November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulenge ataka bei elekezi wanunuzi wa dagaa Pangani

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Pangani

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kuweka bei elekezi kwa wafanyabiashara ikiwemo raia wa DR Congo wanaokwenda kununua dagaa wilayani humo.

Ni baada ya kupewa malalamiko na vikundi vya wanawake wauza dagaa ambao wamesema wafanyabiashara hao wanakwenda kununua dagaa hao moja kwa moja kwa akina mama hao, lakini bei wanayowanunuza haina faida kwa wanawake hao.

Ameyasema hayo Jula 28, 2024 kwa nyakati tofauti alipotembelea vikundi vya wauza dagaa na samaki ikiwa ni ziara ya kutembelea vikundi vya wajasiriamali, kukagua maendeleo ya elimu kwa kuzungumza na walimu na wanafunzi, kugawa Bima ya Afya kwa wanawake na familia zao, na mikutano ya hadhara.

Mhandisi Ulenge amesema wanawake hao kuuza kilo moja ya dagaa waliochemshwa kwa sh. 3,500 haiwezi kumpa faida sababu yeye alinunua dagaa wabichi kwa ndoo sh. 45,000 hadi 50,000, na kutaka bei ya dagaa hao iwe sh. 5,000 ama sh. 7,000.

“Halmashauri ya Wilaya ya Pangani iweke mipango ya kuweza kuwasaidia wanawake wajasiriamali wanaouza dagaa kwa wageni, nimeelezwa na wanawake hapa kuwa bei wanayouza dagaa kwa Wacongo haiwasaidii, wanapata hasara,hivyo ikiwezekana wekeni bei elekezi kuwasaidia na nipo tayari kwenda kulisemea bungeni suala hilo ili wanawake wapate maslahi ya biashara yao” amesema Mhandisi Ulenge.

Akizindua kijiwe cha Kikundi cha Wanawake Wauza Samaki Choba, Mhandisi Ulenge amesema anajua shughuli za kiuchumi kwa wanawake wa Ukanda wa Pwani wanategemea Uchumi wa Buluu kwa shughuli za uvuvi, na kulima mwani, hivyo ni lazima kuwe na mipango ya kuwasaidia ili waweze kunufaika na shughuli za kiuchumi.

“Mimi kama Mbunge, huwa napanga malengo, huwa napanga mikakati na nina ajend na kwa kuwa Tanga yetu imegawanyika katika ukanda wa bahari na ukanda usio na bahari (Usambara), basi huko kote nimeangalia vipaumbele vya wanawake kulingana na mazingira yetu na ikumbukwe kwamba mimi ni mwana bahari, mimi ni mwana pwani, hivyo kuweka kipaumbele cha Uchumi wa Buluu namaanisha haswa akina mama wa pwani.

“Hivyo tuone fursa ambazo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameziweka kwenye Uchumi wa Buluu hata Ilani ya CCM imeelezwa vizuri namna ambavyo inatamani kujenga uchumi shirikishi, uchumi fungamanishi kwa maendeleo ya watu na watu wenyewe ndiyo kama ninyi na katika kutekeleza Ilani ya CCM,Rais Dkt. Samia aliweka kabisa kipengele cha Uchumi wa Buluu” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge amesema yeye kama Mbunge ambaye ametokana na wanawake wa Mkoa wa Tanga amekuwa akifuatilia kuona wanawake wa Ukanda wa Pwani wananufaika na Uchumi wa Buluu na katika maeneo mengine wanaweza kupata mafanikio ikiwemo kujenga nyumba na kutolea mfano Wilaya ya Kilwa, ambapo msichana mdogo amejenga nyumba zaidi ya nne, huku mama zao pia wakiwa wamejenga nyumba.

Akijibu hoja ya wanawake wajasiriamali hao mbele ya Mbunge Mhandisi Ulenge, Ofisa Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Gabriel Namate amesema changamoto hiyo wameichukua na kwa sababu hilo ni suala la mapato kwa halmashauri hiyo, wataipeleka hoja hiyo kwenye Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, na kisha kuingizwa kwenye Baraza la Madiwani ili kuweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema jambo hilo wanakwenda nalo kwa tahadhari ili wanunuzi hao kutoka Congo wasije wakawakimbia wajasiriamali hao, kwani hao watu wanazunguka nchi nzima, hivyo wakiweka bei elekezi ama bei ya juu zaidi, wanaweza kukimbilia Wilaya ya Mkinga, Mafia ama Kilwa.

Hatahivyo katika kuunga mkono jitihada za wanawake wa kikundi cha Choba, aliwapa sh. 300,000 ili kuongeza mtaji wao.