Judith Ferdinand
KATIKA Kata ya Kayenze, wilayani Ilemela Mkoa a wa Mwanza kuna kisiwa kinachoitwa Bezi.
Bezi ni kisiwa lakini pia ni moja ya mitaa ndani ya Kata ya Kayenze. Kutoka katikati ya Jiji la Mwanza inaweza kumchukua mtu hadi saa 3 ili kufika katika kisiwa hiki ambacho ni maarufu kwa shughuli za uvuvi.
Ili kuweza kufika kisiwani Bezi ambapo tunaangazia suala zima la umbali la watoto wanaioshi kisiwani humo kufuata elimu ngambo makao makuu ya Kata ya Kayenze.Hata hivyo elimu ni haki ya kila mtoto ili kuondokana na adui ujinga, umaskini na maradhi,ambayo inamwezesha mtoto kutambua haki zake na kufikia malengo yake.
Lakini upatikanaji wa elimu kwa watoto wa kike imekuwa kikwazo nchini Tanzania kutokana na baadhi yao kukatishwa masomo na kulazimishwa kuingia kwenye ndoa wakiwa na umri mdogo.
Hali hii huchochewa na mimba za utotoni, ambayo inapelekea binti kuangukia katika ndoa za utotoni aidha kwa familia za pande mbili kukaa na kumalizana kimya kimya.
Ambapo husababishwa na mazingira ya maeneo wanayoishi kuwa na muingiliano wa watu mbalimbali,umbali wa kuifuata elimu na wakiwa njiani ukutana na vishawishi,mila na desturi pamoja na taama za wazazi za kupata mahali.
Taarifa mbalimbali zinabainisha kuwa ndoa za utotoni ni changamoto kubwa kwa mabinti wa kitanzania,taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ya Julai,2022 inaeleza kuwa takribani wanawake watatu kati ya 10 nchini Tanzania wanaolewa wakiwa watoto, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya 11 duniani kwa kuwa na ndoa za utotoni.
Kama ilivyo maeneo mengine nchini Tanzania, Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa nchini inayokabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni ambazo zinachochewa na sababu mbalimbali zikiwamo umbali wa kufuata elimu na mazingira ya kuwa kandokando ya Ziwa Victoria,mila na desturi.
Kisiwa cha Bezi ni moja ya mitaa inayounda Kata ya Kayenze kinachopatikana ndani ya Ziwa Victoria, ambako wananchi wake wanajishughulisha na uvuvi kwa kiasi kikubwa.
Pia ni eneo moja kati ya maeneo yaliopo wilayani Ilemela ambalo mazingira yake yanaweza kusababisha watoto wa kike kukatisha masomo na kuangukia katika ndoa za utotoni.
Kutokana na sababu mbalimbali moja wapo ikiwa ni ukosefu wa shule ya sekondari katika kisiwa hicho na ukosefu wa Bweni katika shule ya sekondari Kayenze.Hali inawalazimu wanafunzi wakiwamo wa kike kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu.
Umbali huo unajumuisha wao kuvuka maji kwenda nchi kavu, makao makuu ya Kata ya Kayenze kufuata elimu ya sekondari.
Wawapo njiani hukutana na vishawishi vingi kutoka kwa wafanyabiashara na wavuvi, ambao hukutana nao katika usafiri wa kivuko(,feri) ama wanapokuwa njiani, hivyo kurubuniwa na kujikuta wameingia katika uhusiano wa kimapenzi.
Licha ya serikali kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza umbali wa kutembea kwa wanafunzi kwa kuhakikisha kila Kata inakuwa na shule ya msingi na sekondari hali hiyo imekuwa tofauti kwa wanafunzi wanaotoka kisiwa cha Bezi.
Ambapo licha ya Kata yake kuwa na sekondari lakini kutokana na jiografia ya eneo la mtaa huo kuwa la Kisiwa imechangia wanafunzi kutumia umbali mrefu na masaa mengi katika kufuata elimu na kurejea nyumbani kwa sababu wanatumia usafiri wa majini.
Kutoka kisiwani Bezi hadi makao makuu ya Kata unatumia kivuko cha Mv.Ilemela ambapo itakuchukua takribani saa 1 na dakika 15 hadi 20 na baada ya hapo hadi kufika shule ya sekondari Kayenze itakuchukua takribani dakika 20 kwa kutembea kwa miguu,hivyo kwa wanafunzi wanaotoka kisiwa cha Bezi kwa siku wanatumia wastani wa wa masaa matatu(Dakika 180) njiani sawa na saa 1 na dakika 40 wakati wa kwenda shule na saa moja na dakika 40 wakati akirejea nyumbani.
Adha wanayopata wanafunzi wa kike kutoka Kisiwa cha Bezi wanapokuwa njiani kwenda shule.
Shule ya sekondari Kayenze imepakana na Kituo cha Afya Kayenze ambapo ni takribani dakika 20 kutoka makao makuu ya Kata ya Kayenze yenye mandhari nzuri ya kuvutia ili changiwa na na uwepo wa miti.Mapokezi yanafanyika na Mkuu wa Shule hiyo ambaye baada ya kueleza dhamira ya kutembelea shule hiyo anamuita mmoja wa wanafunzi kutoka Kisiwa cha Bezi.
Mmoja wa wanafunzi wa kike Anes Chacha siyo jina lake halisila anayesoma shule ya sekondari Kayenze akitokea kisiwa cha Bezi anaeleza kuwa wakitoka Kisiwa cha Bezi kwenda shuleni Kayenze wanatumia usafiri wa kivuko(Feri) kwani hamna njia mbadala zaidi ya huo wa kuvuka maji.
Anaeleza kuwa wanapokuwa katika usafiri huo wanakutana na watu mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa kiume ambao wamekuwa wakiwashawishi kwa kuwapa ela ili waweze kuingia nao katika mapenzi.
Pia anaeleza kuwa changamoto wanazokutana nazo wanapokuwa katika usafiri wa feri wakati wa kwenda shule na kurejea nyumbani kunaweza kusababisha kuingia katika ndoa za utotoni kwani mbali na kuchoka pia vishawishi kutoka kwa wanaume vinaweza kusababisha.
“Si rahisi kwa binti mdogo kuweza kukwepa vishawishi hivyo kwa muda mrefu na ukizingatia asilimia kubwa ya maisha yetu ni duni mfano rafiki zangu ambao tulikuwa tunakaa nao mtaa mmoja na kusoma shule moja kwa sasa wamehamishwa shule walishindwa kuepuka vishawishi kwani walijiingiza kwenye mapenzi kwa sababu ya tamaa ya fedha za kula wawapo shuleni,waliniambia kila siku usumbufu wanaoupata wa kupanda feri na kufika shule wakiwa wamechoka ni bora waolewe,”anaeleza Anes.
Kwa mujibu wa takiwmu za mashirika mbalimbali likiwemo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF)na la Elimu, sayansi na Utamadubni (UNESCO),umbali wa kufika shuleni ni moja ya changamoto zinazochangia kukwamisha malengo ya wasichana wengi ya elimu hususani katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo utoro , mimba za utotoni, ndoa za utotoni hata mafanikio duni katika masomo na hatimaye maishani kwa wasichana.
Ombi kwa serikali ili kuwakomboa wanafunzi wa kike Anes anaeleza kuwa,ili kuondokana na changamoto hiyo kulingana na mazingira ya kisiwa na Kata nzima ya Kayenze serikali iwajengee mabweni katika shule ya sekondari Kayenze na shule nyingine zote.
“Mbali na hatari ya kuingia katika ndoa za utotoni,pia tunachoka sana kwa sababu ya kutumia usafiri wa majini, tunakosa baadhi ya vipindi vya asubuhi na vingine vya jioni kwani inatulazimu kuacha kusoma masomo ya jioni ili kuwai usafiri wa kivuko ambao kwa sisi wanafunzi serikali iliamuru tusilipe nauli pia hatuna njia mbadala ya kutumia ili tuweze kufika nyumbani,”anaeleza Anes na kuongeza kuwa
“Pia tukifika nyumbani tumekuwa tumechoka na kukosa muda mzuri wa kujisomea kwani kwa sisi watoto wa kike inatulazimu kusaidia kazi za nyumbani, suluhisho ni tujengewe bweni ili tupate muda mwingi wa kujisomea na mwaka huu tumeingia kidato cha pili ambapo kuna mtihani wa taifa,”.
Pia anaeleza kuwa kila siku viongozi na wazazi wawe wanawafuatilia wanafunzi wote juu ya mahudhurio yao shuleni hususani wanaotoka kisiwa cha Bezi,maana wanafunzi wanaotoka Bezi wanajua kuwa wao wako mafichoni hakuna mtu atakaye wafuatailia.
Baada ya serikali kujenga kivuko hicho kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa maeneo ya Bezi usafiri iliagiza kuwa wanafunzi wote hawapaswi kulipa nauli ila changamoto ni kuwa kivuko hicho kinafanya safari mara nne tu kwa siku mbili kwenda Bezi na mbili Kayenze.
Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Kayenze anaelezaMkuu wa shule ya sekondari Kayenze Mwalimu Deogratias Paul,anaeleza kuwa mazingira kwa ujumla ya Kata hiyo ikiwemo Kisiwa cha Bezi siyo mazuri kwani shughuli kubwa ni uvuvi hivyo watoto wengi ni watoro.
“Shule ya msingi Bezi ina wanafunzi wachache hivyo wanafaulu wote kuja sekondari na wanatumia usafiri wa kivuko(Feri) kuja shule na kurejea nyumbani,hivyo wanatumia takribani saa moja wakiwa ndani ya maji na wakifika nchi kavu wanatumia takribani dakika 15 kufika shuleni ambapo wanakuta kipindi cha kwanza kimeisha cha dakika 40 hivyo hawajawai kuhudhuria kipindi cha kwanza dakika 80,”anaeleza Mwl.Paul.
Mwl.Paul anaeleza kuwa kuna baadhi ya watoto wanaotoka kisiwa cha Bezi wamepanga nyumba(wanakaa geto) katika maeneo ya Kayenze ambapo huko ndio hatari zaidi kwani kunaweza kuchangia wao kuingia kwenye ndoa za utotoni,mimba za utotoni kwa watoto wa kike na kiume kuingia katika makundi mabaya kwa sababu uangalizi haupo maana wazazi wanakuwa mbali nao.
Anaeleza kuwa mazingira hayo ya umbali,kuishi katika nyumba za kupanga kunaweza kuchangia wao kuingia kwenye ndoa za utotoni,anaweza kuwa anaishi na mwanaume mzazi hajui kwa sababu ufuatiliaji haupo ingawa bado hawajabaini kama kuna mwanafunzi anayeishi na mwanaume huku anasoma kutokana na mazingira ya kukaa geto.
“Katika mazingira hayo ingawa hatuwezi kuthibitisha kwa kuwa hatujapata taarifa ya kuwa kuna mwanafunzi anayeishi na mwanaume lakini kiuhalisia kwa mazingira ya kuishi geto kwa mtoto wa kike anaweza kuwa yupo katika ndoa za utotoni lakini anahudhuria shuleni,”anaeleza Mwalimu Paul.Mkuu wa shule anaeleza suluhisho la kuwaokoa watoto wa kike.
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kila mtu anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu,huku serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vingine vya mafunzo.
Mwalimu Paul ,anaeleza kuwa suluhisho la kuwaokoa watoto wote hususani wa kike wanaotoka kisiwa cha Bezi na Kata hiyo kwa ujumla ili waweze kutimiza ndoto zao na kutokatisha masoko kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ndoa na mimba za utotoni ni kujenga bweni katika shule hiyo ya Kayenze sekondari.
“Tunaomba wadau wa elimu na serikali iwaonee huruma hawa watoto ili waweze kuwa shule muda wote na sisi walezi wao tukiwaangalia kwa ukaribu na kufikia malengo yao ili kuwanusuru na changamoto mbalimbali zinazoweza kukatisha masomo yao ikiwemo kuangukia kwenye ndoa za utotoni kwa kutujengea mabweni ya watoto wa kike na kiume hapa shuleni kwetu,”.
Pia ametoa rai kwa wazazi kuacha tabia ya kuwaozesha watoto wa kike katika umri mdogo aidha kwa tamaa ya fedha au kwa kumalizana kimya kimya bila kutoa taarifa kwenye vyombo husika baada ya binti kubeba mimba.
Safari kuelekea kisiwani Bezi nilipada gari (coaster) kutoka katikati ya Jiji la Mwanza mpaka Igombe, Kata ya Bugogwa kwa nauli ya Sh. 850,kisha kutoa Igombe hadi Kayenze kwa usafiri wa pikipiki unaogharimu kiasi Sh.3,000, au gari dogo kwa nauli ya Sh.1,500,Kutoka makao makuu ya Kata ya Kayenze nilipanda kivuko (feri) Mv. Ilemela na baada ya saa moja na dakika kama 15 hivi nilifika kisiwani Bezi.
Baada ya kushuka kwenye kivuko, nilitembea kuelekea upande wa Kaskazini kwa takribani dakika 15 hadi 20, nikafika ilipo ofisi ya serikali ya mtaa huo wa Kisiwa cha Bezi ambapo kwa asilimia kubwa uvuvi ndio shughuli kuu ya kiuchumi inayofanyika katika maeneo hayo.
Ambapo nilipokelewa na
Mbali na sheria,sera na Katiba pia Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (CRC),1989 na Mkataba wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa 1990 ni miongoni mwa jitihada za kuhakikisha mtoto anapata haki yake na kuondokana na vitendo vya ukatili ikiwemo ndoa za utotoni.
Mwenyekiti huyo Haruna, anaeleza kuwa katika uongozi wake suala la ndoa za utotoni katika mtaa wa Kisiwa cha Bezi changamoto hiyo kwa sasa haipo kwani anawaelimisha wazazi,wanashauriana huku akiwakemea ili jambo hilo la watoto kuingia kwenye ndoa za utotoni lisiweze kutokea katika kipindi chote cha uongozi wake.
“Mzazi anayeruhusu mtoto wake kuolewa kwa kukatisha masomo kwa sababu ya maridhiano ya pande mbili ni kinyume cha sheria na dhambi kwa Mungu kumkatisha ndoto zake,watoto wetu tunatakiwa tuwasimamie na tuwaelekeze, tuwafundishe maisha mema na kuchukua hatua za kisheria,sikubali kuridhiana ili watoto wa kike waingie kwenye ndoa za utotoni kwa sababu mbalimbali,”.
Suluhisho la watoto kutoka kisiwani Bezi kutumia umbali mrefu kwa ajili ya kufuata elimu ya sekondari Kayenze ni kupata mabweni katika shule ya sekondari Kayenze kwani siyo tu watoto wakike wanaopata changamoto hiyo hata wa kiume.
“Suala la upatikanaji wa bweni kwa ustawi wa elimu ya watoto wetu,linapaswa kufanyika kwa ushirikiano wa pande zote wazazi,jamii na serikali mfano hapa Ilemela kuna kauli mbiu ya kufanya kazi kwa utatu katika shughuli za maendeleo,hivyo inapaswa kuzingatiwa ili kuwasaidia na kuwaokoa watoto wetu waweze kutimiza ndoto zao,”.
Wazazi na wananchi wa Mtaa wa Kisiwa cha Bezi wazungumza
Mmoja wa wazazi wa watoto wanaishi Kisiwa cha Bezi,Lucy Paulo,anaeleza kuwa kutokana na mtaa huo kutokuwa na sekondari hivyo kuwalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kunaweza kuchangia watoto wa kike kukutana na vishawishi vitakavyowaingiza katika ndoa za utotoni.
“Tunaomba serikali itusaidie katika kuhakikisha shule ya sekondari Kayenze inapata Bweni ili kuepusha changamoto kwa kushirikiana na wazazi na jamii kwa ujumla kwani watoto ni wetu sote,”
Bertha Masasi anaeleza kuwa ndoa za utotoni zipo ambapo kwa asilimia kubwa watoto wanatoka katika maeneo mengine na kukimbilia kisiwani hapo kwa ajili ya kutafuta maisha baada ya kukatisha masomo na matokeo yake waangukia kwenye ndoa hizo.
“Inasikitisha ukiwakuta wapo na wanaume ukiwaeleza kuwa waachane na wanaume na warejee kwa ajili ya kusoma matokeo yake wataishia kukutukana,”
Mwenyekiti wa Mtaa wa Iseni,Kata ya Kayenze anena
Mwenyekiti wa Mtaa wa Iseni uliopo karibu na makao makuu ya Kata ya Kayenze Amos Mmbaga,anaeleza kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa wazazi na jamii juu ya madhara ya kutompeleka mtoto shule au kukatisha masomo yake na kumuingiza katika ndoa za utotoni.
“Hali si mbaya katika mtaa wangu juu ya ndoa za utotoni ila mimba za utotoni zipo mfano binti alipata ujauzito katika umri mdogo mzazi anawasiliana na ndugu yake alioko maeneo mengine ili kufanya namna ya kumuhamisha mtoto hapa ili kuficha hali iliojitokeza,hivyo bado hatujaelewa kama kumuhamisha huko ni kweli anakuwa amempeleka kwa ndugu au anakuwa amemuozesha kwa aliye mpa ujauzito,”.
Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009,ina mueleza kuwa mtoto ni mtu yoyote mwenyewe umri chini ya miaka 18.
Sheria hiyo pia inaeleza kuwa ulinzi wa mtoto ni kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya kikatili ambavyo vinaweza kuathiri mfumo wa ukuaji na maendeleo ya mtoto kiakili,kimwili na kisaikolojia.Ambapo vitendo vya ukatili ni pamoja na ndoa za utotoni,mimba za utotoni,kubakwa,kulawitiwa,kupigwa,utumikishwaji katika umri mdogo,usafirishaji haramu wa binadamu na mengine.
“Mimi ninachokiona ili kuzuia watoto kuingia kwenye ndoa za utotoni kimoja elimu itolewe,pili adhabu iongezeke iliopo kwa sasa haitoshi,mtaani kwangu sijapata kesi za ndoa za utotoni ila waliopata ujauzito wanapelekwa kwa ndugu zao maeneo mengine sasa huko hatujajua kama wanapelekwa kwa ndugu kweli au wanaenda kuozeshwa kwenye ndoa za utotoni,”anaeleza Amos.
Ili wanafunzi kutochangamana na makundi mbalimbali ya watu mfano bodaboda ambao wamekuwa wakitumia fursa hiyo kuwapa lifti watoto wakike ili kupata kile anachokitaka yeye kwa wakati huo bila kujua baadae kitatokea nini suluhisho ni kujenga bweni pamoja kutolewa elimu ya kujitambua na afya ya uzazi kwa watoto waliopevuka angalau mara moja kwa wiki kwani wao wenyewe wanajamiana.
Diwani wa Kata ya Kayenze anena
Diwani wa Kata ya Kayenze Issa Dida,anaeleza kuwa Kata yake ipo mwishoni mwa Wilaya ya Ilemela pia imepakana na Wilaya ya Magu hivyo kuna muingiliano wa watu kutokana na shughuli ya uvuvi, watu wanatoka hadi Ukerewe na Musoma kwa ajili ya kufanya shughuli ya uvuvi.
Kufuatia muingiliano huo changamoto kwa watoto ikiwemo mimba na ndoa za utotoni zinakuwepo kwani wazazi wengi wao hawana elimu na hawaangalii madhara yanaweza kutokea kwa watoto endapo hatopata elimu.
“Uwepo wa kumbi za starehe zimekuwa changamoto kwa watoto kuingia kwenye ndoa za utotoni kwa sababu ni rahisi kwao kupata ushawishi wa kujiingizia kwenye mapenzi katika umri mdogo hivyo kuangukia kwenye ndoa za utotoni,”.
Dida anaeleza kuwa shule ya sekondari Kayenze ina wanafunzi wanaotoka katika kisiwa cha Bezi ambao wanakutana na vishawishi vingi wawapo ndani ya feri wakati wa kwenda shule au kurejea nyumbani.Sera ya elimu ya mwaka 2014 inaeleza kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanakamilisha mzunguko wa elimu na mafunzo katika ngazi husika.
Kisiwani Bezi pia kuna starehe sana hivyo ushawishi ni mkubwa na tiba ni kupata mabweni katika shule ya sekondari Kayenze ambayo itaondoa mimba za utotoni,ndoa za utotoni na mambo mengine ambayo siyo mazuri yanayoweza kuchangia wanafunzi hususani wa kike kukatisha masomo.
Pia sera ya elimu ya mwaka 2014 inatoa tamko kuwa Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika.
“Tumekuwa na mkakati wa ndani ya shule ya sekondari Kayenze kwa kujenga mabweni angalau kwa kuanza na la kike ili wasiweze kukutana na vishawishi ambavyo vitaweza kuwaingiza katika ndoa na mimba za utotoni hivyo kukatisha masomo na ndoto zao,wadau na serikali itusaidie hupatikanaji wa bweni hilo,”.
Wito kwa wazazi na jamii watambue elimu ni kitu muhimu wanacholenga leo wajue kesho itawagharimu bila elimu ni kitu bure wanaangalia mkate wa siku moja ila kwa dunia inapoenda elimu ni muhimu.
Agizo la Makamu wa Rais mkoani Mwanza
Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa stendi ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori ya Nyamh’ongolo,wakati alipofanya ziara mkoani Mwanza mwaka 2022, Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango, anaeleza kuwa mimba na ndoa za utotoni ni kinyume na sheria na inachangia watoto kutofikia malengo na ndoto zao.
Hivyo aliwaagiza viongozi wa Mkoa wa Mwanza kuhakikisha watoto wanasoma na wasisite kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaokiuka na kuhusika kwa namna yoyote kukatisha masomo kwa mtoto wa kike kuwaacha watoto wasome,wasikatishe masomo yao kwani mimba na ndoa za utotoni hazikubaliki.
Hata hivyo Takwimu za UNICEF za mwaka 2012 ziliitaja mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni, huku Mkoa wa Mwanza ulishika nafasi ya kumi kwa kuwa na asilimia 37. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa asilimi 59, ukifuatiwa na Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55, Dodoma asilimia 51 na Lindi asilimia 48.
Takwimu za shirika hilo la UNICEF za kati ya mwaka 2010 na 2017 zinabainisha kuwa Tanzania ni ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni baada ya Sudan Kusini na Uganda. Sudan Kusini kiwango cha watoto wa chini ya miaka 18 wanaoozeshwa ni asilimia 52 na nchini Uganda ni asilimia 40 huku Tanzania ikiwa na asilimia 31.
Aidha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti uliochapishwa mnamo Januari, 2016 uliitaja Tanzania kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni kwa asilimia 28.
Kwa upande wake Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), kwa wastani watoto wakike wawili kati ya watano huolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Pia takwimu za utafiti wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS, 2010) asilimia 37 ya watoto wa kike Tanzania huolewa wakiwa na umri chini ya miaka 18.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika