Na Judith Ferdinand, Mwanza
Mwaka 2022, Serikali ilitoa kiasi cha bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 nchi nzima kwa shule za sekondari zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka mpya wa masomo wa 2023.
Ujenzi wa vyumba hivyo umetokana na Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inayoainisha kuwa Serikali itahakikisha kuwepo kwa miundombinu bora na ya kutosheleza mahitaji ya elimu na mafunzo kwa makundi yote katika ngazi za elimu na mafunzo.
Pia kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na kuwapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia ujenzi wa madarasa.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ni moja ya halmashauri ambayo ilipatiwa fedha kiasi cha bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 pamoja na samani zake kwa maana ya viti na meza 5,500 na ofisi tatu ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwaka kwa mwaka mpya wa masomo wa 2023.
Wakati fedha hizo zinatolewa, halmashauri hiyo ilikuwa na uhitaji wa vyumba vya madarasa kwa kidato cha kwanza 252, vilivyokuwepo ni 142 hivyo upungufu ukiwa ni vyumba 110.
Hali ilivyo kwa sasa
Hadi kufikia Desemba 21, mwaka 2022 tayari vyumba 110 vilikuwa vimekamilika na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima.
Mkurungezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela azungumzia ujenzi wa madarasa hayo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa madarasa 110, katika hafla ya makabidhiano ya madarasa hayo iliofanyika shule ya sekondari Bujingwa,wilayani Ilemela mkoani Mwanza Desemba 22,2022.
Anaeleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipokea kiasi cha bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 katika shule za sekondari 23, pamoja na seti za meza na viti 5,500 na ofisi tatu.
Huku lengo ni kuwezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023, kupata nafasi na kuanza masomo kwa wakati pamoja na kuwa na mazingira bora ya kujifunza na kujifunzia.
Mahitaji ya vyumba vya madarasa
Mhandisi Apolinary anaeleza kuwa mahitaji ya vyumba vya madarasa ya kidato cha kwanza mwaka 2023 ni madarasa 252 kwa ajili ya wanafunzi 12,548 kati yao wasichana 6537 na wavulana 6011 huku vyumba vya madarasa vilivyokuwepo ni 142 na upungufu ni 110.
Ushiriki wa jamii katika mradi huo
Mhandisi Modest, anaeleza kuwa jamii pia ilishiriki katika mradi huo kwa kusaidia kutoa viashiria na nguvu kazi ambavyo vinakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya milioni 12, kama ishara ya kuunga juhudi ya serikali yao.
Mafanikio ya mradi huo.
Anaeleza kuwa kupitia mradi huo waliweza kutoa ajira fupi kwa wananchi,1412, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,kuwezesha serikali kupata kodi kutoka kwa mafundi na wazabuni waliouza vifaa vyao katika ujenzi huo huku jamii ikipata ujuzi wa namna bora wa kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Changamoto katika mradi huo
Mhandisi Modest, anaeleza kuwa katika kipindi cha kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba 110 vya madarasa,wamekutana na changamoto ya kupanda kwa bei ya vifaa ghafla,kukatika kwa umeme na hupatikanaji wa maji,utatuzi wa migogoro ambapo ushirikishaji wa jamii ulisaidia hususani suala la upatikanaji wa maji kwa ajili ya ujenzi.
Ambapo hadi Desemba 21,2022 shule zote zilizopokea fedha katika halmasahauri hiyo zilikuwa zimekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 vyenye seti ya viti na meza 5,500.
Hivyo hali ambayo imesaidia Januari 9,2023 shule zilivyofunguliwa kila mwananfuzni wa kidato cha kwanza aliyeripoti shule katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kukutana na mazingira bora ya kujifunza.
Baada ya shule kufunguliwa Timesmajira online ilipata fursa ya kutembelea shule ya sekondari Bujingwa iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kuzungumza na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,wanafunzi na wazazi juu ya ujenzi huo wa vyumba vya madarasa.
Mkuu wa shule ya Sekondari Bujingwa azungumzia ujenzi wa vyumba vya madarasa 8 katika shule yake kwa ajili kidato cha kwanza mwaka 2023
Mkuu wa shule ya sekondari Bujingwa iliopo Kata ya Buswelu Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Magweiga Magabe,akizungumza na Timesmajira online,Januari 11,2023 ofisini kwake wilayani Ilemela mkoani hapa,anaeleza kuwa mwaka 2022, shule hiyo ilipokea fedha kwa ajili ya maadalizi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa 2023.
“Tulipokea kiasi cha milioni 160,kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8,tunamshukuru Mungu tulifanikiwa kujenga vymba hivyo vya madarasa ambayo ndani yake tumeweka seti ya viti na meza 400,ambapo kila darasa kuna seti ya viti na meza 50,”anaeleza Mwalimu Magabe.
Faida ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 8
Mwl.Magabe anaeleza kuwa ujenzi huo wa madarasa hayo imesaidia kuaondoa mrundikano kwa wanafunzi hao wa kidato cha kwanza kwa sababu ya uwiano wa viti na meza 50 kwa kila darasa ambao utafanya kuwa kila chumba cha darasa kuwa na wananfunzi 50.
“Uwiano wa zamani wa vyumba vya madarasa na wanafunzi ulikuwa kila chumba kimoja cha darasa moja ni wananfunzi 70 hadi 75,ila sasa ni wanafunzi 50,hapo nyuma mtihani ulikuwa ni mkubwa licha ya kwamba suala kukabana na wazazi juu ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa haikuwa kwetu sisi walimu bali ni kwa viongozi ngazi ya mtaa, kata na Wilaya ya kuona namna gani wanachanga,”.
Ambapo hali hiyo ilikuwa ni ngumu sana kwa sababu Januari watoto walikuwa wanatakiwa kuanza masomo lakini madarasa yanakuja kukamilika mwezi Machi hadi Mei hivyo kufanya mrundikano kuwa mkubwa pia kulikuwa na changamoto ya viti na meza kwa ajili ya kukalia wananfunzi.
“Maana wazazi walijikuta wanakuwa na mzigo mkubwa kwani mzazi huyo huyo achangie ujenzi wa darasa pia achange kwa ajili ya viti na meza,hivyo hiyo ilikuwa ni wakati mgumu hata watoto wote kuanza nao masomo kwa wakati mmoja lakini sasa hivi madarasa yapo wazi yanawasubili watoto kuingia,”anaeleza Mwl.Magabe.
Anaeleza kuwa serikali kupitia ujenzi huo wa vyumba vya madarasa imewapunguzia adha kubwa wazazi,walimu na wanafunzi kwani imeboresha sehemu kubwa na wanayo Amani kuwa mtoto anapofika shuleni anaingia darasani na kuanza masomo.
“Ukifuatilia historia ya shule yetu hapo nyuma kwa mwaka juzi kurudi nyuma ufaulu haukuwa mzuri sana,lakini kuanzia mwaka jana tukiangalia matokeo ya kidato cha pili watoto wamefanya vizuri licha ya wao kuwa wengi kwa sababu ya mazingira kuwa bora ambapo kuna daraja la kwanza (division one) 25,daraja la pili 25,daraja la tatu waliofeli ni wanafunzi 14,ukiangalia nyuma waliokuwa wanafeli ni wengi,”.
Hii inaonesha kuwa wanafunzi wanapata hamasa ya kusoma kutokana na mazingira ya shule kuwa vizuri na walimu wanafanya kazi kwa bidi kwa sababu miundombinu ipo vizuri, shule ina walimu 44 ambapo bado hawajapata walimu wa kutosheleza katika masomo ya sayansi ingawa ukosefu wa walimu wakutosha kwa masomo ya sayansi ni changamoto ya kitaifa.
Idadi ya wananfunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 waliopangwa katika shule hiyo.
Mwalimu Magabe anaeleza kuwa kwa mwaka mpya wa masomo shule hiyo imepangiwa jumla ya wanafunzi 555 wa kidato cha kwanza kati yao wavulana 294 huku wasichana wakiwa 261.
“Tunamshukuru Rais Samia na viongozi wote wanaomsaidai kwa kweli madarasa haya ni msaada mkubwa kwa shule yetu na jamii kwa ujumla, kwa sababu watoto 555 tunge kwama sana bila ya kuwa na vyumba hivi nane ambavyo ni vipya, kwa sasa tunawapokea wananfunzi wote bila changamoto yoyote kwani kuna viti vya kukalia na meza na madarasa mazuri,”anaeleza Mwalimu Magabe.
Idadi ya wanafunzi walioripoti shuleni mpaka Januari 11,2023
Mwalimu Magabe anaeleza kuwa mapaka Januari 11,2023 shule hiyo imeisha pokea wanafunzi 252 wa kidato cha kwanza walioripoti shuleni hapo kati yao wavulana 130 huku wasichana 122, tayari wameisha sajiliwa shuleni na wanaendelea na masomo.
Nini utaratibu wa shule kwa kidato cha kwanza kuripoti shuleni
Mwalimu Mkuu huyo anaeleza kuwa shule ilijipangia utaratibu wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti mapema shule kabla ya Januari 9,mwaka huu ili siku hii waanze masomo rasmi lakini wengi wao hawjaripoti na unaweza kukuta kati yao pia walichelewa kuchukua fomu ya kujiunga na kidato cha kwanza.
“Tuliwaambia Januari 5 na 6 mwaka huu waanze kuripoti shule na kusajiliwa ili Januari 9,waanze masomo,walikuja lakini siyo kwa wingi sana ambapo kuna Zaidi ya wanafunzi 300 bado hawajafika hii nafikiri kwa sababu watanzania bado tunachangamoto ya kujali muda wengine mpaka leo Januari 11, bado wanakuja kuchukua fomu za kujiunga na kidato cha kwanza ambapo ukiwauliza wazazi walikuwa wapi wamekuwa na sababu za hapa na pale,”anaeleza Mwl.Magabe.
Ametumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi ambao watoto wao bado hawajaripoti shule kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza shuleni hapo wawapeleke watoto wao shule kwani hawana sababu ya kubaki nao nyumbani kila kitu kimeisha andaliwa ata vitabu wameisha pokea kutoka serikalini.
Ambapo tamko la sera ya elimu ya mwaka 2014 inaeleza kuwa,Serikali itahakikisha vifaa, nyenzo na zana stahiki za kufundishia na kujifunzia katika elimu na mafunzo zinatosheleza kulingana na mahitaji na maendeleo ya sayansi, teknolojia na mbinu za kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote.
“Wazazi hawana sababu ya kubaki na watoto nyumbani waleteni waje wasome maana hakuna mchango wowote ambao atachangishwa ili mtoto kuingia darasani kwani madarasa mapya pamoja na samani zake vipo, tayari tumepokea na vitabu kwa ajili ya kufundisha na kujifunzia,zaidi ni kuwanunulia sare na madaftari,wawalete watoto ili wapate haki yao ya msingi ya kusoma,”.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Bujingwa wazungumzia ujenzi wa madarasa mapya
Mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Bujingwa Emmanuel Makaranga wa kidato cha nne,anaeleza kuwa serikali kuwajengea madarsa hayo imewasaidia kupunguza mrundikano kwa wanafunzi darasani.
Kwani darasani kuwa na mrundikano kunafanya mwanafunzi kutoelewa lakini kupitia madarasa hayo kutasaidia wanafunzi kuelewa zaidi kwani changamoto walizokuwa wanapitia kabla ya madarasa hayo kujengwa ni wanafunzi kutokuwa na mawasiliano mazuri kutokana na kurundikana.
“Mrundikano uliokuwepo darasani ulikuwa unasababisha kelele ambazo zilifanya wanafunzi kutolewa vizuri masomo pindi wanapofundishwa hivyo madarasa hayo yametusaidia sisi wanafunzi kuelewa zaid,”anaeleza Makaranga.
Juliana Aron wa kidato cha kwanza,anaeleza kuwa tangu aliporipoti shuleni hapo amekutana na miundombinu rafiki ya madarasa pamoja na viti na meza ambavyo vitawasaidia wao kusoma na kujielewa kwa bidi zaidi bila kubanana.
“Madarasa hayo yameongezwa na serikali ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi, napenda kuishukuru serikali na wadau wote walioweza kushiriki katika ujenzi wa miundombinu hii na tunaahidi tutasoma kwa bidi kwani miundombinu rafiki itatusaidia kusoma vizuri,”
Kwa upande wake Joyce Laurent wa kidato cha pili,anaeleza kuwa kuwepo kwa miundombinu hiyo ya madarasa mapya imesaidia shule kuwa na muonekano mzuri ambao umefanya wanafunzi kuhamasika kuhudhuria shuleni kwa ajili ya kusoma.
“Kabla madarasa haya hayaja jengwa wanafunzi wengi walikuwa hawahamasiki kuja shule na utoro ulikuwa kwa wingi ambao ulisababisha ufaulu wa shule kushuka,”
Baadhi ya wazazi waeleza namna ujenzi wa madarasa uliofanya na serikali ulivyo saidia wazazi na wanafunzi
Mmoja wa wazazi wenye watoto katika shule ya hiyo,Kilangi Mteminyanda,anaeleza kuwa amefurahi binti yake kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule hiyo kwani shule zimeboreshwa.
Anaeleza kuwa ujenzi huo wa madarasa umeleta nafuu kubwa kwa wazazi kwa sababu ukifikiria shule za binafsi mzazi analazimika kwa mwaka kulipa takribani milioni 3 lakini hizi za serikali mwanafunzi anasoma bure.
· “Serikali kuingilia na kuweka fedha zake katika ujenzi wa madarasa nchi nzima imetusaidia sisi wazazi kupata unafuu kiuchumi kwa sababu fedha ambayo tungechangia kila mzazi takribani 30,000 hadi 50,000,tunaitumia kwa maeneo mengine kwa ajili ya kuboresha hali za familia zetu
Hivyo kufuatia kuwa na madarasa hayo matarajio yao wazazi ni kuwa watoto watasoma bila kubanana na kwa uhuru,kwaio kitaaluma na kitaalamu watasoma kwa hewa na katika mazingira mazuri ambayo yatachangia wao kufundishwa na kufundishika vizuri hivyo kuboresha ufaulu.
“Tunamshukuru Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarsa takribani 8,000 kwa nchi nzima na kuwawezesha watoto wa wakulima kuweza kupata nafasi ya kupata elimu ambalo ni hitaji la msingi kwa wanafunzi wa kitanzania,”anaeleza Nteminyanda.
Nini matarajio ya wazazi kwa serikali baada ya ujenzi wa vyumba vya madarasa
Nteminyanda anaeleza kuwa matarajio yao kwa serikali baada ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ni kuongeza walimu na uwepo wa vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia shuleni ili elimu iweze kuwa bora zaidi na kuleta ufaulu mzuri kwa wanafunzi wa kitanzania.
Naye Rahma Ally,anaeleza kuwa ameiomba serikali kuendelaea na mpango wa kujenga vyumba vya madarasa kwa sababu bado wanafunzi ni wengi ambapo awali walikuwa wanakabiliwa na mrundikano darasani uliokuwa unasababisha wao kutokufanya vizuri katika masomo.
“Wanafunzi walikuwa wanafeli sana kwa sababu ya mrundikano darasani,unakuta darasa moja lina wanafunzi zaidi ya 100,hivyo hata walimu kuwafikia wote inakuwa ni mtihani,nashukuru baada ya haya madarasa watoto watapata elimu ya kutosha na kuongeza ufaulu,”anaeleza Rahma.
Aidha anaeleza kuwa mbali na ujenzi huo kuondoa mrundikano kwa wanafunzi darasani pia umesaidia wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kuchaguliwa kwa awamu moja(one selection), kujiunga kidato cha kwanza tofauti na awali walikuwa kulikuwa wakichaguliwa kwa awamu zaidi ya moja.
“Adha ya wanafunzi kuchaguliwa mara mbili imepungua kwasababu kipindi cha nyuma kulikuwa na awamu ya kwanza na ya pili ya wanafunzi kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini mwisho wa siku kwenye suala la mitihani haijalishi huyu mwanafunzi ni chaguo la kwanza au la pili wote wanafanya kwa wakati mmoja hiyo ilikuwa inachangia wanafunzi wengi wanashuka kwenye masomo yao na wanakuwa hawana ufaulu mzuri lakini kwa sasa hivi watakuwa na ufaulu mzuri kwa sababu wote wamechaguliwa na kuanza masomo kwa pamoja,”.
Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela azungumzia faida za madarasa hayo
Akizungumza na Timesmajira/Majira Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sylvester Mrimi,anaeleza kuwa Rais amewezesha shule 23 za sekondari zilizopo katika halmashauri hiyo kujenga vyumba vya madarasa 110,kwa kutupatia bilioni 2.2.
Kila chumba cha darasa kina madawati 50 ambapo utekelezaji wa mradi wa vyumba vya madarasa hayo kwa ajili ya kidato cha kwanza umewasaidia kwa asilimia 100, kwamba wanafunzi wanapata nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza.
“Kwa mwaka huu wa masomo hakuna nafasi ya wanafunzi waliochaguliwa kwa awamu mbili za masomo na hivi tunavyoongea tayari watoto wameripoti na kila mwanafunzi anaye ripoti shuleni anapata kiti na mezakwaio ni utekelezaji ambao umefanywa na serikali wa kuweka mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia kwa shule za sekondari,”anaeleza Mrimi.
Changamoto iliyokuwa inawakabili wanafunzi kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa
Mrimi anaeleza kuwa awali kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa uliokuwepo ililazimu wanafunzi kuchaguliwa kwa awamu mbili kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza.
“Huko nyuma kabla ya mwaka jana tulikuwa tunafanya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa awamu mbili kwa sababu tulikuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa,tukisha chagua awamu ya kwanza wale ambao wanakosa nafasi ilikuwa tunakimbizana kutafuta michango kwa wafadhili,wadau na wazazi ili muanze kujenga na mkisha kamilisha ujenzi ndio tunachagua wengine kwa awamu ya pili,”anaeleza Mrimi.
Anaeleza kuwa jambo hilo lilikuwa linakwamisha watoto wengine kufika shule kwa wakati kwa sababu muda ule ambao mnajiandaa kujenga vyumba vya madarasa unakuta wanafunzi wengine wamepotelea mtaani.
Pia walimu walikuwa wanapata ugumu kufundisha kwa sababu awamu ya kwanza ya wanafunzi inakuwa imeisha fika mbali kujifunza na awamu ya pili wanapo kuja katikati ya muhula wanakuwa na ujifunzaji ambao siyo mzuri.
Faida ya vyumba hivyo vya madarasa kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza
Mrimi anaeleza kuwa kupitia madarasa hayo kwa sasa hivi wanaanza mada na wanafunzi wote watakuwa sawa katika kiwango cha kujifunza na wana soma katika mazingira mazuri.
Uwiano wa madarasa na wanafunzi utakavyosaidia Halmashauri Kitaaluma
Mrimi anaeleza kuwa kwa uwiano huo wa wanafunzi na madarasa malengo na matarajio yao kiwango cha ufaulu kitaaluma katika halmashauri hiyo kitaongezeka.
“Kwa sababu watoto wote wapo katika mazingira salama na mazuri na walimu wetu wana nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na kwa ufanisi,kwaio ni motisha kwa wanaojifunza,imani yetu ni kwamba tutaenda kufanya vizuri zaidi na siyo tu kwa Ilemela naimani ni kwa nchi nzima,”anaeleza Mrimi.
Changamoto ya baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoripoti kwa wakati shuleni
Sera ya elimu ya mwaka 2014 inatoa tamko kwa Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika pamoja na Serikali itahakikisha kuwepo kwa mazingira bora na yenye usalama katika utoaji wa elimu na mafunzo nchini.
Mrimi anaeleza kuwa suala la baadhi ya wazazi kuwachelewesha watoto wao wa kidato cha kwanza kuripoti shule halmashauri hawatolivumilia na wameisha anza mkakati kwa maana ya vyombo vya matangazo vinapita kutangaza kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kuwa watoto waende shule.
Pia wamekaa na Ofisa Elimu Kata na viongozi wa mitaa kuhakikisha kuwa kila mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza anaripoti shule kwa sababu hakuna sababu ya msingi ambayo watamsikiliza mzazi ambaye ameshindwa kumleta mtoto shuleni.
Ambapo jambo analotakiwa kulifanya mzazi au mlezi ni kumnunulia daftari,kalamu na sare, hakuna usumbufu kwani suala la michango wamepiga marufuku kabisa hawataki kusikia mchango wowote shuleni,wamekuwa wakifuatia maelekezo ya Waziri Mkuu alioyatoa,hawataruhusu jambo hilo litokee.
“Kila shule tunaenda na tunapitia zile fomu za kujiunga kuhakikisha kwamba hatuitaji wala haturuhusu mzazi yoyote asumbuliwe,kabla hatujafungua shule tuliwasikiliza wazazi na walezi kama mzazi alidhani mtoto alipochaguliwa siyo mazingira rafiki na siyo karibu tumeisha tekeleza hilo la kubadilishia shule naimani kwamba wazazi wa watoto na walezi hawatakuwa na sababu yoyote ya kufanya mtoto asiripoti shule,”anaeleza Mrimi.
Pia anawasihi wazazi na walezi watambue elimu ndio mtaji na kinga kwa watoto hivyo wawaruhusu watoto waende shule ili wao waweze kuwasimamia walimu ili waweze kufundishwa vizuri huku kwa upande wao wasimamizi tumeisha kaa na walimu wao na wameisha waandaa na wapo tayari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Nawaomba waandishi wa habari kuwakumbusha wazazi wasiruhusu watoto wao kukaa nyumbani hata kama hajamshonea sare za shule husika kwani tumeruhusu kwamba wakati[U1] maandalizi ya ushonaji yanaendelea zile sare za shule alizokuwa anatumia katika shule za msingi waje nazo ili yale mafunzo ya awali wanayoanzia(English course orientation) yaendelee kufanyika kwa wote,”.
Hata hivyo anaeleza kuwa mwaka mpya wa masomo 2023,halmashauri hiyo ina jumla ya wanafunzi 12,500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa shule za sekondari 32 za serikali huku vyumba vya madarasa hayo yakijengwa kwa shule 23 za serikali ambazo ndizo zilizokuwa na uhaba.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kazungu Safari, anaeleza kuwa kipindi cha nyuma mwezi kama huo Watendaji wa Kata na mitaa wangekuwa wanasumbuana na wananchi kuchangisha shilingi 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa. Lakini kupitia fedha za serikali kazi imefanyika kwa muda mfupi wangeendelea na utaratibu ule ule wa kuchangishana wangechelewa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Massala, anaeleza kuwa kazi ya ujenzi wa vyumba hivyo 110 vya madarasa wameifanya takribani siku 45 hadi 50 huku kuwa,kuna takwimu ya vyumba vya madarasa vilivyojengwa na wananchi lakini havijamaliziwa ni kubwa lakini kwa mwaka wa fedha ulio isha zaidi ya vyumba 126 walivifanyia kazi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza,Elikana Balandya anaeleza kuwa Mkoa wa Mwanza ulipatiwa kiasi cha bilioni 19.66,kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 983 kati ya hayo madarasa 110 yamejengwa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Akizungumza mara baada ya kupokea vyumba hivyo vya madarasa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, ameeleza kuwa katika kupokea madarasa hayo ni mafanikio ya miaka miwili ya Rais ambapo mwaka jana pia walipokea madarasa kama hayo yaliotokana na fedha za uviko-19.
Anaeleza kuwa kwa wale wenye kumbukumbu kwa siku za mwisho za mwezi Desemba,wanajua kuwa kinakuwa ni kipindi kigumu sana cha kufukuziana,kukabana na kukasirikiana kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na uwenda yenyewe yangekuwa mawili au matatu.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika