January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UN yalaani walioshambulia wafanyakazi wake

GENEVA, Umoja wa Mataifa umelaani kitendo cha makundi ya vijana kushambulia wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale yasiyo ya kiserikali kwenye mji wa Torit jimboni Equitoria Mashariki.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu (OCHA), Jens Laerke amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.

“Umoja wa Mataifa unalaani mashambulizi haya yaliyofanywa na vikundi vya vijana. Mashambulizi haya yametokea wakati kuna kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira nchini Sudan Kusini na matakwa ya vijana hao kuajiriwa na mashirika ya kibinadamu,”amesema Laerke.

Baadhi ya mashirika, kwa mujibu wa msemaji huyo wa OCHA, yamelazimika kuhamisha wafanyakazi wao na kuwapeleka maeneo salama na hata maeneo ya kusafiri yamepunguzwa kutokana na ukosefu wa usalama.

“Operesheni za mashirika hayo zimesitishwa au zimepunguzwa ikiwemo huduma muhimu za afya na lishe. Uhamishaji wa wagonjwa mahututi kwenda hospitali ya taifa ya Torit, nao umevurugwa kutokana na kupunguzwa kwa shughuli za tiba mashinani huku baadhi ya vituo 40 ya lishe mjini Torit haviwezi kufikiwa na wananchi,”amesema Laerke.