November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ummy:Kutibu saratani ya mlango wa kizazi ni gharama,pelekeni wasichana wakachanjwe HPV

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Serikali imeeleza kuwa kwa mujibu wa hesabu walizopiga kumuhudumia mgonjwa mmoja wa saratani ya mlango wa kizazi inaweza kugharimu mpaka milioni 8 kwa mwaka huku ikilenga kuwachanja wasichana zaidi ya milioni 4 chanjo dhidi ya kuwakinga na ugonjwa huo(HPV) mpaka ifikapo Desemba mwaka huu wenye umri wa miaka 9-14.

Kwa mujibu wa takwimu za nchi saratani hiyo inaongoza kuwatesa Watanzania ambapo kati ya wagonjwa 100 nchini wanaougua saratani 23 wana saratani ya mlango wa kizazi ikufuatiwa na saratani ya mfumo wa chakula asilimia 11, saratani ya matiti asilimia 10.4 pia ongezeka la saratani ya tezi dume ambayo imefikia asilimia 8.9.

Ambapo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Dunia(WHO), zinaonesha kwamba Tanzania ni nchi ya nne duniani kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa kizazi huku ya tatu ni Zambia,ya pili ni Malawi na ya kwanza Eswatini(Swaziland).

Hayo yamezungumzwa Aprili 22,2024 na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya chanjo kitaifa yalioenda sambamba na uzinduzi wa chanjo ya kuwakinga wasichana wenye umri wa miaka 9-14 na saratani ya mlango wa kikazi(HPV), dozi moja ambapo awali ilikuwa ikitolewa dozi mbili yenye kauli mbiu “Jamii iliopata chanjo,jamii yenye afya” uliofanyika uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela mkoani Mwanza ambapo ameeleza kuwa chanjo hiyo inatolewa bure ambayo gharama yake ni sawa na 10000.

“Tupime kutumia 10,000 na kuja kutumia z milioni 8 kwa ajili ya kutibu mgonjwa mmoja wa saratani ndio maana tunasema kinga ni bora kuliko tiba,umasikini utaikumba familia yenye mgonjwa wa saratani,watoto wataathirika na serikali itaathirika pia, nitoe wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wenu wa kike kupata chanjo hiyo ambayo ni salama na haihusiani na masuala ya uzazi wa mpango,” ameeleza Ummy.

Ummy ameeleza kuwa saratani ni gharama kwenda kumuona Daktari Bugando inaweza kuwa 5000-10000 ukienda mara tatu mpaka tano inaweza kufika mpaka 100,000, lakini utatakiwa kufanya vipimo ambapo cha damu 17,000,utolewe kinyama 80,000, X-ray 20,000, Ultrasound 20,000, waamue wakufanyie CT-Scan 150,000.

“Daktari akisema nataka kujiridhisha zaidi tumfanyie MRI 250,000, vipimo tu vya maabara kwa ajili ya saratani vinaweza kuchukua kiasi cha 500,000, vipimo vya daiolojia kama 600,000 umeisha kutwa na saratani unaambiwa sasa uanze tiba kemia kwa wiki nimepata malalamiko Bugando wananchi wananiambia Waziri 300,000,400,000,600,000 na 700,000, kwa wiki hatuwezi,”ameeleza Ummy na kuongeza kuwa

“Tusifike huko tuwachanje mabinti zetu ili wasije kuugua saratani ya mlango wa kizazi laki 7 kwa wiki fanya mizunguko sita inaweza fika mpaka milioni 4,jamani ni familia ngapi zinamudu kutumia kiasi hicho cha fedha kumuuguza mgonjwa wa saratani hiyo,”.

Pia ameeleza kuwa sayansi iliothibitishwa pasipo na shaka wanaweza kuzuia na kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi endapo watawapa mabinti ambao hawajaanza masuala ya ngono chanjo ya kuwakinga na saratani hiyo.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa malengo Shirika la Afya Dunia(WHO) katika kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi ,inawataka inapofika mwaka 2030 asilimia 90 ya binti yoyote wa kitanzania atakaye fikia umri wa miaka 14 awe amepata chanjo ya HPV.

Huku lengo jingine ni kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa mapema dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi na kufikia asilimia 70 mwaka 2030 pamoja na kuwafikia asilimia 90 ya kuwatibu wagonjwa wote wa saratani hiyo.

“Nitoe wito kwa wanawake hususani wenye umri wa miaka 25 mpaka miaka 49, angalau mara moja kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na Rais ametuwezesha tumepeleka vifaa vya kupima na kutibu mabadiliko ya awali ya saratani hiyo mpaka ngazi ya zahanati,ukigundulika mapema ni rahisi kupona na kutumia gharama ndogo badala ya kusubili saratani imefika hatua ya tatu na ya nne ni ngumu kutibu,”.

Sambamba na hayo ameewachia changamoto wataalamu wa afya juu ya kuwachanja chanjo hiyo wasichana wenye umri wa miaka 15 mpaka 19 wale ambao watathibitika kuwa hawajaanza masuala ya ngono ili kuwakinga.

Naye Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania Elke Wisch,ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza kutokana na janga la UVIKO-19 ambalo liliathiri mpango wa chanjo,serikali kwa msaada kutoka kwa washirika imekuwa ikifanya kazi kwa bidii kurejesha chanjo na kuongeza chanjo maalumu.

“Wakati saratani ya mlango wa kizazi ikiendelea kuwa chanzo kikubwa cha vifo vinavyotokana na saratani ambayo huchangia asilimia 38 ya vifo hivyo nchini Tanzania,tunatambua hatua iliofikiwa na serikali katika kuboresha upatikanaji wa chanjo ya HPV nchi nzima ili kuwakinga wasichana dhidi ya magonjwa hayo,”ameeleza Elke.

Elke ameeleza kuwa hadi sasa chanjo ya HPV dozi ya kwanza imefikia asilimia 79 huku ya pili ni asilimia 60 huku akisisitiza kuwa juhudi za pamoja zinahitaji ili kuhakikisha kila msichana nchini hapa anapata Ulinzi muhimu dhidi ya saratani ya mlangi wa kizazi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, ameeleza kuwa kwa Mkoa wa Mwanza una jumla ya vituo 400 vinavyotoa chanjo katika Halmashauri zote nane.

Ameeleza kuwa kwa mwaka 2023 idadi ya watu waliofanyiwa huduma ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi kimkoa ni zaidi ya 40,000 kati yao waliogundulika zaidi ya wanawake 1,510 walikuwa na dalili za awali zilizosababisha wanawake 919 kufanyiwa tiba katika hospitali ya Rufaa ya Bugando huku wanawake 90 sawa na asilimia 18 walithibitika kuwa na saratani hiyo.

Mtaalamu Bigwa wa Afya ya Jamii Idara ya Saratani Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando
Kidaya Bashari,ameeleza kuwa hospitali hiyo ya Bugando kwa mwaka wanapokea wagonjwa wapya zaidi ya 46,000 wa saratani ambapo hali ikiendelea hivi wagonjwa wataongezeka kufikia mwaka 2030,

Kwa sasa wanahudumia wagonjwa takribani 130 kwa siku upande wa kliniki na 80 kwa upande wa mionzi tiba hali imezidi kuongezeka hadi mtu anapewa tarehe kwamba anakuja lakini hawezi kuanza mionzi leo kwani wagonjwa wamekuwa ni wengi kuliko idadi ya vitendea kazi.

“Tunamshukuru Rais Samia kupitia Wizara ya Afya tumeletewa mashine nyingine mpya ya matibabu ya mionzi ambayo tunategemea itafika Juni mwaka huu na itasaidia kupunguza changamoto ya wagonjwa kusubili muda mrefu kwa ajili ya kupata matibabu ya saratani.

Hata hivyo ameeleza kuwa kwa taarifa zilizopo sasa hivi zaidi asilimia 70-80 wagonjwa wao wamekuwa wakichelewa matibabu na wanafika wakiwa katika hatua ya tatu na ya nne,kiafya hatua hizo ni ngumu kutibika na kupona kabisa.