March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega: Samia ndiye pekee mwenye nia ya kuletea katiba mpya

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

Waziri wa Ujenzi na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Ulega, amewataka Watanzania kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, akisema ndiye kiongozi pekee mwenye dhamira na uwezo wa kufanikisha upatikanaji wa Katiba Mpya ya Tanzania.

Akizungumza leo katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa CCM uliofanyika katika viwanja vya Kongowe, Ulega alisema kuwa ilani ya chama hicho kwa mwaka 2025–2030 imeweka bayana mpango wa kufufua mchakato wa Katiba Mpya, na kwamba Rais Samia ana uzoefu na maono ya kulitekeleza jambo hilo.

“Uchaguzi huu unatupa fursa ya kihistoria. Rais Samia anaweza kutuachia zawadi kubwa ya kitaifa – Katiba Mpya ambayo Watanzania tumekuwa tukiitamani kwa muda mrefu,” amesema Ulega.

Akimnukuu Rais Samia kama kiongozi mwenye historia ya maridhiano, Ulega alikumbusha mchango wake katika Kamati ya Maridhiano iliyowezesha Mwafaka wa Kisiasa Zanzibar, nafasi yake kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, pamoja na kuasisi falsafa ya 4R inayojikita katika maridhiano ya kitaifa.

Ulega amesisitiza kuwa marais wengi nchini wamefanikisha mageuzi makubwa katika awamu zao za pili za uongozi, akitoa mifano ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyeruhusu mfumo wa vyama vingi na Jakaya Kikwete aliyeunda Tume ya Jaji Warioba.

“Tukimchagua Rais Samia kuingia awamu ya pili, Katiba Mpya itakuwa kipaumbele chake. Tukimchagua mtu mwingine, suala hili litasahaulika. Hivyo Oktoba lazima twende kumchagua Dk. Samia,” amesema.

Katika mkutano huo uliovutia maelfu ya wananchi, Ulega pia alieleza mafanikio yaliyopatikana Mkuranga chini ya uongozi wa Rais Samia, ikiwemo ongezeko la zahanati, vituo vya afya, pamoja na shule za msingi na sekondari. Aliongeza kuwa Mkuranga sasa imekua kitovu cha viwanda na inatarajiwa kunufaika zaidi iwapo Rais Samia ataendelea kuongoza.

Miongoni mwa miradi inayosubiri utekelezaji ni upanuzi wa barabara ya Kilwa, ambao utarahisisha usafiri kati ya Mkuranga na Jiji la Dar es Salaam.

“Mkuranga ya leo siyo ya jana. Umeme umefika vijiji vingi, shule za ghorofa zimeanza kujengwa. Nikishirikiana na Rais Samia, hakika kesho ya Mkuranga itakuwa bora zaidi,” amesema Ulega, ambaye anawania ubunge kwa mara ya tatu.