December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulenge agawa mbegu kwa wanawake Tanga

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amegawa mbegu bora za mazao ya mahindi, mpunga, ngano, alizeti, maharage, mchicha, nyanya na ngogwe zikiwa na thamani ya milioni 12.5 kwa wanawake wa Mkoa huo.

Ulenge amewaeleza wanawake hao kuwa hawataweza kuendelea bila kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Waziri Ally

Amesema siasa za kugawa khanga na vitenge anazijua sana, lakini yeye hawezi kufanya hivyo sababu vitu hivyo haviwezi kumsaidia mwanamke ili waendelee ni bora akawawezesha ili waweze kujitegemea na kuendesha shughuli za kiuchumi.

Ameyasema hayo Aprili 6, 2024 kwenye hafla ya kukabidhi mbegu hizo kwa wanawake wa Mkoa wa Tanga iliyofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe, na kuongeza kuwa dhamira yake ya kwenda kugombea Ubunge ni kuwapa nafuu wanawake wa Tanga katika kuwajenga kiuchumi.

“Dhamira ya mwanamke na uchumi
itakwenda kupitia kilimo,kiongozi lazima aoneshe dhamira iliyomfanya kugombea nafasi aliyoomba,siyo kusema kero tu Bungeni bali nia yangu ni kumuona mwanamke wa Tanga anasimama kiuchumi,”.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge (katikati) akigawa mbegu za maharage na alizeti kwa wanawake wa Wilaya ya Kilindi

Mhandisi Ulenge amewataka maofisa ugani kuwasaidia wanawake ili waweze kufanikiwa kwenye shughuli za kilimo kwani wao ni watumishi wa serikali na wapo hapo ili kumsaidia mkulima kulima na kuvuna kwa tija.

Lakini pia amewataka wanawake hao wasiogope kuwapigia simu maofisa ugani ili kupata ushauri wa namna ya kuboresha kilimo chao kwani Mkoa wa Tanga una ardhi nzuri ya kuweza kulima alizeti kuliko Mkoa wa Singida.

Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Korogwe Mjini Faidha Bayagubu amesema kuwa kupitia mbegu waliyopewa na Mbunge huyo kuwa watalima alizeti kwa wingi na kupanga vidumu pembezoni mwa barabara kuu ya Dar es Salaam- Arusha.

Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Korogwe Vijijini Hadija Mshahara amesema wanajivunia kuwa na Mbunge Ulenge, kwani hicho anachowafanyia kuwawezesha wanawake hasa kwenye shughuli za kilimo ni ukombozi kwao.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge

Mwenyekiti wa CCM Wilaya Korogwe Vijijini Waziri Ally amewataka maofisa ugani kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora ikibidi waweze kutengeneza mbegu wenyewe, kwani wataweza kuzalisha nyingi na kuweza kupanda mazao mengi.

Wanawake wa Mkoa wa Tanga wakimpokea Mbunge wa Viti Maalumu Mhandisi Mwanaisha Ulenge
Sehemu ya mbegu iliyogawiwa kwa wanawake wa Mkoa wa Tanga.