Judith Ferdinand na Seleiman Abeid, Timesmajira Online, Mwanza
Ujenzi wa meli mpya ya MV.Mwanza,umefikia asilimia 98,huku ukielezwa kuwa utaenda kuboresha huduma ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria ndani ya Ziwa Victoria pamoja na kuunganisha nchi jirani za Kenya na Uganda.
Huku rai ikitolewa kwa wataalam kuhakikisha meli hiyo inadumu muda mrefu kwani itakuwa haina maana kama viongozi wamewezesha maono makubwa kutokea halafu baada ya muda mfupi ikaharibika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali,Gerson Msigwa ameyasema hayo,Mei 02, 2025, wakati wa ziara yake na Waandishi wa Habari wa mkoa wa Mwanza na Shinyanga kwenye ziara ya kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Msigwa amesema kuwa, ujenzi wa meli hiyo ni uwekezaji utakaoleta uhakika wa kukua kwa uchumi wa nchi kwani wananchi wataweza kunufaika na fursa za nchi jirani pamoja na kufungua nyingine.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Neema Mwale, amesema meli hiyo,atakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori 3.
Amesema,meli hiyo inatarajiwa kufanya safari zake kati ya Mwanza, Musoma, Bukoba kupitia bandari ya Kemondo Bay na nchi jirani za Uganda na Kenya.
“Gharama za utekelezaji wa mradi huu hadi kukamilika kwake zitakuwa ni jumla ya bilioni 139, kwa sasa mradi huu umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake,unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 31, 2025,”amesema Neema.
More Stories
AAFP yampitisha Ngombare Mwiru kugombea Urais Bara
DC Mpogolo:DMDP kujenga barabara za urefu km 67 Ilala
Uhakiki na uchambuzi wa kazi za waandishi wa tuzo za Samia Award wafanyika kwa weledi