Na Zena Mohamed ,Timesmajiraonline,Dodoma
UMOJA wa Vyombo vya Habari vya Mitandao ya Kijamii Mkoa wa Dodoma (UMIKIDO) umeshiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji nchini.
Mkutano huo wa siku mbili unafanyika katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, ukianza leo Februari 12, 2026. Mkutano huo umeandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika mkutano huo, mada na mafunzo mbalimbali yanawasilishwa kwa waandishi wa habari pamoja na wadau wa sekta ya utangazaji.
Aidha, kunafanyika mijadala mbalimbali inayolenga kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo na uboreshaji wa vyombo vya utangazaji nchini.
Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA,ambapo pamoja na mambo mengine ametangaza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa ada za usajili kwa watoa maudhui mtandaoni, akisema hatua hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi, kuongeza ushindani na kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Utangazaji (Annual Broadcasters’ Conference – ABC) 2026 uliofanyika leo, Mwinjuma amesema ada ya leseni ya utoaji maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000, huku ada ya watoa maudhui ikishuka kutoka shilingi milioni moja hadi laki moja kwa mwaka.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya habari, akisisitiza kuwa lengo ni kuwezesha na siyo kudhibiti.

“Kwa gharama hizi nafuu, tunaamini watoa maudhui wengi wataingia kwenye mfumo rasmi na hivyo kuongeza ufanisi, ushindani na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi,” amesema Mwinjuma.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ameagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unazingatia mikataba na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari.
Amesema amepokea taarifa kuwa baadhi ya vyombo havijalipa wafanyakazi mishahara kwa zaidi ya miezi sita, na kuagiza mamlaka husika kufuatilia suala hilo na kuwasilisha mrejesho ndani ya wiki moja.
“Nina taarifa kwamba kuna vyombo havijalipa wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezi sita. Hili siyo suala la siasa, nataka mrejesho ndani ya wiki moja,” amesisitiza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, amesema mwaka 2025 jumla ya wanahabari 2,054 wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo, huku usikivu wa redio ukifikia asilimia 85 na usambazaji wa televisheni kupitia satelaiti kufikia asilimia 100.
Aidha, hadi Desemba 2025, jumla ya leseni 770 za utangazaji zilikuwa zimetolewa, huku TCRA ikiwa na mpango wa kuanzisha mfumo wa redio kidijitali ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la mawasiliano


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama