Judith Ferdinand, Mwanza
IMEELEZWA kuwa kampeni ya kunawa kwa maji tiririka na sabuni ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya vya UVIKO 19, imesaidia kupunguza magonjwa mbalimbali ya mlipuko yakiwemo ya kuhara hasa katika maeneo ya visiwani kikiwemo kisiwa cha ukerewe mkoani Mwanza.
Akizungumza na mtandao huu,mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Kangunguli wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, ambacho ni miongoni mwa maeneo ya visiwani ambayo yalikuwa yakikumbwa na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara,Sungulwa Mgema amesema, miaka ya nyuma magonjwa ya mlipuko yalikuwa mengi ila kwa sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu watu wameelimika na wanazingatia kanuni za usafi katika maeneo yao.
Alisema, kwa sasa yeye na familia yake hawaendi hospitali mara kwa mara kutibiwa magonjwa ya kuhara kutokana na unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara kwa lengo la kujikinga na maambukizi ya UVIKO 19 lakini kumbe unakinga na magonjwa mengine kama kuhara.
“Mimi na familia yangu kwa Sasa hatuendi hospitali mara kwa Mara kutibiwa magonjwa ya kuhara kwa sababu tunazingatia unawaji mikono na usafi tukiwa nyumbani,” amesema Mgema
Pia mmoja wa wananchi wa mtaa wa Bugogwa wilayani Ilemela mkoani hapa, Constantine Luhari,amekiri kuwa kampeni hiyo ya unawaji mikono kwa ajili ya kujikinga na UVIKO 19 imesaidia kuwaepusha na magonjwa mengine ya mlipuko.
Amesema,magonjwa ya mlipuko husababishwa na vimelea vya kinyesi cha binadamu na wanyama,chakula kichafu pamoja na kutozingatia kanuni za usafi ikiwemo kula bila kunawa mikono.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi katika kituo cha Afya Kangunguli wilayani Ukerewe, Dkt.Paschal Peter,amesema miaka ya nyuma katika kituo hicho walikuwa wanapokea wagonjwa kati ya 30 hadi 40 kwa mwezi wa magonjwa ya mlipuko hasa kuhara lakini sasa idadi ya wagonjwa imepungua na kufikia wagonjwa 10 tu kwa mwezi.
Dkt.Peter amesema msisitizo wa wataalam wa afya wa kuhimiza wananchi kunawa mikono umechangia kupungua kwa idadi ya watu wanaotibiwa magonjwa hayo.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe, Dkt. Getera Nyangi amesema katika kipindi cha miezi 12 iliyopita magonjwa ya kuhara, kuharisha damu na homa ya matumbo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Amesema,tabia ya watu kunawa mikono kwa maji tiririka yaliyotokana na kampeni ya unawaji mikono ili kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 imesaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na magonjwa hayo.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, magonjwa hayo yamepungua ambapo katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2021 wagonjwa waliotibiwa magonjwa hayo walikuwa 6,652 kutoka 12,406 waliotibiwa mwaka 2020.
Ofisa Afya wa Mkoa wa Mwanza, Fungo Masalu amesema licha ya kwamba hawajafanya utafiti wa kina kuona hali ilivyo kuhusu magonjwa ya mlipuko kwenye jamii lakini takwimu zao zinaonesha yamepungua.
hata hivyo amesema ,zipo sababu nyingi zilizosababisha kupungua kwa magonjwa hayo ikiwemo watu kupunguza kwenda hospitali kutibiwa kutokana na imani potofu juu ya Uviko-19 au ni kweli kwamba kampeni ya unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni wa mara kwa mara umesaidia magonjwa hayo kupungua.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi