December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujio viongozi wa kimataifa matokeo ya uongozi thabiti wa Rais Samia

Na Amani Abdallah,TimesmajiraOnline, Dodoma

“DIPLOMASIA ya Tanzania imezidi kung’ara kimataifa.” Hiyo ndiyo lugha rahisi ambayo Mtanzania yoyote anaweza kutumia kueleza mafanikio makubwa ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha ushirikiano mataifa mengine.

Ziara mbalimbali zinazofanywa na viongozi nchini kuanzia wale wanaotoka mataifa kubwa duniani yakiongozwa na Marekani hadi wale wanaotoka nchini zinazoendelea ni kielelezo kwamba diplomasia ya Tanzania inazidi kung’ara.

Ujio wa ziara za viongozi hao tangu Rais Samia ashike uongozi Machi 19, mwaka 2021 hadi sasa umeleta neema na kufungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii, huku zikizalisha ajira nyingi.

Lakini pia, mwaka huu wa 2024 nao umekuwa wa neema kwani viongozi wakuu kutoka mataifa mbalimbali wanazidi kufanya ziara nchini kwa lengo la kuimarisha na kudumisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na mataifa hayo.

Hiyo inawekwa waza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na viongozi wakuu wa kitaifa wataofanya ziara nchini mwezi huu na mwanzo mwa mwezi wa pili,2024.

Akielezea ziara za viongozi hao nchini Waziri Makamba amesema 22 (juzi) amewasili Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China na Mjumbe wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China, Liu Guozhong ambaye atakuwa nchini hadi leo, Januari 24, 2024.

Mara baada ya kuwasili kiongozi huyo alikuwa na mazungumzo na Rais Samia, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa npamoja na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko.

Anasema kiongozi mwingine mkuu anayetarajiwa kuwasili nchini ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes Mesa, ambaye atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia Januari 23 (jana) hadi 25, 2024.

Pamoja na mambo mengine, ziara hiyo imelenga kuendelea kudumisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Cuba.

Waziri Makamba, amesema, Mesa anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais Samia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Rais wa Zanzibar, Dkt. Husein Ali Mwinyi na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson.

Pamoja na mambo mengine, Mesa atamtembelea Mjane wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere na kushiriki mkutano wa wanachama wa urafiki kati ya Tanzania na Cuba, Watanzania waliosoma Cuba na Taasisi ya Pan African Movement na kutembelea kiwanda kinachozalisha dawa za viuadudu ya Biolarvicide cha Kibaha, Pwani.

Kiongozi mwingine anayetarajiwa kuwasili nchini ni Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda atakayewasili nchini kwa ziara ya kikazi Februali 8 hadi 9, 2024.

Akiwa nchini, Cuda atakutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia, ambapo lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Poland.

Anasema Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji, usimamizi wa mazingira, utalii, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.

Aidha, ziara hiyo inatarajia kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika maeneo ya ulinzi na usalama, nishati na gesi, madini, usafiri, ulinzi wa mitandao, utamaduni na uchumi wa buluu.

Mbali na viongozi wakuu wa mataifa tajwa kufanya ziara nchini, Rais Samia, atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia Januari 24 – 26, 2024 kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Joko Widodo.

Ziara hiyo ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya nchini Tanzania Agosti, 2023.

Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Liu Guozhong akiwa ameambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko mara baada ya kuwasili nchini kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia Januari 22 hadi 24, 2024.

“Ziara hii inalenga kukukuza na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Indonesia kupitia sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji, kilimo, nishati, madini, mifugo, uvuvi, uchumi wa buluu, elimu, utalii na ulinzi,” anaongeza Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba anasema Rais Samia Suluhu anatarajia pia kufanya Ziara ya Kitaifa Vatican Februali 11 – 12, 2024 kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Francis.

Waziri Makamba ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.

Uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini.

Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya.

Kwenye ziara hiyo, Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo.

Aidha, Makamba anasema Rais Samia, atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway, Februari 13-14, 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja.

Ameongeza kuwa ziara hiyo inafanyika ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Norway.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Norway akiwemo Mfalme Herald. Pamoja na mambo mengine, Rais pia atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Norway pamoja na Kongamano la Nishati la Oslo,” alisema Waziri Makamba

Tanzania na Norway zinashirikiana kupitia sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, nishati kama mafuta na gesi, elimu na masuala ya kodi na utawala bora.

Kuanzia mwaka 2010, Serikali ya Norway imekua ikishirikiana na Tanzania kwenye programu mbalimbali za maendeleo zilizo gharimu takribani sh. bilioni 300.

Programu hizo zimesaidia na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Nishati; Sekta ya Elimu; Sekta ya Mafuta na Gesi; Mpango wa Usimamizi wa Fedha za Umma; programu za Mabadiliko ya Tabianchi; na programu za Usimamizi wa Misitu.

Rais Samia Suluhu Hassan anaandika historia kupitia ziara hii nchini humo kwani mara ya mwisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutembelea nchi hiyo kwa Ziara ya Kitaifa ilikua mwaka 1976.

Ziara za viongozi hao nchini na zile ambazo zitafanywa na Rais Samia ni fursa kubwa, hivyo Tanzania, inatakiwa kutumia vizuri fursa za wageni wa kimataifa nchini kuzidi kujiimarisha kiuchumi.

Wasomi waliozungumza na gazeti hili kuhusu ziara za viongozi hao watatu kutoka China, Cuba na Poland, kuitembelea Tanzania ni suala linalo thibitisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na mataifa ya kigeni.

Mchumi Paul Endrew, anaamini kwamba ziara hizo zitaitletea manufaa ya Tanzania, hivyo viongozi wa serikali wanapaswa kujenga mahusiano mazuri.

“Kuna haja kwa Serikali na viongozi walio karibu na Rais Samia kujenga mahusiano na wale viongozi waandamizi ambao viongozi hao watafuatana nao,”anasema Endrew.

“Tuna matumaini makubwa kwamba ziara hii zitafungua fursa kubwa sana za masoko na kutasainiwa mikataba kwa ajili ya kukuza mahusiano katika sekta ambazo tunafikiria tunaweza kupata faida kubwa,” anasema.

Naye Amon Joanes amesema endapo yale yatakakayokubaliana viongozi hao kupitia ziara zao yatatekelezwa itakuwa ni mwendelezo wa mafanikio makubwa ambayo yanazidi kupatikana chini ya uongozi wa Samia.

***Ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes
Mesa

Ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes, inakuja huku kukikuwa na kumbukumbu ya ahadi ya nchi hizo mbili
(Tanzania na Cuba) kuahidi kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika nyanja za afya (chanjo), biashara na uwekezaji, uzalishaji wa mbolea na kilimo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akisalimia na Makamu wa Rais wa Cuba, Salvado Valdés Mesa yaliyofanyika Machi 1, 2023 katika Mji wa Baku nchini Azerbaijan. jana kiongozi huyo aliwasili nchini kwa ziara yake nchini ikiwa ni matunda ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali.

Ahadi hiyo imetolewa katika kikao baina ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na Balozi wa Cuba, Yordenis Despaigne Vera katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam mwaka jana.

Kuanzishwa kwa maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba kulikusudia kuimarisha ushirikiano uliodumu kwa takribani miaka 60 pamoja na kunufaisha wananchi wa mataifa yote mawili kiuchumi.

Mbali na maeneo mapya ya ushirikiano, Tanzania imekuwa ikishirikiana na Cuba katika sekta za afya, elimu, utalii, ulinzi na viwanda.

Uhusiano huo wa Tanzania na Cuba umekuwa imara tangu ulipooasisiwa na viongozi wakuu wa Mataifa hayo, Hayati Fidel Castor na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kupitia mazungumzo ya viongozi hao, Cuba iliahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha misingi ya kidiplomasia kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.

Kufuatia ahadi hiyo watanzania wanaimani kuwa ziara ya makamu Rais wa Cuba itazidi kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha unakuwa na mafanikio ya kiuchumi kwa manufaa ya mataifa yote mawili,” aliongeza Balozi Vera. Tanzania ilianzisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Cuba mwaka 1963.

***Ziara ya Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China, Liu Guozhong

Ziara ya Guozhong inakuja wakati Tanzania wakiwa na kumkumbu ya mazungumzo ya Rais Samia chini na Rais Xi Jinping wa China walipokutana wakati wa Mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Johannesburg.

Rais Xi alidokeza kuwa ziara ya Rais Samia nchini China ilikuwa na mafanikio na ilikuja wakati muhimu katika uhusiano kati ya China na Tanzania.

Makubaliano mbalimbali waliyofikia yanatekelezwa kikamilifu na kwa ufanisi. Ushirikiano kati ya China na Tanzania siku zote umekuwa mbele zaidi katika ushirikiano kati ya China na Afrika, na Reli ya TAZARA ni kumbukumbu nzuri ya watu wa nchi hizo mbili.

China zina zaidi ya miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi, ndiyo maana China ina nia ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kupitia fursa hii.

Wakati wa mazungumzo yao, Rais Samia alifurahi kutembelea China na kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hadi kuwa ushirikiano wa kimkakati na Rais Xi Jinping.

Anasema Tanzania na China zimedumisha mawasiliano ya karibu katika ngazi zote, na miradi ya ushirikiano inaendelea vizuri. “Tanzania inathamini sana misaada na uungaji mkono wa China kwa maendeleo ya nchi zinazoendelea,” alisema Rais Samia.

Aliongea kuwa Tanzania na nchi nyingine zinazoendelea zimenufaika sana na ujenzi wa pamoja wa pendekezo la “Ukanda Mmoja na Njia Moja” lililotolewa na Rais Xi Jinping.

Tangu wakati wa ziara ya Rais Samia nchini China, Tanzania ilitarajia kuongeza zaidi kiwango cha maendeleo ya uhusiano kati ya Tanzania na China kupitia fursa ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi na China.

***Rais wa Jamhuri ya Poland, Andrzej Duda

Ziara hii itamkutanisha na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu kwa lengo la kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili.

Tanzania na Poland zinashirikiana katika miradi ya maendeleo ya miundombinu, uhifadhi wa wanyama pori, elimu, maji na usimamizi wa mazingira, utalii, biashara na uwekezaji na ushirikiano wa mabunge.

Balozi Buzalski alipotembelea maeneo ya miradi ya maendeleo ya Ubalozi wa Poland nchini Tanzania.

Eneo la Udzungwa na Bonde la Kilombero, ni sehemu ya ruzuku ndogo zinazofadhiliwa ndani ya Msaada wa Kipoland, Ubalozi wa Jamhuri ya Poland jijini Dar es Salaam umekuwa ukisaidia kwa miaka kadhaa shughuli za shirika lisilo la kiserikali la STEP kulinda bioanuwai ya Tanzania na kufikia hali ambapo watu na wanyamapori wanaweza kuishi pamoja bila migogoro.

Likiwa kati ya Hifadhi ya Kitaifa ya Milima ya Udzungwa na Hifadhi ya Kitaifa ya Nyerere, Bonde la Kilombero lina watu wengi na lina rutuba nyingi.

Eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa ustawi wa kiikolojia wa kusini mwa Tanzania.

Mwaka 2022, Ubalozi wa Jamhuri ya Poland jijini Dar es Salaam uliendelea kusaidia shughuli za STEP zenye lengo la kuhakikisha kuwepo kwa amani kati ya binadamu na tembo katika Bonde la Kilombero.