October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujue wajibu na majukumu ya wadau wa hifadhi ya jamii

DHANA ya msingi ya sekta ya hifadhi ya amii imejikita katika kuhakikisha kuwa Wananchi wanawezeshwa kuishi maisha yenye staha, kwa kuwawezesha kupata huduma za msingi, hasa pale wanapopata majanga mbalimbali ya kijamii, kama vile uzee, kifo, maradhi, ukosefu wa kazi, uzazi, na matatizo mengine yatakayosabibisha mtu asiweze kufanya shughuli za kuongeza kipato. 

Inapotokea majanga makubwa kama haya, imejidhihirisha wazi kuwa si wananchi wote wanaweza kukabiliana nayo, kwa maana fedha nyingi huwa inahitajika. Hivyo basi, kwa Watanzania hasa wanachama wa mifuko husika wanapata ahueni kwa kuwa wanakua wamejiwekea akiba   kukabiliana na janga lolote, pindi litakapotokea.

Na mifuko inatakiwa kufanya juhudi za makusudi kuhakikisha kuwa wanachama wanapata taarifa za mafao yao kwa uwazi zaidi na hasa kupitia mitandao ya kielektroniki, hususani kupitia simu zao za mikononi hasa kama kwa wakati huu wa ugonjwa na mapavu unaosababishwa na virusi vya corona.

Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kufanya uwekezaji katika miradi mbalimbali kwa malengo ya kulinda thamani ya michango ya wanachama wake, kupata fedha za uendeshaji wa shughuli za mfuko za kila siku, kuweza kuboresha mafao kwa wanachama na kuchangia juhudi za serikali katika kuinuia uchumi wa nchi.

Mafao ya wanachama yanatakiwa kuboreshwa kila mara kwa mara, kulingana na hali halisi ya maisha kwa wakati husika na mahitaji ya wanachama kwa ujumla.

Na jambo muhimu ni kuhakikisha ya kuwa wafanyakazi yaani wanachama wanapata kujua haki na wajibu wao, na pia Mwajiri kujua ni nini hasa anachopaswa kutenda kwa Waajiriwa wake, kuendana na nafasi yake katika sekta ya hifadhi ya jamii.

Hivyo basi, Waajiri wote nchini wanapaswa kutambua kuwa madhumuni hasa ya maelekezo haya ni kuelekeza, kuonesha njia sahihi kwa Waajiri wote nchini, kuhusu sheria za Hifadhi ya Jamii na matakwa yake. 

Hapa maelekezo haya yanapambanua haki na wajibu  kwa wadau wa sekta ya hifadhi ya jamii, kwanza kabisa kwa Serikali, wanachama husika wa Mifuko, Waajiri, pamoja na mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini.

Tukianza na wajibu wa Serikali, pamoja na mambo mengine ni kutunga sera madhubuti ambazo zitalenga katika kuboresha na kuleta maendeleo endelevu ya sekta ya hifadhi ya jamii nchini. 

Lakini pia, Serikali ina jukumu la kutengeneza mpango mkakakati katika kuhakikisha kuwa inapanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi wengi nchini, hususani wale ambao bado hawajafikiwa na sekta ya hifadhi ya jamii. 

Na hili si jukumu la Serikali peke yake, bali hata mifuko ya hifadhi ya jamii na taasisi zingine za watu binafsi kama vile HakiPensheni zinafanya juhudi za makusudi kutoa elimu kwa Wadau wakuu wa Sekta na wananchi kwa ujumla, katika kuona umuhimu wa wao kujiunga na mifuko hii ya hifadhi ya jamii nchini.

Serikali pia ina jukumu lingine la Usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa sera zilizotungwa katika kusimamia sekta nzima ya hifadhi ya jamii, lakini pia kusimamia mikakati iliyojengwa kisheria katika kusimamia sekta nzima kwa ujumla.  

Serikali ina jukumu lingine la msingi kuhakikisha kuwa inatoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa wananchi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kusaidiana na Serikali kuzunguka nchi nzima kuwaelimisha Watanzania wote hususani wale ambao bado hawaoni umuhimu wa kujiunga na mifuko hii ya hifadhi ya jamii, kufanya hivyo mapema kabla ya kuja kujutia baadae pindi majanga yanapowakuta.

Pia, maelekezo haya kwa Waajiri katika sekta ya hifadhi ya jamii, pia yanatoa wajibu na haki ya wafanyakazi na wananchi wote kwa ujumla. 

Hapa ndipo inaposisitiza ya kuwa kila mwananchi nchini, ana haki ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, na hivyo kupata wasaa wa kupata mafao mbalimbali ambayo huko mbeleni yatakuwa ni ya manufaa makubwa kwao. 

Maelekezo haya yanaenda mbele zaidi kutoa elekezo kuwa kila mwanachama ana wajibu ufuatao;

Kwanza, kuhakikisha kuwa kila mwanachama wa Mfuko husika kuangalia na kufuatilia kwa makini mtiririko wa michango yake katika akaunti yake. 

Hapa, maana yake ni kwamba, kila baada ya muda fulani, inapendekezwa kuwa mwanachama awe anafuatilia kama michango yake na ya mwajiri, inawekwa kwa kuzingatia muda uliowekwa kisheria, lakini pia kuhakikisha kama michango inayowekwa ni sahihi, na kuwa hakuna mapunjo ya aina yoyote kutoka kwa mwajiri, ama Mfuko husika.

Wanachama wa mifuko husika ya hifadhi ya jamii, wanatakiwa kuhakikishiwa ya kuwa wanapata namba ya usajili ya Mfuko wanaojiunga nao.  Na hili ni jambo la msingi sana kwa upande wa  mwanachama, maana ni kwa kupitia namba hii maalumu, ambayo hutolewa na Mifuko husika, kupitia kadi maalumu ya Mifuko, ndipo mwanachama anapata huduma ya kujua mwendelezo wa michango katika akaunti yake, pamoja na huduma nyingine zozote muhimu ambazo wanachama angependa kujua yeye binafsi.

Pia mwanachama, mwisho wa siku analindwa pia na elekezo hili, pale ambapo anahakikishiwa kwa mujibu wa sheria kupata mafao yake pindi tu anapostaafu.  Na utaratibu wa kupata mafao yake, umeanishwa vizuri katika sheria za kila Mifuko husika.

Mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ina wajibu wa kuhakikisha ya kuwa wanasimamia katika ukamilifu wake mambo yafuatayo ya msingi;

Kwanza, ni kuhakikisha kuwa inawaandikisha Waajiri na Waajiriwa kwa mujibu wa sheria za nchi

Lakini pia, mifuko ya hifadhi ya jamii ina wajibu wa kukusanya michango ya waajiri wote waliosajiliwa katika Mifuko husika, ili kupata takwimu sahihi za michango ya wanachama na Waajiri wao. 

Ni kwa kufanya hivyo, ndipo Mifuko husikia inajua idadi kamili ya michango ya wanachama wao, na hivyo basi kuamua mipango yao ya uwekezaji waielekeze katika vipaumbele vipi.

Pia mifuko hii inatakiwa kufuata kanuni za usalama wa mtaji, uwezo wa kuleta faida, uwezo wa kitega uchumi kubadilika kuwa fedha taslimu, kuchangia masuala ya kijamii, na kutawanya uwekezaji.

Na kuhakikisha ya kuwa sera za uwekezaji za mifuko zinafanyiwa marekebisho ya mara kwa mara ili ziendane na mabadiliko ya uchumi ndani na nje ya nchi.

Kwa kuzingatia kanuni mifuko inatakiwa kuwekekeza katika maeneo tofauti kwa viwango tofauti kulingana na sera ya uwekezaji kama vile kwenye dhamana za kiserikali, akiba ya muda maalumu, miradi ya ujenzi, hisa kwenye makampuni, mikopo kwa makampuni, dhamana za makampuni na hisa kwenye soko la mtaji.