January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ulega awahimiza wafugaji kuishi kwa kufuata sheria

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewataka Wafugaji kuishi kwa amani na kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kuacha tabia ya kuingiza na kulisha mifugo yao katika mashamba ya Wakulima.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa kikao chake cha kusikiliza kero na changamoto za wafugaji wa Wilaya ya Namtumbo kilichofanyika Wilayani humo Septemba 19, 2024.

“Wafugaji muishi na watu vizuri, acheni ubabe, fuateni sheria, msiingize mifugo katika mashamba ya watu kwa makusudi, ni jambo baya sana,, msipofuata sheria kila mtu mtamuona mbaya”, amesema

Waziri Ulega aliongeza kwa kuwataka wafugaji hao kuunda mabaraza ya wazee ya wafugaji ili yasaidie kusuluhisha migogoro na kukemea wale wafugaji wachache wanaotaka kuharibu taswira ya ufugaji hapa nchini.

Halikadhalika aliwahimiza wafugaji hao kuweka utaratibu wa kuvuna mifugo yao na kuiuza, kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kujipatia kipato lakini pia kupunguza wingi wa mifugo ili kujiepusha na migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amewaelekeza Wataalamu kutoka Wizarani kwake kwenda kutoa elimu ya ufugaji bora na fursa zilizopo kwenye ufugaji kwa viongozi, wafugaji na makundi mengine katika wilaya hiyo ili wajue umuhimu wa uchumi jumuishi.