Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online Sengerama
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekitaka Chama cha
Ushirika cha Zilagula wilayani hapa kutumia vyema mkopo uliotolewa na
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kujenga boti za kisasa ili boti
hizo zisaidie viwanda vya samaki Jijini Mwanza kupata malighafi kwa
wakati na kwa uhakika.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki mara baada ya
kuridhishwa na ujenzi wa boti tatu za kisasa za uvuvi, kati ya boti
tano, ambazo zinajengwa kwa mkopo wa sh. milioni 100.7 ambao umetolewa
TADB kwa chama hicho.
Ulega amesema pesa hiyo ni mkakati wa Serikali wa kuwapatia wavuvi vyombo vya kisasa na kwamba matumizi mazuri ya boti hizo utavifanya viwanda kupata malighafi kwa uhakika na pia kuifanya sekta ya uvuvi kutoa mchango mkubwa zaidi kwenye pato la taifa.
“Mpango wa Serikali ni kuona sekta ya uvuvi inatoa mchango zaidi
katika ukuaji wa pato la Raifa na ndiyo maana TADB wametoa kiasi hiki
cha pesa ili muweze kupata boti za kisasa zitakazowasaidia kufanya
vyema shughuli zenu,” amewaeleza wanaushirika hao na kuongeza kuwa ni
vyema mkopo huo ukatumika vizuri na marejesho yake yafanyike kwa
wakati.
Amesema kuwa viwanda vya samaki mkoani hapa vinakabiliwa na uhaba wa
samaki na kwamba ni matumaini ya Serikali kwamba boti hizo
zitaongeza samaki wanaohitajiwa na viwanda.
Amesema kwamba wavuvi nao wauze samaki moja kwa moja viwandani ili kuepuka njama za walanguzi.
“Kilio cha wavuvi wengi ni walanguzi wanaowanyonya. Walanguzi
wamekuwa wanufaikaji wakubwa wa nguvu ya mvuvi. Uwepo wa boti hizi
utawezesha kupata samaki wengi zaidi ambao watauzwa kwa bei nzuri kwa
sababu samaki wanahitajika katika soko la ndani na nje ya nchi,”
amesema.
Aidha amewashauri wavuvi wengine mkoani Mwanza waunde vyama vya
ushirika ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi za
fedha, ikiwemo TADB.
“Wito wangu kwenu ni kujiunga katika vyama vya ushirika ili muweze
kupata mikopo inayotolewa na taasisi za fedha. Vyama hivyo sio tu
kwamba vitawawezesha kupata mikopo lakini pia vitawawezesha kuwa na
uhakika wa soko la samaki mtakaowavua,” amesema Ulega.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, aliambia hadhara hiyo
kuwa benki yao itaendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazojitokeza
ikiwemo kukosekana kwa mikopo kwa baadhi ya vyama vya ushirika licha
ya kufuata taratibu zinazotakiwa.
“Mwanzoni tuliwaomba wavuvi waunde vyama vya ushirika ili tuweze
kuwapa mikopo. Tunashukuru kwa sababu mwitikio umekuwa mkubwa na hivyo
kurahisisha kazi ya kuratibu mikopo inayotolewa na benki,” alisema na
kuongeza kwamba mkakati wa benki ni kunufaisha vyama vyote vya
ushirika.
Justine ameeleza kuwa mkopo huo wa sh. milioni 100.7 umelenga
kutengeneza boti tano za uvuvi, kujenga eneo la kuhifadhia samaki
pamoja na kukisaidia chama hicho kutekeleza mipango yake mingine.
Mwenyekiti wa chama cha Ushirika cha Zilagula, Joram Yuda,
aliipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya kuweka mikakati madhubuti
ambayo alisema imeifanya sekta ya uvuvi kuaminiwa na taasisi za fedha,
ikiwemo TADB.
“Kwa sasa wavuvi tunapata huduma za mikopo kutoka kwenye taasisi za
fedha ikiwemo Benki ya Kilimo. Haya ni matunda ya Serikali katika
kuhakikisha sekta muhimu kama kilimo, uvuvi na ufugaji zinaaminiwa na
kukopesheka ili kurahisisha utendaji wa sekta hizo muhimu,” alisema
Yuda.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi