December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ukamilishwaji wa kituo cha Afya Rusumo charudisha kicheko kwa wananchi

Na Penina Malundo, Timesmajira,Ngara

UKAMILISHWAJI wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Rusumo na uwekwaji wa vifaa tiba pamoja na ufungwaji wa mashine za kiuchunguzi za kisasa zimerudisha tabasamu jipya kwa wananchi waishio Rusumo na Benako mkoani Kagera kwa kurudisha kicheko kilichopotea miaka mingi.

Tabasamu hilo limekuja baada ya wananchi hao kuona huduma bora za kiafya na za kibingwa kuanza kutolewa katika Kituo hicho cha afya ambacho kipo karibu na maeneo yao.

Miaka ya nyuma wananchi hao walikuwa wakipata huduma hizo kwa hospitali zilizopo umbali wa Kilomita tano ikiwemo hospitali ya wilaya ya Ngara kupata matibabu .

Upatikanaji huo wa huduma za afya kwa maeneo hayo ya rusumo yamewezeshwa na Miradi ya Maendeleo ya Kijamii (LADP) chini ya Mradi Mkubwa wa kufua umeme wa Rusumo uliopo katika Mpango wa bonde la mto nile (Nile Basin Initiative NELSAP ) na kufadhiliwa na Benki ya Dunia(World Bank),kwa kuwajengea kituo cha afya wananchi hao.

Kituo cha Afya hicho kilijengwa na LADP,kwa kuwezeshwa na  NELSAP kupitia ufadhili wa Benki Kuu ya Dunia ambapo kilianza kazi rasmi Februari,2022 lengo ikiwa ni  kusogeza huduma kwa wananchi badala ya kutumia muda mrefu kutembea kufata huduma ya afya kwa vijiji vingine.

Kwa sasa kituo hicho kimekamilika kwa asilimia 100 na kimeweza kuongeza idadi ya  wagonjwa wanaotibiwa kutoka wagonjwa  250 kwa mwezi,hadi  kufikia wagonjwa 600 kwa mwezi.

Ongezeko hilo la wagonjwa ni kutokana na kituo hicho cha afya kukamilika kwa asilimia 100 na wananchi kuanza kujipatia matibabu bila kutumia gharama kubwa za usafiri na hata kupoteza wapendwa wao sababu ya umbali kama hapo awali.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Rusumo,Atwemela Adolph anasema wanaishukuru Serikali, Benki kuu ya Dunia pamoja na NELSAP kwa kukamilisha ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho kilikuwa kilio cha wananchi wengi waishio maeneo hayo.

Anasema wanufaikaji wakubwa wa kituo hicho  cha afya ni  wananchi wanaozunguka mradi wa kikanda wa kuzalisha nishati ya umeme kutoka maporomoko ya maji Rusumo pamoja na maeneo jirani ambao wamekuwa wakipata huduma za kiafya katika kituo hicho. 

Adolph anasema baada ya kukamilika kwa kituo hicho kwa asilimia 100 kwa sasa na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo ya  kulaza wagonjwa ,kufanya upasuaji na kupima vipimo mbalimbali ikiwemo figo,Ini na damu.

Anasema kwa sasa majengo yote yamekamilika pamoja na vitendea vya maofisini na mashine mbalimbali za uchunguzi za kimaabara zimeweza kufungwa katika hospitali hiyo.

Adolph anasema kwa hatua hiyo kazi yao imeweza kuimarika kwa asilimia kubwa kwani awali baada ya majengo ya kituo cha afya hicho kukamilika walikuwa wanatoa huduma za kawaida kuwatibu wagonjwa huku wakiwa hawana umeme hivyo kuradhimika kutumia umeme wa jua kipindi cha jua kali au tochi za kawaida kukiwa kipindi cha mvua.

”Tunashukuru sana NELSAP kwa hatua hii kubwa ya kututoa chini hadi hapa tulipofikia tunaona mashine za kimaabara zimefungwa,wagonjwa sasa tunawalaza kutokana na vitanda kuwa vingi na vya kutosha,umeme umepatikana ambao ni wa uhakika hata tukisema tunataka kufanya operesheni inafanyika bila wasiwasi labda ukikatika,”anasema.

Aidha anasemakutokana na uwepo huo wa umeme sasa  mashine nyingi zilizoletwa za kiuchunguzi zinatumika kwa sababu ya uwepo wa umeme na kuwarahisishia ufanyaji wa upasuaji kwa urahisi zaidi na kuweza kubaini magonjwa.

“Kituo hiki kilichoanza kujengwa mwaka 2020 na kukamilika 2021 huku 2022 kimeanza rasmi kutoa huduma zake,ni kituo ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo ambao walikuwa wanatembea umbali wa Kilomita tano kufika katika Zahanati nyingine,”anasema na kuongeza

Anasema mwaka 2021 kituo hicho cha afya kilianza kikiwa hakina baadhi ya vifaa pamoja na umeme hali iliyofanya kutolewa kwa huduma chache.”Awali baada ya kukamilika kwa majengo ya kituo hicho tulianza kutoa huduma chache za kawaida kwa wagonjwa wa nje(OPD) ambapo hali hiyo ilitokana na kusaidia wananchi wa maeneo hayo karibu kutopata shida ya kutembea umbali wa  muda mrefu katika kupata matibabu ya kawaida,”anasema 

Anasema mwanzoni hali ilikuwa mbaya kwani  kulikuwa na kituo cha afya cha zahanati moja tu ya Mshikamano ambacho kilikuwa hakiwezi kutibu magonjwa mengi kwa huduma za Kihospitali kama upasuaji ambapo iliwagharimu wananchi kwenda Wilayani Ngara.

“Wananchi walikuwa wanaenda wilayani ngara kupata huduma na ukizingatia ni mbali sana pia gharama za usafiri zilikuwa ni kubwa hadi kufika huko hivyo changamoto kubwa ilikuwa mtu anapopata tatizo mida ya usiku kutokana na kivuko kufungwa mida ya jioni uwalazimu kukodi pikipiki na kuwapeleka,anasema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Maabara cha Kituo hicho cha Afya cha Rusumo, Philimon Mabara anaishukuru NELSAP kwa kujenga kituo hicha afya kupitia LADP na kuhakikisha wamepata vifaa mbalimbali ikiwemo Mashine za kimaabara.

Anasema miongoni mwa mashine hizo ipo ya kutunza damu na Sampuli ambayo awali walikuwa hawana hivyo kuwalazimu kuwataka wagonjwa kwenda kutibiwa katika vituo vingine vya afya.

”Tunashukuru sana kwa kuhakikisha kituo chetu kimekamilika kwa asilimia kubwa na wagonjwa kuwatibia hapa hapa lakini naombi moja la kuwepo kwa jenereta ambalo litakuwa masaa yote tayari pindi umeme unapokatika ili kuweza kunusuru damu kutoharibika,”anasema na kuongeza

”Tumepata mashine nyingi za kupima magonjwa mbalimbali kama moyo,figo,ini na upigaji wa Ultrasound kwa mama wajawazito hii imefanya kituo chetu kutoa hudua bora kwa wananchi waishio rusumo,”anasema.

Kwa Upande wake Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ya Kijamii LADP Irene Chalamila anasema kituo hicho cha afya cha Rusumo kimegharimu kiasi cha Sh. Bilioni 1.5 kwa majengo 13 ikiwemo jengo la Wagonjwa wa Nje(ODP),Maabara,Mionzi,Wamama kujifungua,Kliniki ya Baba ,Mama na Mtoto ,Jengo la Kulazwa la Magonjwa ,Sehemu ya Kufulia Nguo,Jengo la kuhifadhi Maiti pamoja na Nyumba tatu za watumishi wa Kituo hicho.

Anasema hadi kufikia sasa kituo hicho kimekamilika kwa asilimia 100 huku wananchi wakiendelea kupatiwa huduma za kiafya katika kituo hicho ambapo awali walikuwa wakipata Mshikamano au hospitali ya Wilaya ya Ngara ambayo ipo mbali.

”Kwa awamu ya kwanza LADP iliweza kukamilisha baadhi ya majengo na vitu vingine vidogo vidogo ila awamu ya pili ya LADP imeweza kukamilisha asilimia chache iliyobaki kwa kuweka vifaa vya maofisini,kufunga mashine mbalimbali pamoja na kuweka umeme katika kituo hicho lengo ni kutoa huduma bora za afya kwa wananchi waishio rusumo karibu na mradi mkubwa wa nishati ya umeme katika maporomoko ya rusumo,”anasema.

Katabazi Saimon (60)Mmoja wa wagonjwa wanaotibiwa na kituo hicho anasimulia miaka ya nyuma walikuwa wanapata changamoto kubwa ya kupata matibabu kwa hospitali ya karibu.

Anasema hali iliyowafanya kwenda Kituo cha Mshikamano au Hospitali ya Wilaya ambayo ipo umbali wa kilomita sita kufika kwake.”Tulipata shida sana,tunawashukuru NELSAP kwa hatua hii tulikuwa tunalipa kiasi cha sh.10000 kwaajili kupelekwa  hospitali na pikipiki,kiukweli kituo kinatusaidia sana,”anasema.

Anasema wengi wanaenda katika kituo hicho na kupata matibabu yote kama ni upasuaji au matatizo yoyote kwa sasa ni rahisi kupata huduma hapa, kwa kweli tumerudisha kicheko kwa hatua hii,”anasema.

Julieth Abdallah  Mkazi wa Kijiji cha Kumbuga kata ya Rusumo anasema alikuwa anauguliwa na mtoto wake Maralia na kuvimba macho hivyo ilimfanya ampeleke mtoto wake katika kituo hicho kwa lengo la kupatiwa matibabu.

Anasema kwa sasa mtoto wake anaendelea vyema baada ya kupatiwa huduma iliyobora katika kituo hicho cha afya.”Tunashukuru kwa ujenzi wa kituo hiki kimeleta furaha kwa sisi wakazi wa rusumo awali tulikuwa tunapata shida sana sana,”anasema.