai ubunifu na umakini katika kupima maelezo na maombi ya mkopaji badala ya kutumia utaratibu unaotumiwa na mabenki ya biashara wa kupitia vigezo vya urari na ukwasi wa mwombaji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Ishmael Kasekwa akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda (kushoto). Muda mfupi baada ya kukabidhi matrekta 15 yenye thamani ya sh. milioni 950 kwa Chama cha Msingi cha Nguvu Moja Wilayani Mbarali, Mbeya hivi karibuni. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbarali CCM (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Amezitaka benki na Serikali kutumia ubunifu katika kufiria mahitaji ya fedha ya sekta ya kilimo.

“Ili kilimo kifanikiwe, unahitajika mtazamo mpya na tofauti na ule uliozoeleka katika kupeleka fedha katika sekta hii.

Wakati taasisi za fedha zatazamiwa kufikiria namna tofauti ya kuhudumia kilimo, Serikali pia lazima ichunguze fursa mpya za kupata fedha ya kupeleka katika kilimo.

Kilimo, kama alivyoeleza Prof Mkenda, kinaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania. Maana yake ni kwamba uwezo wa kilimo ikitumiwa kikamilifu malengo ya Ajenda 2030 yatafanikiwa bila wasiwasi.

Nashauri Serikali iangalie fursa mpya za kupata fedha na bidhaa za kifedha kwa ajili ya kilimo zikiwemo Blue Bond na Green Bond,” alisisitiza.

Mapema Justine aliueleza mkutano huo kwamba uelekezaji wa fedha katika sekta ya kilimo unahitaji majadiliano katika kufikiria maombi ya mikopo badala ya kutumia utaratibu wa kupitia vigezo vya urari na ukwasi wa mwombaji wa mkopo.

“Ni kweli ili mchakato uwe na maana, lazima mradi unaoombewa mkopo uwe mzuri na stahiki. Lakini ni muhimu pia kuwa na majadiliano yenye sura ya ubunifu, kusikiliza na kupima kwa makini maelezo ya mwombaji mkopo,” ameueleza mkutano huo.

Akieleza uzoefu wa TADB katika kuokoa ulimaji wa zao la kahawa na kuvinusuru na kufilisika vyama vya ushirika Mkoani Kagera, Justine alisema kwamba benki za biashara ziliuona mnyroro mzima wa thamani wa zao hilo haukopesheki, lakini TADB kwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya mnyororo wa thamani, kutumia njia ya majadiliano na kufanya madiliko kidogo katika masharti na namna ya kutoa fedha, iliviokoa vyama vya ushirika vikuu na vya msingi ambavyo ilikuwa vifilisike kutokana na madeni makubwa.

“Kama mradi huu ungelitazama kwa vigezo vya urari na ukwasi ni dhahiri usingelikopesheka,” aliwambia wawekazaji hao kutoka Ulaya.