November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujue Mfuko wa Barabara na Bodi yake

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online

Katika kuhakikisha kuwa kuna kuwa na fedha endelevu za kugharamia matengenezo ya barabara nchini, serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa Barabara na Bodi yake (Roads Fund Board).

Mfuko wa Barabara na Bodi yake (Roads Fund Board), vilianza kufanya kazi mwaka 2000, kupitia Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta Sura 220.Ambapo mfuko na bodi vilianzishwa kama sehemu ya mabadiliko (reforms) yaliyofanywa na Serikali kwenye sekta ya barabara.

Na ulianzishwa ili kuhakikisha kuna kuwa na fedha endelevu za kugharamia matengenezo ya barabara za Kitaifa ambazo ni barabara kuu na barabara za mikoa pamoja barabara za Wilaya kama zilivyoainishwa kwenye Sheria ya Barabara Namba 13 ya Mwaka 2007 ambapo Sheria hiyo inazihusu barabara zilizopo Tanzania Bara.

Azimio la kwanza la uanzishwaji wa mfuko liliitwa”azimio la kuanzisha mfuko maalum wa fedha za barabara au mfuko wa barabara”lilifanyika mnano Agousti 1991, na azimio la pili liliitwa “azimio la kuanzisha mfuko wa barabara wa serikali za mitaa ambalo lilifanyika Agousti 1992. Uanzishwaji wa Mfuko wa Barabara ulilenga matengenezo ya barabara kuu pamoja na matengenezo ya barabara za mijini na vijijini.

Kuanzishwa kwa tozo katika mafuta ya dizeli na petroli katika Ibara ya 17 ya Sheria ya Hazina na Ukaguzi (sura ya 439) ambayo inaipa mamlaka Serikali kuanzisha mfuko maalum hivyo kutokana na taratibu za utawala azimio hilo halikuwa na nguvu ya kisheria hivyo hakukuwa na uwajibika katika azimio hilo.

Ili kuupa mfuko nguvu ya kisheria na kupata nguvu katika kufadhili matengenezo ya barabara na usimamizi wa mfuko, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho ya sheria za Barabara (Namba 2) ya mwaka 1998 ambayo ilianzisha Mfuko wa Barabara na Bodi ya Mfuko wa Barabara.

Ambapo mwaka 2006 sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na inatumika kama sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta Sura 220 (iliyofanyiwa marekebisho 2006).

Bodi ilianza kufanya kazi mwaka 2000 katika jengo la TETEX Barabara ya Pamba Dar-es-Salaam huku Mwenyekiti wake wa kwanza akiwa Rose Mangenya, Philipo A.Magani aliefuatiwa na Dkt. James Wanyancha na Mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Mfuko wa Barabara ni Joseph Haule.

Majukumu ya Bodi ya Mfuko wa BarabaraMajukumu ya Bodi ya Mfuko wa BarabaraKutokana na kifungu cha 5(4) cha Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta, Sura ya 220, majukumu yake makuu ni pamoja na kumshauri Waziri mwenye dhamana ya barabara juu ya vyanzo vipya vya mapato ya mfuko.

Marekebisho ya viwango vya vyanzo vilivyopo na kanuni za ukusanyaji wa mapato ya mfuko kwa dhumuni la kuhakikisha uwepo wa mapato ya kutosha na endelevu kwa ajili ya shughuli za barabara.

Kutumia fedha za mfuko kwa makusudi yaliyoidhinishwa na Bunge, kuweka na kutoa utaratibu utakaotumiwa na wakala wa ukusanyaji mapato ya mfuko. Pia kuhakikisha kuwa mapato yote yamekusanywa na kupelekwa kwenye akaunti ya mfuko, kutengeneza au kurekebisha utaratibu wa ugawaji wa fedha za mfuko na kumshauri Waziri mwenye dhamana ya barabara kuhusu utaratibu huo.

Sanjari na hayo pia majukumu mengine ni pamoja na kumshauri Waziri mwenye dhamana ya barabara juu ya ugawaji wenye ufanisi wa fedha za mfuko, kugawa fedha za mfuko kwa Wakala wa Barabara.

Vile vile kuhakikisha kuwa shughuli za kiufundi na kifedha za Wakala wa Barabara na mfuko wenyewe zinafanyika kwa ufanisi mkubwa, kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa Wakala wa Barabara ili kuhakikisha kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kutoa mapendekezo mengine yoyote kwa Waziri wa barabara yatakayoonekana ni muhimu ili kuiwezesha bodi kutimiza malengo yake.

Vyanzo vya mapato ya Mfuko wa BarabaraVyanzo vya mapato ya Mfuko wa Barabara ni pamoja na tozo ya mafuta ambayo ni chanzo kikuu cha mapato kwani huchangia wastani wa asilimia 97 ya mapato yote ya mfuko huo.

Tozo ya mafuta ambayo ni shilingi 263 kwa kila lita ya petroli na dizeli,mapato yake hukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuongezeka kwa mapato kutoka chanzo hiki kunategemea zaidi kukua kwa sekta za kiuchumi ambazo hutegemea zaidi matumizi ya nishati za dizeli na petroli.

Huku ushuru kwa magari ya kigeni yanayoingia nchini, kwa wastani unachangia asilimia moja ya mapato ya mfuko ambapo mapato kutoka kwenye chanzo hiki yanategemea zaidi hali ya usalama nchini, ufanisi wa bandari na ubora wa barabara zetu.

Chanzo kingine ni fedha zipatikanazo kupitia magari yanayozidisha uzito barabarani (overloading charges), kwa mujibu wa Sheria ya Afrika Mashariki ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya mwaka 2016.

Mfuko haukichikulii kama chanzo endelevu kwa kuwa kimewekwa ili kudhibiti uzidishaji wa mizigo kwa magari yanapokuwa barabarani.

Hivyo mapato yake yanatarajiwa kushuka kadri wasafirishaji watakavyozidi kufuata sheria hiyo, lengo la chanzo hicho ni kufidia uharibifu halisi wa miundombinu ya barabara uliosababishwa na chombo husika cha usafiri au usafirishaji.

Ufanisi wa Mfuko wa BarabaraIli kuongeza ufanisi kwenye ufuatiliaji wa matengenezo na hali ya barabara, katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita, Bodi ya Mfuko wa Barabara imeunda mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji hali ya barabara. Mfumo huo ulizinduliwa rasmi Julai 2022 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya katika warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara iliyofanyika jijini Mwanza.

Naibu Waziri huyo aliiagiza bodi hiyo kufuatilia na kuhakikisha taarifa na malalamiko yanayotolewa na watumiaji wa barabara kupitia mfumo huo mpya wa ufuatiliaji wa hali ya barabara yanafanyiwa kazi kwa wakati na Wakala wa Barabara wanaohusika na utengenezaji wa barabara hizo ambao ni TANROADS na TARURA.

“Upatikanaji wa taarifa za hali ya barabara kwa wakati ni moja ya njia muhimu za kutunza miundombinu ya barabara,naipongeza bodi kwa kubuni mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na wananchi na watumia barabara katika kufuatilia na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya hali ya barabara katika maeneo yao,”anaeleza Mhandisi Kasekenya.

Meneja wa Mfuko wa Barabara Eliud Nyauhenga anaeleza kuwa kwa zaidi ya kipindi cha miaka 20 iliyopita Tanzania imeshuhudia uharibifu mkubwa wa mara kwa mara wa miundombinu ya barabara kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Nyauhenga anaeleza kuwa uharibifu huo ni pamoja na kusombwa kwa madaraja na makalavati kunakoleta usumbufu na hasara kubwa kwa wasafiri na wasafirishaji na kuisababishia Serikali gharama kubwa za matengenezo.

“Mfano wa karibuni ni kuzolewa kwa daraja la Kiyegeya mwaka 2020 ambako kulisimamisha kwa muda shughuli za usafiri na usafirishaji kupitia barabara ya Morogoro-Dodoma ambayo inatumiwa na mikoa ya kati, Kanda ya Ziwa na nchi jirani kama Rwanda, DRC Congo na Burundi, kutokana na kusombwa kwa daraja hilo, Serikali ililazimika kutumia takribani bilioni 10.89 kujenga daraja jipya na barabara unganishi,” anaeleza Nyauhenga.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi Ufundi kutoka Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga aliwaambia waandishi wa habari kuwa lengo la mfumo mpya wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara ni kuwashirikisha wananchi na hasa watumiaji wa barabara katika kusimamia na kutunza miundombinu ya barabara.Hali itakayosaidia kuepusha uharibifu wa miundombinu ya barabara unaoweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

Mhandisi Kalimbaga anaeleza kuwa kupitia mfumo huo, taarifa za hali ya barabara kutoka kwa watumiaji wa barabara zitapelekwa kwa mameneja wa TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na hatimaye kupeleka mrejesho kwa watoa taarifa.

Matumizi ya Mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabaraTakwimu zinaonesha kuwa tangu Julai hadi Octoba 2022 baada ya kuanza kwa matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara tayari malalamiko 7308 yamepokelewa kati ya hayo malalamiko 1526 ni kuhusu kuharibika kwa barabara.

Malalamiko 953 ni kuhusu mashimo barabarani, malalamiko 678 ni kuhusu kukosekana kwa alama za barabarani, malalamiko 649 ni kuhusu uchafu kwenye mifereji, malalamiko 408 ni kuhusu kuvunjika kwa kalavati pamoja na malalamiko ya aina nyingine.

Hivi sasa wananchi wanaweza kutumia simu-janja (smart phones) kwa kupakua mfumo mpya wa barabara na kutoa taarifa za hali ya barabara au simu za kitochi kutoa taarifa ya hali ya barabara kwa kubofya *152*00# na kufuata maelekezo.

Gharama za kutuma taarifa kwa wanaotumia simu za kitochi au kishikwambi ni bure na wanaotumia simu-janja wenye mitandao ya Airtel na Vodacom kupitia mfumo wa Barabara, wanaweza kutumia mfumo huo bila ya kuwa na kifurushi cha mtandao. Aidha, mazungumzo yanaendelea ili matumizi ya mfumo wa barabara bila gharama kwa simu-janja yawezeshwe kwa watumiaji wa mitandao mingine.

Kutumika kwa wataalamu wa ndani na wataalamu washauri katika mfumo huo Mfuko wa Barabara hutumia wataalamu wake wa ndani pamoja na wataalamu washauri katika kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS na TARURA) kwa ajili ya matengenezo ya barabara zinatumika ipasavyo.

Ambapo wataalam hao huzungukia miradi iliyopokea fedha za matengenezo ya barabara ili kujiridhisha kuwa thamani ya fedha iliyotolewa inaendana na matengenezo ya barabara yaliyofanyika.

Mwananchi azungumzia mfumo wa ufuatiliaji wa hali ya barabara Kwa upande wake Joshua Mkelemi ambae ni mkazi wa Dodoma ameipongeza serikali kwa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa hali ya barabara kwa unawaweka watoa huduma za barabara na wananchi karibu. Hivyo inakuwa rahisi kwa wananchi kutoa malalamiko yao kwa watoa huduma moja kwa moja, ambapo nao wanatakiwa kuyafanyia kazi malalamiko hayo kwa wakati ili kuboresha zaidi huduma ya barabara nchini.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya akisalimiana na Meneja wa Mfuko wa Barabara Eliud Nyauhenga, wakati akiwasili kwenye warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kwenye miundombinu ya barabara jijini Mwanza,huku mwenye kitambaa kichwani ni Katibu Mkuu Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Joseph Haule wa kwanza kushoto.
Muonekano wa daraja jipya la Kiyegeya linalounganisha mikoa ya Morogoro na Dodoma, lililojengwa na Serikali kwa kutumia fedha za matengenezo ya dharura kutoka Mfuko wa Barabara, baada ya daraja la zamani kusombwa na mafuriko ya mvua.
Barabara ya Waziri Mkuu iliyojengwa kama njia mbadala baada ya barabara ya njia panda ya Area D kufungwa.