November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukarabati Mv Ukerewe na meli ya MT Nyangumi kurudisha usafiri wa uhakika ziwa Victoria

 Na Penina Malundo, timesmajira

UKARABATI wa viwango vya juu vya meli kongwe za abiria MV Ukerewe pamoja na meli ya MT.Nyangumi zinazofanya kazi katika ziwa Victoria,zinaelekea kuanza kufanyiwa uboreshwaji wake katika kuhakikisha zinarudisha safari yake ili kuhakikisha usafiri wa uhakika unapatikanaji kwa wananchi wa maeneo hayo ya kanda ya ziwa.

Na meli hizo zinapoenda kukamilika zitaweza kuleta tija kwa wananchi na kukuza uchumi wao mmoja mmoja au kwa taifa kwa kufanya biashara kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kampuni ya kizalendo ya Dar es Salaam Merchant Group (DMG), ni miongoni mwa kampuni ambayo itaenda kufanya ukarabati uliotukuka na wenye uwezo wa viwango vya juu katika meli hizo na kuzirudisha katika hali yake ya awali.

Ukarabati wa meli hizo utatumia gharama ya kiasi cha sh. Bilioni 14 ambazo zitatumika kufanyia ukarabati hadi hapo  zitakapokamilika.

Kufuatia ukarabati huo,sasa ni wakati wa wananchi waliopo kanda ya ziwa wanaotumia usafiri huo kupitia ziwa victoria kuanza kujiandaa katika kuhakikisha wanatumia vyombo hivyo vya majini kwa manufaa makubwa na yenye kuleta tija kwa jamii.

Katika hili tunaona ni namna gani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inavyoendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha meli hizo zinafufuliwa na zinaanza kazi ili kuendelea kuboresha usafiri huo katika maeneo hayo ya kanda ya ziwa.

Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja  na hivi karibuni serikali kutia saini ya mikataba mitatu ya ukarabati wa meli hizo ambao ulifanyika katika bandari ya kusini Mwanza chini ya  Waziri wa Wizara ya Uchukuzi David  Kihenzile.

Nionavyo ukamilikaji wa meli hizi utaweza kufungua fursa nyingi za ajira binafsi na kupunguza gharama za usafirishaji sambamba na kuongeza tija katika shughuli za biashara kufanya wananchi wengi kunufaika.

Hivyo katika kutekeleza vyema ukarabati huo,serikali itaweza kuokoa gharama ya kujenga au kutengeneza meli mpya.

Ni wakati wa wananchi  kuchangamkia fursa kwani meli hizo zitaweza kupbeba bidhaa mbalimbali ambazo zitaongeza chachu ya ukuaji wa uchumi katika maeneo hayo.

Ukamilikaji wa meli hizi unapaswa kuangalia wananchi wenyeji wanapaswa kupewa kipaumbele cha kupewa ajira  hivyo ni jukumu la viongozi wa mikoa kusimamia vyema na kuhakikisha wanalinda na na kupinga uhujumu uchumi katika miradi hiyo.