NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
UJUMBE
wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
ukiongozwa na mwenyekiti wake, Mhe. Mihayo Juma Nunga umetembelea ofisi za
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) jijini Dar es Salaam kwa nia ya kubainisha
masuala muhimu ya Fidia.
Akizungumza
baada ya kukutana na Watendaji wa WCF wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. John
Mduma, Mwenyekiti huyo amesema ziara hiyo imewawezesha kupata uelewa mpana wa
namna Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inavyotekelezwa na faida ambayo
Watanzania wamepata kutokana na uwepo wa chombo hicho.
“Kwetu
jambo hili ni geni bado halijatengenezewa utaratibu bora zaidi wa kuwalipa
fidia wafanyakazi waliopata changamoto kwenye maeneo ya kazi, Zanzibar tuko
katika maandalizi ya kutengeneza utaratibu wa jinsi gani Mfanyakazi atapata
fidia pindi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, kwahivyo tukaona
tutembelee Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao wana uzoefu mkubwa katika
masuala haya nasi tuweze kuishauri serikali ili tuwe na chombo walau chenye
uwiano na WCF.” Alifafanua Mhe. Nunga.
Alisema
wameona jinsi watu wengi walivyonufaika na uwepo wa WCF kwa hivyo ni wakati
muafaka kwa Zanzibar kuwa na Mfuko utakaotoa huduma bora kama ambavyo
wameshuhudia hapo WCF.
Naye
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw.Ali
Nassor Shaaban, alisema Mfuko huo uko katika maandalizi ya kuanzisha huduma
kama hiyo ya kufidia wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na
kazi.
“Tumeona
kabla ya kuanzisha chombo hicho ni vema kujifunza kwa wenzetu WCF ambao kwa
kweli wamefanikiwa sana ili kujua sheria na kanuni zake zilivyo hatimaye tuwe
katika nafasi nzuri ya kuanzisha chombo chetu kitakachotoa huduma kulingana na
mazingira ya Zanzibar.” Alifafanua.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dtk. John
Mduma ameema , WCF ina uzoefu wa miaka saba (7) katika masuala ya utoaji fidia
kwa wafanyakazi na imekuwa ni wakati mzuri wa kubadilishana mawazo ya namna
bora ya kuendesha vyombo hivi vya Fidia kwa Wafanyakazi.
“Tumewaeleza
namna tunavyotenda katika miaka hii saba (7) na mafanikio tuliyopata,
tumejifunza mambo mengi ambayo wamekuwa wakituuliza na tunaamini wamejifunza
mengi.” Alifafanua.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mihayo Juma Nunga (kushoto), akibadilishana mawazo na Mkurtugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dtk. John Mduma (kulia) na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Bw. Ali Nassor Shaaban wakati wa ziara ya Kamati hiyo na watendaji wa ZSSF kwenye Ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kujifunza jinsi unavyoendesha shughuli zake hususan ulipaji fidia kwa wafanyakzi.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro