Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Handeni
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amewataka watumishi wa afya watoe huduma kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao ikiwemo weledi,umahiri na upendo.
Amesema haitakuwa na maana Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya kwa kujenga miundombinu ya majengo,vifaa tiba na dawa kama watumishi watakuwa hawatoi huduma iliyo bora kwa wananchi.
Ameyasema hayo Julai 20,2024 alipotembelea Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni na kuzungumza na watumishi ikiwa ni muendelezo wa kufanya ziara kwenye Mkoa wa Tanga ambapo pamoja na mambo mengine, pia anakagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na viongozi wa UWT na wananchi.
“Mnatakiwa kutoa huduma iliyo bora kulingana na maadili ya taaluma yenu Msifanye kazi au kuhudumia watu kutokana na hali zao, bali toeni huduma sawa kwa watu wote na hayo ndiyo maadili ya kazi yenu” amesema Mhandisi Ulenge.
Mhandisi Ulenge pia alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Mkata na kuweza kutembelea wodi ya mama na mtoto kama alivyofanya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni ambapo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliweza kutoa shuka 10 kwenye kila hospitali hizo mbili kwenye wodi za mama na mtoto
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Handeni Dkt. Hudi Shehedadi alimshukuru Mhandisi Ulenge kwa kuwasaidia watoto njiti na watoto wachanga wanaozaliwa kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni kwa kutafuta wafadhili waliowezesha kupata vifaa vya kuwahifadhi watoto njiti na wachanga vyenye thamani ya sh.milioni 54,Pia amewezesha hospitali hiyo kupata sh.milioni 90 kwa ajili ya dawa za kuanzia matibabu kwa watoto hao.
Dkt.Shehedadi amesema kwa mchango huo alioutoa siku za nyuma na kwa niaba ya Halmashauri ya Mji Handeni wamempa Cheti cha Shukrani Mhandisi Ulenge kwani walikuwa hawana huduma hiyo na ili kuwapa huduma watoto hao kwa ajili ya kuwapa dawa na kuwahifadhi, walilazimika kuwapeleka Hospitali ya Rufaa Bombo, lakini kwa sasa huduma hiyo inapatikana hapo.
“Tunatoa Cheti hiki kama pongezi na shukran kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge,jambo alilofanya ni kubwa kwa kuweza kutafuta fedha kwa wafadhili sh.milioni 54 kwa ajili ya vifaa vya kuboresha huduma kwa watoto njiti na watoto wachanga,Lakini pia alitafuta fedha zaidi ya sh. milioni 94 zilizosaidia kununua dawa za kuanzia kwa ajili ya watoto njiti na watoto wachanga.
“Tulikuwa hatuna huduma hiyo na ili kuwapa huduma watoto hao kwa ajili ya kuwapa dawa na kuwahifadhi, tulilazimika kuwapeleka Hospitali ya Rufaa Bombo, lakini kwa sasa huduma hiyo inapatikana hapa hapa Handeni Tunawaomba wadau wengine kuiga mfano huo kwa ajili ya maendeleo ya jamii yetu” amesema Dkt. Shehedadi.
Mhandisi Ulenge akiwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Sindeni ya kidato cha tano na sita aliitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni (HTM) kupeleka maji ya uhakika kwenye shule hiyo. Kwani pamoja na jitihada alizozikuta hapo za kuchimba maji ya visima vifupi, bado haitoshi, kwani wanafunzi hao ni wengi, na hasa ukichukulia hao ni watoto wa kike.
Kwenye shule hiyo ambayo inafanya vizuri kwenye masomo ya sanaa, alitoa zawadi kwa wanafunzi 10 wa kidato cha sita waliofanya vizuri kwenye mitihani ya majaribio kwa masomo ya HGK na HGL kwa wale waliopata Daraja la Kwanza la pointi tatu hadi tano.
Akiwa Shule ya Sekondari Misima ya kidato cha kwanza hadi sita, aliwataka walimu kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao,ni baada ya shule hiyo kuonekana ina matokeo ya chini na kutoa motisha ya sh. 10,000 kila mmoja kwa wanafunzi 10 wa kidato cha kwanza waliofanya vizuri kwenye mitihani ya majaribio.
Mhandisi Ulenge ambaye alitembelea vikundi 11 vilivyopo Kata ya Kabuku na Komkonga vya akina mama wanaoponda kokoto na mawe meupe kwa ajili ya kuuza maeneo mbalimbali nchini, ambavyo vipo kata ya Kabuku na Komkonga, pamoja na kuwanunuza kokoto za sh. 550,000, bado ameahidi kuwanunulia vifaa ikiwemo viatu, miwani na nyundo kwa ajili ya kazi hiyo.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam