Na Benny Mwaipaja,TimesMajira Online
UMOJA wa Ulaya (EU) kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 30 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 84 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia.
Sehemu ya fedha hizo, kiasi cha Euro milioni 26 sawa na shilingi bilioni 72, mkataba wake uliingiwa jana jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Stephanie Mouen Essombe.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema kuwa fedha hizo kiasi cha Euro milioni 26 kitatumika kujenga kituo cha kupooza umeme – Tunduma, kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kv 330 yenye urefu wa kilometa 4 kutoka Tunduma hadi mpakani mwa Tanzania na Zambia.
“Mradi huu pia unahusisha ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme katika maeneo ya vijijini, ambayo hayajafikiwa na Grid ya Taifa na kuongeza uwezo wa njia zilizopo za kusafirisha umeme kupitia Iringa – Kisada – Mbeya – Tunduma – Ushoroba wa Sumbawanga,”amesema James.
Amesema, hatua hiyo itaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea uzalishaji katika maeneo ya vijiji husika na pia kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo yasiyofikiwa na yale ambayo umeme hautoshi hususan maeneo ya Kusini Magharibi mwa nchi yetu, ambayo yamekithiri umaskini.
James amesema kuwa msaada huo unaonesha kwamba Jamhuri ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya ni marafiki wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na dhana ya baadhi ya wapinzani wa nchi wanaodai kwamba uhusiano wa Tanzania na wadau wake wa maendeleo unadorora.
“Kupitia uhusiano wetu huu mzuri tunatambua kuwa kiwango cha uwekezaji cha AFD kwa Serikali ya Tanzania kimefikia takriban Euro milioni 454.5, sawa na shilingi trilioni 1.26 ambazo zinajumuisha mkataba uliosainiwa hivi karibuni wa mkopo wa masharti nafuu wa Euro milioni 100 kwa ajili ya mradi huu,”ameongeza James.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa Bi Stephanie Mouen Essombe amesema kuwa miezi michache iliyopita Shirika lake lilisaini mkataba wa mkopo nafuu wenye thamani ya Euro milioni 100 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa kusafirisha umeme wa Tanzania na Zambia.
“Leo tumekutana tena kwa ajili ya kusaini mkataba wa kiasi kingine cha nyongeza cha Euro milioni 26 sawa na shilingi bilioni 72 ambazo ni msaada uliotolewa na Umoja wa Ulaya kupitia Shirika letu,”amesema Stephanie.
Amesema,mradi wa kusafirisha umeme kati ya Tanzania na Zambia ni sehemu ya mwisho ya utekelezaji wa mradi wa ushoroba (corridor) kutoka Ethiopia, Kenya, Tanzania na Zambia unaolenga kupunguza gharama za matumizi ya nishati hiyo pamoja na kukuza uchumi wa nchi husika.
Amesema kuwa hivi karibuni, Shirika lake litatoa kiasi kingine cha Euro milioni 130 kwa ajili ya kutekeleza mradi mwingine mkubwa wa nishati jua (solar PV Power) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50, utakaojengwa mkoani Shinyanga.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Mhe. Frederic Clavier, amesema uhusiano wa Tanzania, Ufaransa na Umoja wa Ulaya uko imara na kwamba nchi hizo zitaendelea kuchangia maendeleo ya nchi kwa juhudi zote.
Amefafanua kuwa nchi yake kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) itaendelea kuwekeza katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii ambapo katika kipindi cha miaka 10 Bodi ya wakurugenzi ya AFD imeidhinisha matumizi ya kiasi cha Euro milioni 430 kwa ajili ya sekta ya nishati.
Naye Kaimu Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti, amesema kuwa mbali na msaada wa kiasi hicho cha Euro milioni 26 zilizosainiwa, Umoja wake utatoa kiasi kingine cha msaada wa Euro milioni 4 kwa ajili ya kulijengea uwezo Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) na kufanya kiasi kilichotolewa na EU kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) kufikia Euro milioni 30 sawa na shilingi bilioni 84.
Amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya unatambua jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kwamba Umoja wa Ulaya utaendelea kuunga mkono juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa