Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ametetea hoja ya dharura ya kutaka kuwepo kwa Mfuko utakaosaidia nchi zitakazopata majanga yatokanayo na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund).
Ameyasema hayo kwenye Mkutano wa 146 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika nchini Bahrain, ambapo Mhandisi Ulenge ni miongoni mwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania ambao wanashiriki.
Mkutano wa Bunge la Dunia unafanyika kwa siku saba kuanzia Machi 9 hadi 15, 2023 nchini Bahrain, huku wabunge wa Tanzania wakiongozwa na Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa nchi za Afrika katika Bunge la Dunia.
Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi Machi 12, 2023, Mhandisi Ulenge alisema kuna vikao ndani ya Bunge la Dunia, na Waafrika kupitia Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC), huwa wanakutana ili kujadili mambo yanayowahusu wao, na moja ya jambo wanalotaka ni kuwepo Mfuko utakaosaidia Mabadiliko ya Tabianchi.
“Kuna kuwa na vikao vya mabara mbalimbali ndani ya Bunge la Dunia ambapo Afrika nao wanakutana kama Bara la Afrika, na pia baadae wanagawanyika katika kanda mbalimbali, nasi Tanzania tunakutana kwenye upande wa nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
“Nimeweza kuchangia katika mkutano wa Bunge la Dunia kikao cha Umoja wa nchi za Afrika (Africa geopolitical group) unaofanyika nchini Bahrain kuhusu hoja ya dharura itakayojadiliwa na Umoja wa Mabunge ya Dunia. Nimeunga mkono hoja iliyowasilishwa na Tanzania kwa niaba ya Umoja wa Nchi za Afrika ya kuanzishwa kwa mfuko utakaosaidia nchi zitakazopata majanga yatokanayo na Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund)” alisema Mhandisi Ulenge.
Mhandisi Ulenge alisema katika mkutano huo, Spika ameambatana na Wabunge Wawakilishi kwenye Umoja huo ambao ni Joseph Mhagama (Jimbo la Madaba), na Elibariki Kingu (Jimbo la Singida Mashariki),
Wengine ni Mhandisi Ulenge ambaye ni mwanamke pekee kutoka CCM, Ramadhan Ramadhan (Chakechake), Dkt. Faustine Ndugulile (Jimbo la Kigamboni), Esther Matiko (Viti Maalumu- CHADEMA), pamoja na Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru