Na Edward Kondela,TimesMajira Online,Dar
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesikiliza kero za wafanyabiashara wa mnada wa kimataifa wa Pugu uliopo jijini Dar es Salaam ukiwemo utaratibu wa utoaji wa huduma katika mnada huo, uhaba wa maji, uchakavu wa miundombinu ya kuhifadhia mifugo na ubovu wa eneo la kushusha na kupakia mifugo.
Akiwa jijini Dar es Salaam katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mnada huo jana, Naibu Waziri Ulega amearifiwa pia changamoto ya ukosefu wa taa ndani ya mnada huo, jambo ambalo Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Bi. Tabu Shaibu ameahidi kulishughulikia ndani ya wiki moja.
Wakifafanua juu ya changamoto hizo baadhi ya wafanyabiashara hao wamemueleza Naibu Waziri Ulega kuwa biashara katika mnada huo inaanza saa moja asubuhi, lakini changamoto wanayoipata ni suala la ukatishaji wa ushuru ambapo watumishi wanafungua ofisi saa tatu asubuhi kwa mujibu wa mwongozo wa minida.
Aidha wameeleza kuwa bado wanakabiliana na kero mbalimbali ikiwemo ya uchakavu wa paa la eneo la kuhifadhia mifugo yao, wakisema wakati wa mvua wanapata shida ya kujikinga wao pamoja na mifugo wanayoihifadhi.
Akifafanua juu ya utatuzi wa kero hizo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (Mb) amewaelekeza watendaji wa mifugo wa wizara hiyo, kurekebisha mwongozo wa mnada ili kuruhusu shughuli za huduma kuanza saa moja asubuhi badala ya saa tatu asubuhi.
“Lengo la ziara hii ni kuangalia utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo kukagua ujenzi wa uzio unaozunguka mnada huu pamoja na kupokea na kushughulikia kero zinazowakabili wafanyabiashara.” amesema Ulega.
Ameongeza kuwa mwongozo huo uliwekwa wa saa tatu asubuhi kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanaweza kufanya ujanja wa kwenda na mifugo katika minada kisha kuondoka nayo kwa kisingizio cha kukosa wateja na kuikosesha serikali mapato.
Amebainisha sababu nyingine kuwa ni upatikanaji wa huduma za kifedha kwa muda wa kuanzia saa moja asubuhi, hata hivyo amesema kitendo cha huduma hizo kuanza saa tatu badala ya saa moja asubuhi kinasababisha watanzania kukosa biashara kwa wale wanaotegemea mazao ya mifugo.
“Shusheni muda hadi saa moja asubuhi, ongeeni na watu wa mabenki waanze kutoa huduma kuanzia muda huo. Polisi wapo wana uwezo na uweledi wataimarisha ulinzi. Rais Samia Suluhu Hassan anapenda watu wafanye kazi na kulipa ushuru naagiza shusheni muda.” alisema Ulega.
Kuhusu changamoto la paa, Mhe. Ulega amesema mkandarasi ameshapatikana na kazi ya kupaua na kurekebisha eneo itaanza mara moja na itafanyika usiku na mchana na kwamba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeshafikisha maji katika mnada huo.
Ameongeza kuwa kilichobaki ni miundombinu ya mabomba na mchakato utakamilika ndani ya wiki moja na kuhusu uzio kazi imeshaanza na amemuelekeza mkandarasi akamilishe kazi hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu.
Pia Naibu Waziri Ulega amewaarifu wafanyabiashara hao kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameupa mnada wa Pugu Shilingi Milioni 600, kwa ajili kutengeneza eneo la kunyweshea mifugo maji na mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kazi hiyo itakayoanza wiki ijayo.
More Stories
Rais Dkt.Samia asajili timu ndani na nje ya Nchi kukabili Marburg
RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa
Wapanda miti 500,kumbukizi ya kuzaliwa Dkt.Samia