November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukerewe Kisiwa chenye fursa ambazo hazijachangamkiwa

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

MKOA wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa mabayo imebarikiwa kuwa na visiwa vingi katika ziwa Victoria, ambavyo sio tu muhimu kiuchumi bali ni urithi wa kihistoria katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na hata Kusini.

Miongoni mwa visiwa hivyo ni Ukerewe ambavyo ni muunganiko wa visiwa 38 kati yake vikubwa vikiwa viwili Ukerewe ambapo ndio makao makuu ya Wilaya na Halmashauri kwa ujumla katika mji wa Nansio, pamoja na Ukara, aidha visiwa vingine 36 na vyenyewe vina ukubwa tofauti na kila kimoja kina shughuli zake za kimaendeleo zinazofanyika.

Kumekuwa na dhana potofu juu ya visiwa vya Ukerewe kwamba hakuna fursa wala hakuna shughuli zozote ambazo zingeweza kuwaletea wananchi maendeleo, lakini pia hakuna shughuli za kiuchumi na kibiashara ambazo zingeweza kuinua kipato cha wakazi wa Ukerewe kadhalika wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika Nyanja mbalimbali.

Ukweli ni kwamba Ukerewe ni visiwa vyenye fursa adhimu ambazo hazijachangamkiwa na wawekezaji pia wafanyabiashara, hii inasababishwa na kutokuwepo kwa taarifa sahihi na za kina juu ya umuhimu na urahisi wa kuwekeza katika visiwa hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Esther Chaula, anabainisha kuwa katika Tanzania hususan Kanda ya Ziwa visiwa hivyo vina fursa nyingi sana ambazo wawekezaji wakizichangamkia wanaweza kupata faida kubwa, pia wakaazi wa visiwa hivyo wakapata ajira, kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa kipato kutokana na uwekezaji utakaokuwepo.

“Unapozungumzia samaki katika ziwa victoria, Ukerewe peke yake inazalisha tani 3800 za sangara na sato kwa mwaka, pamoja na tani 8000 za dagaa kwa mwaka jambo ambalo linaweza kukaribisha wawekezaji wakubwa wa viwanda vya kuchakata na kusindika samaki” anasema Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Ukerewe.

Anasema visiwa hivyo pia ni maarufu kwa uzalishaji wa machungwa na machenza, ambapo kwa mwaka wanazalisha takriban tani 78000 pia kwa upande wa maembe wanazalisha tani 12000 kwa mwaka.

Uwepo wa kiasi kikubwa cha uzalishaji wa matunda, ni fursa pia ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza na kukamua juisi kutokana na matunda hayo.

Kuhusu uwekezaji katika hoteli, Chaula amesema Ukerewe ni sehemu yenye uhitaji mkubwa sana wa hoteli kwa ajili ya wageni, hivyo akawahamasisha wawekezaji mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi kwenda kuwekeza kwani watapata faida kutokana na kukosekana kwa hoteli za uhakina na zenye viwango.

Aidha Chaula anasema kuwepo kwa fukwe nzuri kwenye visiwa vyote 38 kunaweza pia kukawa fursa kwa wawekezaji wa hoteli za kitalii ambao watahitaji kuwekeza katika eneo hilo.

Uwekezaji mkubwa pia unahitajika katika usafiri wa majini kati ya Mwanza na Ukerewe, pia kutoka visiwani kwenda katika mikoa mingine kama Mara na Kagera hii itasaidia kupanua shughuli za kiuchumi katika visiwa hivyo,” anasema Chaula.

Ukerewe, Kisiwa kikubwa kuliko vyote katika ziwa Victoria na kikubwa zaidi barani Afrika chenye ukubwa wa takribani kilometa za mraba 530.

Anasema pamoja na kuwa na meli ya Serikali ya Mv.Clarious ambayo inafanya safari zake kati ya Ukerewe na Mwanza, pamoja na meli nyingine za kampuni binafsi, usafiri wa uhakika katika visiwa hivyo unahitajika hivyo akatoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kuchangamkia fursa hiyo ili kuongeza wigo wa usafiri.

Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Bi.Esther Chaula, amesema kwa upande wa kilimo visiwa hivyo vinazalisha tani 17000 za mpunga kwa mwaka hivyo ni fursa pia, kwa uwekezaji mkubwa wa viwanda vya kukoboa na kuchakata mpunga pamoja na mazao mengine ya nafaka.

Visiwa vya Ukerewe ni mahali salama kwa uwekezaji, kwanza kuna huduma zote muhimu za kijamii ikiwemo maji, umeme wa uhakika,barabara za lami, shule za msingi na sekondari ,hospitali ya wilaya na vituo vya Afya pamoja na chuo cha ualimu Murutunguru, anasema Mkurugenzi huyo.

“Nawakaribisha wawekezaji waje kwa wingi huku kuna fursa nyingi mno ambazo hazijachukuliwa wala kufanyiwa kazi, mtu akihitaji ardhi kwaajili ya kuwekeza ipo aje mara moja ofisini kwangu tumwelekeze taratibu na tutahakikisha anapata ardhi yake ndani ya muda mfupi ili aanze shughuli zake, anasema.

Mkurugenzi huyo wa Ukerewe anasema hakuna urasimu wowote kwa mwekezaji anayetaka kuwekeza, kwani lengo lao ni kuona wanaanchi wanapata maendeleo lakini pia wawekezaji wanawekeza kwenye eneo ambalo wanapata faida na hatimaye wafurahie matunda ya kuwekeza visiwani humo.